Prime
HADITHI: Mwiba mdogo-6
ILIPOISHIA
Miaka mitatu baadaye tulianzisha uhusiano uliopelekea kushika ujauzito uliosababisha tufunge ndoa haraka kabla mtoto wetu wa kwanza hajazaliwa.
Endelea
Baada ya kuolewa nilihamia kambini kama mke wa mfanyakazi wa mgodi ule.
Pamoja na kufanya kazi kwenye mgodi, maisha yalikuwa magumu sana, siku zote mume wangu aliniambia siku akifanikisha dili lake ataacha kazi ile mara moja. Siku zote nilimpa moyo kuwa wakati bado, kwani wakati sahihi ni wakati wa Mungu.
Tangu tuoane tulikaa kama miaka sita mule kambini mpaka siku moja mume wangu alipotoweka ghafla. Hali ile ilinishtua sana na kutaka kujua mume wangu amekwenda wapi bila taarifa. Lakini siku ya tano tangu mume wangu atoweke ghafla alinipigia simu kuwa nimfuate Dar es Salaam.
Sikutaka kuhoji, siku iliyofuata nilipanda basi hadi Dar na kufikia kwenye hoteli moja ipo Manzese ambako tulikaa mwezi mmoja, kisha tulihamia Kinondoni Morocco.
Pale tulikaa kwa miezi sita kabla ya kuhamia kwenye nyumba yetu aliyojenga Tabata Bima ambako nako tulikaa miaka mitatu ndipo tukahamia hapa.”
“Samahani naomba nikurudishe nyuma,” Shila aliingilia mazungumzo.
“Bila samahani, unataka kujua nini?” mke wa marehemu alionyesha ni mtu mwenye hekima na busara.
“Unamfahamu marehemu Mchungaji Samweli?”
“Ndiyo.”
“Unamfahamu vipi?”
“Yule naweza kusema hakuwa rafiki tu bali ndugu wa damu, japokuwa hawakuzaliwa tumbo moja na mume wangu.”
“Mmejuana vipi na Mchungaji Samweli?”
“Huwezi kuamini maisha haya yana siri kubwa, hujui kesho ya mtu bali siri ya Mungu, shemeji Samweli kabla ya kuwa mchungaji kama alivyokuwa mume wangu, wote walikuwa wakifanya kazi pamoja, yeye akiwa fundi wa mitambo pale mgodini na mume wangu kwenye uchenjuaji wa madini.”
“E’he.”
“Kuna kitu cha ajabu kilitokea kwa watu sita ambao kabla ya kufanikiwa kwao walikuwa karibu, muda wa jioni baada ya kazi walikuwa pamoja walizungumza kwa muda mrefu mpaka saa tano usiku. Kisha kila mtu alienda kwake kulala mpaka siku ya pili.
Ile hali iliendelea kwa siku mbili mpaka walipotoweka ghafla na siku nilipokuja mjini niliwakuta wote wakiwa kwenye sherehe ya kula na kunywa kasoro mtu mmoja, shemeji Hanzuruni.”
“Kwa nini hakuwepo?”
“Niliwauliza waliniambia yeye hakuwepo ana udhuru.”
“Huyo Hanzuruni kwa sasa yuko wapi?”
“Mmh! Baada ya wiki mbili nilipata taarifa za kukutwa mwili wa shemeji Hanzuruni kuuawa kinyama kwa kuchomwa visu vingi mwilini.”
“Unafikiri kwa nini alikufa peke yake hata katika sherehe ya kugawana pesa hakuwepo.”
“Mume wangu alinieleza kuwa baada ya kila mtu kupata pesa zake za mgawo wao, pesa zao waliingiza benki, ila yeye aliondoka na pesa zake na kulala nazo nyumba ya wageni.
Majambazi walipojua ana pesa nyingi walimvamia na kumuua kisha kuchukua pesa zote, kitu kilichopelekea mkewe kupata uchizi wa kupoteza kiasi kikubwa cha pesa na pia kumpoteza mumewe.”
“Mkewe mlikuwa mnafahamiana?”
“Ndiyo, tulikuwa karibu sana kama majirani.”
“Nini kiliendelea baada ya kupata uchizi?”
“Alipelekwa Hospitali ya Muhimbili wodi ya wagonjwa wa akili.”
“Uliwahi kwenda kumtazama?”
“Nilikwenda siku moja mbona nilijuta, nilipofika alinivamia na kunikaba nusura anitoe roho, huku akisema lazima tutalipa damu ya mumewe haitamwagika bure, kwa kweli bila madaktari kumshika kisha kumpiga sindano ya usingizi, angeniua.”
“Unafikiri kwa nini alisema mtalipa damu ya mumewe haitamwagika bure?”
“Niliporudi nyumbani nilimuuliza mume wangu, alinieleza kuwa mke wa Hanzuruni anaamini wao ndiyo waliomzunguka na kumuibia pesa zake na kumuua. Nilimuuliza mume wangu kuna ukweli gani? Alinieleza yule mwanamke amechanganyikiwa baada ya kumpoteza mumewe na kiasi kikubwa cha pesa.
“Unaweza kuniambia kuna siri gani ya kifo cha mumeo na mchungaji?”
“Kwa kweli siwezi kujua zaidi ya kile nilichokueleza ambacho nakijua.”
“Huoni kama kuna siri ya watu watano, akiwepo mumeo na mchungaji na kifo cha Hanzuruni?”
“Kwa kweli baba yangu nje ya nilichokueleza sijui chochote.”
“Kuna taarifa yoyote kuhusu mke wa marehemu Hanzuruni uliisikia tangu siku ulipokwenda kumuona hospitali?”
“Mmh! Kuna siku mume wangu alinieleza mke wa Hanzuruni amefariki kwa sonona baada ya kushindwa kuhimili yaliyomtokea.”
“Nasikia alikuwa na mtoto mdogo, ninyi kama watu wake wa karibu mlichukua jukumu gani kumlea?”
“Msema kweli kipenzi cha Mungu, Mume wangu alikataa kwa kuamini kama tutamchukua anaweza kutugeuka akiamini tumewaua wazazi wake.”
“Hao watatu ni kina nani na wapo wapi na wanashughulika na nini?”
“Mmoja anaitwa Alhaji Swaleh Bashir, yeye ana asili ya kichotara, kwa sasa anamiliki kituo cha misaada kwa wajane, watoto wanaoishi katika mazingira magumu na mayatima. Ni mtu maarufu sana ambaye pia kila mwaka husafirisha watu 10 kwenda hija akisaidiana na watu wa Oman. Pia ni mmoja ya wafadhili wa misikiti mingi jijini na mikoani.
“Mwingine.”
“Ni Joseph Maliki, mmiliki wa makampuni ya mafuta yanaitwa JOIL ambayo yanasambaza mafuta nchini na nchi za jirani, pia ana magari zaidi ya 200 ya kusambaza mafuta na kusafirisha mizigo.”
“Huyo namjua, mmh! Inaonekana waliuza mzigo wa mabilioni ya pesa.”
“Ndivyo inavyoonekana, maana katika watu wote sita kila mmoja maisha yake yalibadilika ghafla, ambao mpaka sasa wana maisha mazuri sana hata sijui waligawana kiasi gani kila mmoja.”
“Wa mwisho?”
“Anaitwa Seba Mabula, ambaye yeye baada ya mgawo wake alirudi kwao Mwanza, kwa kweli taarifa zake sina kwa vile tangu aondoke alikuja mara moja tu. Yeye hakuwa muongeaji, kitu kilichofanya nisiwe naye karibu kama wenzake.”
“Asante na....,” kabla ya kumalizia sentesi simu yake iliita, ilikuwa ya kibandani kuonyesha mpigaji ni mtu makini.
Kabla ya kupokea alituma zile namba Mamlaka ya Mawasiliano kujua mpiga simu yupo wapi. Baada ya dakika tano alijulishwa kibanda cha simu kipo Kinondoni, haraka aliwatuma vijana wake kufuatilia kile kibanda cha simu kilichokuwa Kinondoni B.
“Mbona hupokei?” mke wa Balize aliuliza.
“Hizi simu hazina usalama, huenda mmoja wa washirika wa mumeo ameuawa.”
“Mmh! Makubwa, sasa kwa nini anafanya hivyo?”
“Siri wanaijua wahusika, hiki ni kisasi cha jino kwa jino.”
“Jino kwa jino unamaanisha nini?”
“Muuaji amejinasibu kila limkutalo linamhusu.”
“Au...hapana sidhani, mawazo yangu siwezi kukubaliana nayo kwa vile pesa waliyogawana ni nyingi.”
“Unawaza nini?”
“Sasa naanza kuingiwa na wasiwasi, kuna siku mume wangu alivamiwa na mwanamke kichaa ambaye alimjeruhi vibaya na kisu na kusababisha kupoteza jicho moja.”
“Ha! Nini kiliendelea?”
“Nakumbuka baada ya mume wangu kwenda kutibiwa Afrika ya Kusini ambako alikaa mwezi mmoja na kurudi nyumbani, waliitana wanne kasoro shemeji Mabula na kuzungumza kwa muda mrefu, sikujua kikao kile kilihusu nini.”
“Wewe wasiwasi wako nini?”
“Labda walimdhuru Hanzuru...”
Mke wa Balize alinyamaza baada ya simu ya mkuu kuita tena, namba ilikuwa nyingine.
Aliitazama kabla ya kuipokea kitu kilimfanya mke wa Balize kuuliza tena.
“Mbona hupokei, hebu pokea ujue anataka kuueleza nini?”
“Amebadili eneo, huyu atakuwa amejipanga kweli.”
“We pokea tu bila hivyo mtakesha.”
Shila alipokea simu kwa sauti iliyopoteza kujiamini:
“Haloo.”
“Baba,” sauti ile ilionyesha kabisa mambo yameharibika.
“Mwanangu,” alijibu kwa sauti ya upole kutaka huruma ya mpigaji asiwe ameharibu tena.
“Baba yangu pole sana najua nakusumbua, bado kazi mbili nawe upumzike.”
“Ehe una taarifa gani?”
“Alhaj....”
“Alhaj Swaleh Bashir,” Mkuu Shila alimalizia.
“Ewaaa, sasa baba tunakwenda vizuri, tunaweza kwenda sawa, mwili wake upo ofisini kwake Kigamboni.”
“Binti kwa nini unaua hata kama wamekukosea kwa nini usiwaripoti polisi.”
“Kwanza hakuna ushahidi wa kuwatia hatiani, pili kufuata sheria ndiko kulikompoteza kipenzi mama yangu kuuawa kwa sumu na aliyetumwa kumuua yeye nitamalizana naye mwisho.”
“Wewe binti unajiamini vipi?”
“Kwa vile hata nikifa sina faida, nimewapoteza wazazi wangu mimi nani niogope kufa.”
“Usijisahaulishe mkono wa jeshi mrefu.”
“Sawa najua, unasema hivyo kwa vile nimekueleza lakini fanya kazi yako nami nifanye yangu, kukutaarifu ni kukupunguzia kazi ya kuuchukua mwili wa marehemu haraka.
“Sitaki mtu afe na mwili wake kugundulika kwa harufu baada ya kuharibika kwa sumu kali. Japo nipo katika haki ya Mungu, lakini mtu akifa kuzikwa haraka ni haki yake,” baada ya kusema vile simu ilikatwa.
“Vipi kuna taarifa gani?”
Unaweza kufuatilia hadithi hii kupitia tovuti yetu ya Mwananchi na kusikiliza kwa njia ya sauti kupitia Mwananchi Digital kwenye Youtube
Itaendelea Ijumaa.