Prime
HADITHI: Mwiba mdogo-5
ILIPOISHIA JANA
“Ni kazi tuliichagua, hatuna budi kutumikia, ninyi mabosi wetu.”
Endelea..
Mpelelezi Mkuu Shila aliagana na wafiwa na kuingia kwenye gari kuelekea Mikocheni B kwa mzee George Balize aliyeuawa muda mfupi. Njiani alizidi kujawa na mawazo juu ya mauaji yale, mwanzo alifikiria huenda ni vita ya kiimani iliyosababisha Mchungaji Samweli kuuawa kutokana na sifa zake katika huduma za kiroho.
Lakini maneno aliyoyasema muuaji anayejiita mtoto wa marehemu ambaye analipa kisasi cha wazazi wake, ilionyesha kuna kundi la watu waliofanya unyama wa kuidhuru familia ya muuaji na kuonyesha sehemu kubwa ya mali za aliouawa zinatokana na dhuluma.
Mpelelezi Shila aliamini kama Mchungaji Samweli alikuwa anafanya kazi katika migodi kama fundi wa mitambo, ghafla ameweza kuwa na pesa za kujenga kanisa kubwa, wazo lake lilikuwa huenda pesa alizojengea kanisa alitoa kwenye pesa za mgodini. Lakini alibakia na maswali kama walivusha madini na kuyauza iweje mmoja auawe na wengine wagawane bila tatizo.
Aliamini kupitia mazungumzo yake na mke wa marehemu angepata mwanga ili kuunganisha doti maisha ya awali ya Mchungaji yana ukaribu gani na wa tajiri Balize.
Taratibu alianza kupata picha kamili ya maelezo ya mtoto wa marehemu na watu waliouawa.
Mkasa ule aliufananisha na wa Manka kwenye Operesheni Rwanda ambaye alilipa kisasi cha mumewe, lakini kwa mtoto wa marehemu kisasi cha wazazi wake.
Kabla ya kutoka Mbezi aliwasiliana na askari wa barabarani ili kumsafishia njia.
Njia aliyopita akitokea Mbezi haikuwa na foleni mpaka anafika Mikocheni B. Eneo la tukio kulikuwa kumewekwa uzio wa tahadhari na kuwafanya watu wasimame kwa umbali na kuwaacha askari wafanye kazi yao.
Alipofika aliteremka kwenye gari na kutembea kuelekea eneo la tukio ambako bado mwili wa marehemu ulikuwa haujatolewa.
Kwa vile kulikuwa na giza iliwashwa tochi na kuumulika, ulikuwa hautamaniki.
Damu ilimtapakaa mwili mzima na mwili ulikuwa hautamaniki kwa kutobolewa na kisu.
Aliwaeleza vijana wake wachukue picha ya mazingira kisha aliwaacha polisi wauchukue mwili na kuupeleka hospitali ya Muhimbili.
Kwa vile tukio lile lilitokea muda mfupi, aliamini haukuwa muda mwafaka wa yeye kuzungumza na wafiwa ambao bado wapo kwenye maumivu makali ya kufiwa na mume kipenzi na baba wa familia.
Alipanga kurudi siku ya pili ambayo kidogo itakuwa imetulia na kuweza kuzungumza naye.
Aliondoka kurudi ofisini makao makuu ya polisi ili kuzungumza na vijana wake wamepata nini baada ya kuzunguka maeneo waliyoelekezwa.
Mwili ukiwa umechoka kwa mizunguko ya kutwa nzima, aliingia ofisini ambako aliwakuta vijana wakimsubiri, alipoingia wote walisimama.
“Kaeni chini.”
“Asante,” walijibu kwa pamoja.
Baada ya kukaa chini palipita kimya kifupi kabla ya kuanza kikao, Mpelelezi Mkuu Shila alikumbuka sekretari wake Suzana hajaondoka. Wakati huo Suzy naye alikuwa akiingia ofisini na kikombe cha kahawa.
“Karibu mkuu.”
“Asante, Suzy unaweza kwenda, mwambie John akupeleke nyumbani tuonane kesho.”
“Asante mkuu,” Suzy alibana mikono na kugeuka kikakamavu na kutoka nje kuacha kikao kiendelee.
Baada ya Suzy kutoka Mkuu alipiga funda tatu za kahawa kisha aliweka kikombe mezani na kuiacha kahawa iteremke. Alikohoa kidogo kuiandaa sauti yake na kuyaandaa masikio ya vijana wake kumsikiliza.
“Habari za muda huu?” alianza kuwasalimia.
“Nzuri mkuu,” waliitikia kwa pamoja.
“Nina imani mnahitaji maelezo yangu ili nanyi mchangie.”
“Sawa mkuu,” waliitikia kwa pamoja.
Mkuu Shila aliwaeleza toka taarifa ya awali ya kifo cha mchungaji na taarifa alizozipa usiku ule kabla ya kupata taarifa za kifo cha Balize.
Baada ya kuzungumza kwa muda mrefu aliwageukia vijana wake na kuwauliza.
“Nina imani mmenisikiliza kwa makini, mnaweza kuniambia mmegundua kitu gani?”
“Mkuu.” Alianza Sele.
“Naam Sele.”
“Mkuu kutokana na maelezo ya pande mbili ulizozisikiliza inaonyesha kulikuwa na kundi la watu sita walifanya dili moja la pesa nyingi, watu watano waliungana kumuua mwenzao na kugawana hizo pesa.”
“Mawazo yako kama yangu.”
“Mkuu.”
“Eeh Ibra.”
“Mkuu inaonekana kabisa hii issue imefanyika mgodini, inawezekana kabisa watu watano wa ndani na mmoja wa nje ya mgodi, hivyo wameungana kumdhulumu na alipowadai walimgeuka na kumfutilia mbali.”
“Nawe pia umeonesha mwanga.”
“Mkuu.”
“Ndiyo Jimmy.”
“Mkuu kwa kuongezea inaonekana hawa watu walikuwa wakifanya kazi mgodini, baada ya kupata madini na kuyauza ambayo yaliwapa pesa nyingi na kuamua kuachana na kazi ya uchimbaji madini kila mmoja alitafuta njia yake ya maisha kwa Mchungaji Samweli kuchagua kumtumikia Bwana na Balize kugeukia biashara.”
“Well done, vichwa vyenu vinafanya kazi vizuri, nina imani hakuna aliyekwenda nje ya mawazo yangu na kwenda mbele zaidi. Mnafikiria nini tufanye?”
“Mkuu, inavyoonesha kabisa muuaji ni mtu aliyejipanga vizuri, huenda anatujua vizuri sana, pia anajua muda gani tupo wapi, hivyo basi hutekeleza kazi yake kwa uhuru.”
“Ndiyo maana tumechagua kazi hii ngumu tutatue vitu vigumu kama hivi.”
“Ni kweli mkuu, kazi kubwa ipo kwenye kuijua sura ya muuaji ambaye ni mzoefu, ila kuna jambo moja muhimu tunatakiwa kulifanya kwa haraka.”
“Lipi hilo?”
“Kuwahi kujua nani katika watu hao watatu waliobakia kwa vile hatujui ni nani na lini amepanga kuua mwingine.”
“Mkuu umesema mke wa Mchungaji ni msichana tofauti na umri wake, hivyo amemkuta tayari ni mchungaji hivyo hawezi kujua siri ya nyuma ya mumewe.”
“Kesho ukienda kwa mke wa mzee Balize anaweza kutujuza nani rafiki wa zamani wa mumewe.”
“Nina imani itatusaidia kuwajua marafiki wake wa miaka kumi na nane iliyopita.”
“Nina imani tuna kazi kubwa ya kufanya kesho kabla ya jioni tuwe na majibu kamili juu ya kumjua muuaji na watu walio kwenye kwenye foleni ya kifo.”
“Sawa mkuu.”
Mkuu Shila aliagana na vijana wake na kubakia ofisini kwa ajili ya kuwasiliana na vijana wake waliokwenda kumfuatilia mwanamke albino mwenye ujauzito.
Alijikuta akitoka ofisini saa saba za usiku na kurudi nyumbani kupumzika kwa ajili ya kazi nzito ya saa chache kabla ya kupambazuka.
Siku ya pili mkuu Shila alikwenda nyumbani kwa marehemu Balize ili aweze kuzungumza na wafiwa apate mawili matatu ambayo yataonesha mwanga wa tukio lile la mauaji. Alipofika nyumbani kwa mzee Balize alikuta maandalizi ya msiba, pia watu hawakuwa wengi kwa vile ilikuwa bado asubuhi.
Alikaribishwa kwa heshima zote, kwa vile alikuwa pale kikazi hakutaka kupoteza muda, aliomba kukutana na wafiwa. Wa kwanza aliomba kukutana na mke wa mzee Balize, alikutanishwa na mwanamke mmoja wa makamo kuonyesha mke wa marehemu alikuwa ndani ya ndoa kwa muda mrefu, tofauti na mke wa mchungaji pamoja kuwa mtu mzima, mkewe alikuwa binti mdogo.
Kwa umri wa mke wa marehemu, aliamini historia ya mume wake itakuwa na mwanga mkubwa kujua harakati za mumewe tangu ujana wao mpaka kuwa watu wa makamo wenye watoto na wajukuu.
“Karibu baba.”
“Asante, pole na msiba.”
“Asante ni mapenzi ya Mungu.”
“Samahani naomba nikuulize juu ya historia fupi ya marehemu.”
“Hakuna tatizo, uliza chochote ukitakacho.”
“Wewe na marehemu mna muda gani kwenye ndoa yenu kabla ya kufikwa na mauti jana usiku?”
“Mmh! Mwanangu ndoa yetu ina miaka thelathiini na saba.”
“Hongera ni muda mrefu sana.”
“Asante, nina imani bila kifo cha ghafla tungetembelea mkongojo pamoja.”
“Naomba unieleze historia ya marehemu kwa ufupi mlianzia wapi mpaka mpo hapa.”
“Miaka arobaini iliyopita mume wangu alikuwa akifanya kazi kwenye machimbo ya Tanzanite upande wa uchenjuaji madini. Wakati huo mimi nilikuwa nasoma na naishi kwa dada yangu pale Mirerani.
“Basi kila nilipokuwa nikienda palemachimboni nilikutana na mume wangu ambaye tulianzisha uhusiano. Miaka mitatu baadaye tulianzisha uhusiano uliopelekea kushika ujauzito uliosababisha tufunge ndoa haraka kabla mtoto wetu wa kwanza hajazaliwa.”
Itaendelea