Prime
HADITHI: Mwiba mdogo-7
![](/resource/image/4848082/landscape_ratio2x1/320/160/4a2cb5d2570b36db4d8883675da62444/fU/hadithi-pic.jpg)
“Alhaji Swaleh Bashir ameuawa ofisini kwake Kigamboni.”
“Mungu wangu! Tumekwisha, akiwamaliza si atatugeukia na sisi?” mke wa Balize aliuliza kwa taharuki.
“Wala, yeye anadili na waliohusika kumuua baba yake na mama yake tu.”
“Mmh! Sasa nimeanza kuielewa kauli ya mke wa Hanzuruni, inawezekana kabisa kifo cha Hanzuruni hakikuwa kama nilivyoelezwa bali kuuawa na mume wangu na washirika wenzake?”
“Inawezekana muuaji amepania, inaonyesha ni binti mdogo akishirikiana wa watu wenye kazi hiyo ya kijasusi.”
“Basi huyo atakuwa binti wa Hanzuruni ambaye mume wangu alijua lazima atalipa kisasi.”
“Sasa naomba nikuache ili nifike Kigamboni, naomba mazungumzo yetu yabakie siri, la sivyo utawatia taharuki familia yako.
“Sawa baba.”
“Ukiwa na jambo lolote unalolijua utanijuza.”
“Sawa.”
Mkuu Shila aliingia kwenye gari na kuelekea Kigamboni maeneo ya Gezaulole, ambako kulikuwa na kituo kikubwa cha Alnuru chenye ghorofa tatu na eneo kubwa la nyumba za kulala watoto, madarasa ya elimu ya kidunia na dini kwa watoto na viwanja vya michezo.
Kitu kingine kilichomshitua ni ramani ya jengo kuu lilikuwa sawasawa na ramani ya kanisa la Mchungaji Samweli, pia inaonekana mjengaji alikuwa mmoja. Hakika eneo lilikuwa kubwa na limependeza sana kwa unadhifu, majengo na watu wake.
Alipofika alishangaa kuona mazingira ya pale kila mmoja akiwa bize kuonyesha hakuna mtu yeyote alikuwa akijua kimetokea kitu gani. Waliulizia ofisi ya mkurugenzi wa kituo kile na kuelekezwa.
Walipanda hadi ghorofa ya kwanza kwenye ofisi ya vioo vitupu, hali ya hewa ilikuwa ikivutia kwa manukato mazuri ya ndani. Walipokewa na binti aliyekuwa amevalia vazi la hijabu nyuma ya kompyuta.
“Karibu ofisa.”
“Mheshimiwa nimemkuta?”
“Ndiyo.”
“Mjulishe Juma Shila nipo hapa.”
“Hakuna tatizo.”
Binti alinyanyua mkonga wa simu na kumpigia bosi wake, lakini ilionyesha simu ya ndani mkonga wake umewekwa pembeni.
“Inaonekana mkonga haupo juu ya simu.”
“Hiyo inamaanisha nini?”
“Mara nyingi akiwa na kazi nyingi huwa hapendi usumbufu.”
“Hii hali hutokea mara ngapi?”
“Hasa ukikaribia wakati wa hija.”
“Kwani kipindi cha hija si bado miezi sita.”
“Hata mimi nashangaa, ngoja nimfuate ndani nijue anafanya nini ili niwajuze.”
“Ngoja kwanza, leo umepokea wageni wangapi toka asubuhi?”
“Mmh! Mmoja.”
“Yupo vipi?”
“Binti mmoja amevaa vazi la heshima lililouziba mwili wake na kubakiza usoni chini ya pua na miwani nyeupe. Alipofika nilielezwa na bosi kuwa apite kwa vile alikuwa na miadi naye. Baada ya kuingia bosi alinipigia simu kuwa ana kazi maalumu na mgeni wake haruhusiwi mtu yeyote kuingia ndani.”
“Mgeni alitoka baada ya muda gani?”
“Yule mgeni alitoka baada ya saa moja na nusu na kuniaga kuwa nisiingie mpaka aniite, nami nimetii amri sijaingia mpaka sasa.”
“Mmh! Kazi ipo,” mkuu alisema huku akifuta jasho juu ya pua kwa kitambaa.
“Vipi, kuna nini?” Sekretari wa Alhaji Swaleh alishtuka.
“Kuna tukio ofisini kwa bosi wako tunakuomba uwe tayari kwa tutakachokikuta.”
“Amefanya nini tena?” hofu ilizidi kumpanda.
Waliongozana hadi ndani ya ofisi na kukutana na tukio la kutisha ambalo halikuwa tofauti na la Mchungaji Samweli. Alhaji Swaleh alikuwa amelalia meza akitokwa na damu puani, masikioni, machoni na mdomoni huku ulimi na macho vikiwa vimetoka pima.
Baada ya kuchukua ushahidi wa kimazingira waliuchukua mwili na kuupeleka hospitali kwa uchunguzi zaidi. Wakati huo familia yake ilikuwa imeshapewa taarifa.
Mkuu Shila hakutaka kupumzika, kwa vile Joseph Mkiki alikuwa na namba yake alimpigia na kupokelewa upande wa pili.
“Haloo Joseph salama?”
“Salama mkuu.”
“Una taarifa gani za rafiki zako?”
“Hapa nilipo nimechanganyikiwa hata nje naogopa kutoka, wasiwasi wangu huenda hata nikifika msibani nikauawa.”
“Kwa sasa upo wapi?”
“Nipo nyumbani.”
“Nakuja sasa hivi usitoke nimetuma ulinzi nyumbani kwako na ofisini.”
“Nashukuru hata sijui nini kimetokea.”
“Mengi tutazungumza nikifika kwako.”
“Sawa mkuu, mimi na familia yangu tumejifungia ndani siruhusu hata paka kuingia tulipo.”
Mkuu Shila aliwasha gari na kuelekea Masaki alipokuwa akiishi Joseph, nyumba ilikuwa ufukweni ya ghorofa moja. Alipofika alikuta ulinzi mzuri uliompa moyo. Baada ya kufunguliwa geti na kuingiza gari ndani alipokelewa na Joseph ambaye alipungua mwili kwa saa chache za hofu, kweli maisha matamu.
“Karibu mkuu.”
“Asante.”
Waliingia ndani hadi sebuleni, kabla ya kuanza mazungumzo alikuja binti mrembo na kuuliza.
“Samahani mgeni unatumia kinywaji gani?”
“Kahawa ya maziwa.”
“Nami niletee kama mkuu wangu,” alisema Joseph.
Binti aliondoka kuelekea jikoni na kufanya Shila kujiandaa kumhoji.
Kabla ya kuanza kumhoji kahawa ya maziwa ililetwa vikombe viwili na kuwekwa kwenye meza ndogo. Baada ya kuwapatia kahawa aligeuka na kuondoka na kuwaacha waendelee na mazungumzo.
“Karibu kahawa mkuu,” Joseph alimkaribisha mpelelezi mkuu Shila.
“Asante,” alisema huku akichukua kikombe cha kahawa na kukipeleka mdomoni na kupiga funda mbili na mwenyeji wake naye kufanya vilevile kwa kupiga funda mbili kisha alirudisha mezani ili amsikilize mgeni wake.
“Joseph.”
“Naam mkuu.”
“Hivi marehemu Mchungaji Samwel, marehemu Balize na marehemu Alhaj Swaleh..”
“Wee usiniambie! Alhaj Swaleh naye amekufa lini na saa ngapi. Asubuhi nilikuwa nimezungumza naye na kumpa taarifa za vifo vya Mchungaji Samwel na Balize.”
“Kifo chake kimetokea muda mfupi hivi natoka Kigamboni kuchukua mwili wake na kuupeleka hospitali kwa kuuhifadhi na uchunguzi zaidi.”
“Tumekwisha! Tumekwishaaa! Haya niliyajua mapema niliwakatalia, lakini ubabe wa Balize ndio umeyazaa yote haya. Niliwaeleza haya wakadharau sasa yanatutokea puani, siku zote tamaa inaponza kichwa,” Joseph aliitoa siri bila kujua anamwaga mtama kwenye kuku.
“Tamaa gani?”
“Kafara ya damu ndiyo iliyotufikisha hapa.”
“Kafara ya damu inahusiana nini na mauaji haya?”
“Aa..aa..unajua sote tulifanya dili la pesa ambalo lilituwezesha kupata pesa nyingi sana la..lakini mwenzetu Balize kumbe alikuwa na siri nyingine ambayo ndiyo sababu ya mauaji haya.”
“Ukisema kafara ya damu unamaanisha nini na inahusianaje na mauaji haya?”
“Hii ni siri nzito ambayo haikutakiwa mtu yeyote kuijua la..la..laa...” hakuendelea kuzungumza, ghafla maneno yakawa hayatoki vizuri, mikono yake ikawa inaupapasa mwili upo kama kuna kitu kinamuuma. Macho yalianza kuwa makubwa na damu kuanza kumtoka, alianza kuunguruma, kujishika usoni kama uso unawaka moto.
Shila kwa mara ya kwanza aliuona mchezo mubashara na kufanya atetemeke kwa kuamini sumu ilikuwa kwenye kinywaji. Alishuhudia mbele ya macho yake Joseph akiteseka, ulimi ulimtoka pima huku damu zikimtoka mdomoni masikioni na puani.
Alijinyonganyonga akiwa ameegemea kochi kuonesha yupo kwenye mateso mazito yenye maumivu makali sana. Aliendelea kuteseka kwa maumivu makali.
Mkuu Shila kila alipotaka kupiga simu alijikuta akiishiwa nguvu na kubakia akishuhudia Joseph akifa kifo cha kikatili sana. Baada ya mateso ya dakika tano alitulia akiwa amekata roho.
Mkuu Shila akawa haamini alichokiona mbele ya macho yake huku woga ukimtawala.
Baada ya akili kutulia alishituka kama anatoka usingizini na kupiga simu kuwaita vijana wake ambao walikuwa wameimarisha ulinzi mkubwa na gari la wagonjwa.
Alijiuliza muuaji alijuaje kama atakwenda pale na amewezaje kuingia pamoja na ulinzi mzito uliokuwepo pale. Ile hali ilimtisha sana na kuona jinsi gani muuaji ana uwezo wa hali ya juu.
Aliamini kabisa dada wa kazi ndiye aliyeleta vinywaji hivyo, alikuwa anajua kilichokuwa kikiendelea. Wakati huo sauti za vilio zilikuwa zikivuma ndani ya jumba la tajiri Joseph.
Gari la wagonjwa lilifika na kuuchukua mwili wa marehemu na kuondoka nao.
Wakati huo dada wa kazi alikuwa amezirai baada ya kifo cha bosi wake ambacho alijua yeye ndiye sababu. Baada ya kupata fahamu alianza kulia huku akisema:
“Ndiyo, wakati naandaa maziwa jikoni alikuja na kunieleza kikombe hiki nimpe baba na hiki nikupe wewe.”
Unaweza kufuatilia hadithi hii kupitia tovuti yetu ya Mwananchi na kusikiliza kwa njia ya sauti kupitia Mwananchi Digital kwenye Youtube
Itaendelea kesho.