Sitta ahaha kulinusuru Bunge Maalumu la Katiba

Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akizungumza kwenye kikao
cha Bunge hilo juzi, alipokuwa akieleza masikitiko yake baada ya Kundi la Ukawa kugoma kuhudhuria vikao vya Bunge mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Habari ambazo zimelifikia gazeti hili zilisema Sitta anawasaka viongozi wa Ukawa kwa lengo la kukaa nao katika meza ya mazungumzo, kutafuta maridhiano yatakayowezesha kundi hilo kurejea bungeni.

Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta anahaha kulinusuru Bunge hilo, baada ya wajumbe ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vinavyoendelea mjini Dodoma.

Habari ambazo zimelifikia gazeti hili zilisema Sitta anawasaka viongozi wa Ukawa kwa lengo la kukaa nao katika meza ya mazungumzo, kutafuta maridhiano yatakayowezesha kundi hilo kurejea bungeni.

Sitta jana aliliambia Mwananchi kuwa wako njiapanda, kwa sababu hawafahamu kama wajumbe hao wa Ukawa wametoka tu nje ya ukumbi na watarudi au wamejiuzulu.

“Hapa ninapozungumza na wewe nimesitisha kwenda mapumziko ya Pasaka… Nimewapigia simu Lipumba (Ibrahim) na Mbowe (Freeman), lakini hawapokei simu,” alisema Sitta na kuongeza;

“Niliyempata ni Mbatia (James) peke yake na ameniambia yeye yuko na wenzake na hana uamuzi wa pamoja…Nataka nikutane nao ana kwa ana nasubiri kama inawezekana tufanye mazungumzo.”

Aliongeza: “Nasubiri hata kama watatuma mwakilishi wao tukae tuzungumze hili jambo, lakini mpaka sasa sijaona mwakilishi yoyote…huwezi kuamini sijaenda Pasaka niko hapa Dodoma.”

Sitta alisema pamoja na viongozi hao wawili wakuu wa Ukawa hawapokei simu, lakini amefanya jitihada ikiwamo kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), lakini hadi jana mchana alikuwa hajajibiwa.

“Sitaki kuongeza chochote kuhusu hili jambo kwa sababu kwa mazingira yenyewe nikisema chochote ninaweza kuharibu japo nina maoni yangu binafsi kuhusu hili, lakini sitaki kusema sasa,” alisema Sitta.

Jana gazeti hili lilimtafuta Mbatia ambaye alikiri kuzungumza na Sitta. “Ni kweli amenipigia simu na nimemwambia kwamba nimemsikia, lakini siwezi kufanya uamuzi peke yangu, lazima nishuriane na wenzangu.”

Hata hivyo, Mbatia alisema kwa mtizamo wake hadhani kama Sitta anaweza kutatua mvutano uliopo na kwamba wanaopaswa kusimamia suala hilo ni viongozi wa vyama vya siasa vinavyovutana.

“Mimi naamini katika maridhiano, lakini vyama vya siasa ndivyo vinaweza kutatua mzozo huu, kwa hiyo viongozi wa CCM ndiyo wanaweza kuonyesha nia ya kuzungumza, Sitta ni kiongozi wa Bunge ambaye kazi yake ni kusimamia uendeshaji wa vikao, hivyo suala la maridhiano kwake ni kumtwisha mzigo mzito ambao hapaswi kuubeba,” alisema Mbatia.

Kanuni za uendeshaji wa Bunge hilo za 2014, zinasema kuwa ili ibara au Rasimu ya Katiba iweze kupitishwa itahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe kwa pande zote za Muungano.

Kanuni ya 37 (1), inasomeka: “… ili ibara au Rasimu iweze kupitishwa itahitaji kuungwa mkono na wingi wa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili toka Zanzibar”.

Taarifa zisizo rasmi zinasema ili kuwezesha kupatikana kwa theluthi mbili kutoka upande wa Tanzania Visiwani CCM walikuwa wakihitaji kupata kura 16 ikilinganishwa na idadi yao ya sasa ya wanaounga mkono.

Kamati ya Uongozi

Harakati zinazofanywa na Sitta zimekuja saa chache tangu kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu, ambacho habari zinasema kilimwelekeza kiongozi huyo kufanya jitihada za kutatua mgogoro uliopo.

Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad alisema kikao cha Kamati ya Uongozi hakikufikia uamuzi kuhusiana na wajumbe wanaounda Ukawa kutoka bungeni kwa sababu hawajapata taarifa ya nini kilichowafanya waondoke.

“Hakuna cha kushika hapa, hatukujua kwa nini walitoka bungeni lakini Mwenyekiti (Sitta) alikuwa akiwatafuta ili kujua sababu za kutoka kwao bungeni,” alisema Hamad na kuongeza: “Mwenyekiti anawatafuta na tulikubaliana wakipatikana atatuita ili tuzungumze,” alisema Hamad.

 Hamad alimnukuu Sitta kuwa milango iko wazi kwa Ukawa kwa mazungumzo. Pia alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda yuko tayari kuzungumza nao ili kufikia mwafaka kuhusiana na tatizo ambalo limewafanya kutoka bungeni.

Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho aliliambia gazeti hili kuwa: “Kimsingi tulikubaliana wote katika kikao kwamba bila wenzetu hatuwezi kupata Katiba Mpya, kwa hiyo tulimwomba mwenyekiti (Sitta) awatafute viongozi wa Ukawa ili afahamu msimamo na mwelekeo wao na ikiwezekana waanze mazungumzo.”

Mjumbe huyo aliongeza: “Tulishauri pia kwamba Mwenyekiti awafahamishe wakubwa walioko serikalini kuona jinsi gani wanaweza kuwatafuta wenzao ili watafute mwafaka, maana hali tuliyofikia ni mbaya.”

Alisema ilishauriwa kwamba zitafutwe njia za kumhusisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Seif Sharif Hamad kama hatua ya kushawishi upande wa Ukawa kulegeza msimamo wao.

Mjumbe mwingine alisema katika kikao hicho yalitolewa mapendekezo kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuruhusu kufanyika kuwa kura ya maoni kwa sura mbili; ya kwanza na ya sita za Rasimu ya Katiba, lakini wazo hilo lilipingwa.

“Hilo wazo lilitolewa sawa, lakini lilionekana kama halitafaa kwa sababu kimsingi hata kura zikipigwa baina ya serikali mbili na tatu, matokeo ya Zanzibar yanafahamika, kwa hiyo tuliona jambo la msingi ni kufanyika kwa mazungumzo,” alifafanua mjumbe huyo.

Alisema kikao hicho hakikuwa na hitimisho kuhusu suala hilo kutokana na wajumbe wa kikoa hicho ambao ni wanachama wa Ukawa akiwamo Mbowe kukisusia.

Mazungumzo Zanzibar

Habari zaidi ambazo zililifikia gazeti hili zinasema kumekuwa na harakati zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutaka mazunguzo na CUF.

Mmoja wa viongozi wa CUF ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge la Katiba, Ismail Jussa alisema awali mazungumzo ya kutaka Zanzibar kuwa na msimamo mmoja yalianzia kabla ya wajumbe kufika bungeni.

“Sisi Chama cha CUF tulitaka kuwapo na msimamo mmoja mara kadhaa kabla ya kuja bungeni lakini Balozi Seif Alli Idd (Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar), hakuliafiki jambo hili,” alisema.

Alisema Jumamosi iliyopita Balozi Idd aliwaita yeye na Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui ili kutaka mazungumzo yafanyike.

“Alituambia kuwa kuna Wawakilishi wa upande wa CCM walimfuata na kumwomba akutane nasi ili tufanye maridhiano kupata sauti moja kutoka Zanzibar,” alisema.

Alisema lengo la mwito huo ni kuwashawishi ili kupata Katiba yenye muundo wa serikali mbili ambao utatatua kero mbalimbali.

Alisema walimshauri Balozi Idd kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ili akutane na Maalim Seif kufanya maridhiano hayo. “Sisi wakishafanya maridhaino yatashuka chini na sisi tutayapokea na kuyafanyia kazi,” alisema.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Balozi Iddi alisema hakuna mazungumzo yoyote ambayo yamekwishaanzishwa baina yao na CUF.

“Hili siyo suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu wao waliondoka katika Bunge wenyewe na uamuzi wa kurejea ni wa kwao wenyewe,” alisema Balozi Iddi.

Msimamo wa CUF

Jussa alisema msimamo wao ni serikali tatu ambazo zilipendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa sababu hawaoni ni vipi mfumo wa serikali mbili utaondoa kero ya Tanganyika kuvaa koti la muungano.

“Kwa hatua hii tuliyofikia amechelewa kufanya maridhiano ambayo tuliyaomba tangu awali kabla ya kuja huku,” alisema Jussa.

Hata hivyo, alisema hawataweza kufikia maridhiano bila kushirikisha wenzao wa Tanzania Bara kwani wataua nguvu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Hatuwezi kufikia maridhiano bila kuwashirikisha wenzetu wa Bara (Ukawa), maana huko kutakuwa ni kuvunja nguvu umoja wetu,” alisema.

Alisema maridhiano ya kutaka Zanzibar kuwa na kauli moja yalianza miaka mitatu iliyopita lakini yalikwamishwa na viongozi wa juu wa CCM wa upande wa Zanzibar.

“Tatizo ni kwamba wenzetu hawana nia njema na maridhianao haya ya kutaka Zanzibar tuwe kitu komoja,” alisema Jussa.  

Imeandikwa na Neville Meena, Daniel Mjema, Ibrahim Bakari, Sharon Sauwa, Edwin Mjwahuzi na Beatrice Moses.