Amani na maendeleo ni chanda na pete
Lilian Timbuka ni mhariri mkongwe wa Jarida la Siasa kwenye gazeti la Mwananchi.
Kuna jambo moja ambalo Watanzania wengi hulitaja kwa fahari wanapozungumzia taifa lao; amani. Kwa zaidi ya miongo sita tangu kupata uhuru, Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizofanikiwa kudumisha utulivu wa kisiasa na mshikamano kwa wananchi wake licha ya tofauti za kidini, kikabila na kisiasa.
Huo ni urithi mkubwa ambao haukupatikana kwa bahati, bali kwa uamuzi wa makusudi wa kujenga taifa linalotanguliza umoja kuliko tofauti.
Lakini kadiri miaka inavyosonga, mjadala mmoja unazidi kupata uzito. Je, amani peke yake inatosha? Au ni wakati sasa wa kuendelea kuibeba sambamba na maendeleo yanayoonekana katika maisha ya wananchi?
Swali hilo lina umuhimu mkubwa kwa sababu hakuna mwananchi anayekula amani peke yake. Amani ndiyo mazingira yanayowezesha uzalishaji, biashara, uwekezaji na utoaji wa huduma za jamii, lakini matokeo yake yanapaswa kuonekana katika maisha ya kila siku ya wananchi. Ndipo amani inapokuwa na maana pana zaidi.
Kwa miaka ya karibuni, Tanzania imewekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati. Reli ya kisasa, uzalishaji wa umeme, ujenzi wa madaraja, barabara, viwanja vya ndege na maboresho ya bandari ni sehemu ya jitihada za kujenga uchumi imara. Hayo ni mafanikio yasiyopaswa kubezwa.
Hata hivyo, swali ambalo wananchi wengi hujiuliza ni moja; maendeleo hayo yanabadilisha kwa kiwango gani maisha yao? Mkulima anahitaji kuona mazao yake yanapata soko lenye uhakika. Mvuvi anahitaji mazingira bora ya kufanya kazi. Mfanyabiashara mdogo anahitaji mtaji na sera zinazomwezesha kukua. Kijana aliyehitimu elimu anahitaji ajira au mazingira yanayomruhusu kujiajiri. Mama wa kawaida anahitaji huduma bora za afya na elimu kwa watoto wake. Hivyo ndivyo maendeleo yanavyopimwa. Ndiyo maana dhana ya maendeleo ya kweli haiwezi kuishia kwenye takwimu za ukuaji wa uchumi au ukubwa wa miradi. Ukuaji wa uchumi unapokuwa hauonekani katika kipato cha wananchi, uwezo wao wa kumudu gharama za maisha na upatikanaji wa huduma bora, bado kunakuwa na kazi kubwa ya kufanya.
Vivyo hivyo, amani nayo haiwezi kuendelea kuwa imara bila wananchi kuona matunda ya utulivu huo. Historia ya dunia inaonyesha kuwa jamii nyingi zimeingia kwenye migogoro si kwa sababu ya tofauti pekee, bali kutokana na hisia za kutengwa, ukosefu wa fursa na changamoto za kiuchumi. Hivyo, maendeleo jumuishi ni sehemu ya ulinzi wa amani. Katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaendelea kujijenga kiuchumi, kuna kila sababu ya kuhakikisha sera zote za maendeleo zinamlenga mwananchi wa kawaida. Serikali inapowekeza katika miundombinu, ni muhimu uwekezaji huo uzalishe ajira, uongeze uzalishaji wa ndani na kuinua kipato cha wananchi.
Hapa ndipo nafasi ya sekta binafsi inakuwa muhimu. Serikali inaweza kujenga mazingira, lakini uchumi unaokua kwa kasi unahitaji uwekezaji wa wazawa na wa kigeni, ubunifu wa vijana, matumizi ya teknolojia na sera zinazorahisisha biashara. Maendeleo endelevu hayawezi kujengwa na Serikali peke yake.
Lakini hata hayo hayawezi kufanikiwa bila kuwapo kwa uwajibikaji. Wananchi wanapolipa kodi wanatarajia kuona fedha zao zikirejea katika huduma bora, miradi yenye tija na matumizi yenye uwazi. Imani kati ya Serikali na wananchi hujengwa pale ambapo kila upande unatimiza wajibu wake.
Kwa upande mwingine, wananchi nao wanapaswa kutambua kuwa maendeleo si jukumu la Serikali pekee. Kulipa kodi, kufanya kazi kwa bidii, kulinda mali za umma, kuheshimu sheria na kushiriki katika shughuli za maendeleo ni wajibu wa kila Mtanzania. Taifa lolote huendelea pale ambapo wananchi wake wanakuwa sehemu ya suluhisho badala ya kuwa watazamaji.
Vyombo vya habari navyo vina nafasi ya kipekee. Mbali na kuripoti mafanikio, vina wajibu wa kuibua changamoto, kufuatilia uwajibikaji na kuhamasisha mjadala unaojenga. Huo ndio mchango wake katika kulinda amani na kuchochea maendeleo.
Tunapoelekea katika hatua mpya za maendeleo ya taifa, ni muhimu tusiangalie amani na maendeleo kama dhana mbili zinazojitegemea. Moja haiwezi kudumu bila nyingine.
Amani hujenga mazingira ya maendeleo na maendeleo huimarisha amani kwa kuwapa wananchi matumaini ya maisha bora. Ndiyo maana mafanikio ya Tanzania hayapaswi kupimwa kwa utulivu wake pekee, wala kwa ukubwa wa miradi inayojengwa.
Yapimwe pia kwa tabasamu la mkulima anayeuza mazao yake kwa faida, kijana anayepata ajira, mfanyabiashara anayekua, mtoto anayesoma katika mazingira bora. Hapo ndipo tutakapokuwa tumefanikiwa kuibeba kwa vitendo dhana ya amani na maendeleo.
Mwandishi ni Mhariri wa Gazeti la Mwananchi