ANTI BETTIE: Ninawaza kujamiiana mara nyingi, nifanyeje nifikirie mambo ya maana?
Swali: Mmh! Hata sijui nianzie wapi, maana muda wote ninawaza kujamiiana kiasi najisikia vibaya.
Kibaya zaidi ninasubiri niambiwe na mtu nakupenda, bora ningekuwa mwanamume ninajichagulia wa kuwa naye.
Nina rafiki, lakini nahisi ameanza kunichoka, kwani siku hizi anachelewa kurudi na vile vimeseji nilivyokuwa namtumia kutwa nzima kuhusu suala hilo, havijibu au anavijibu kwa kuchelewa sana.
Pia zamani alikuwa anajitahidi walau kufikia viwango vya kukidhi haja zangu, lakini siku hizi anachoka mapema.
Nisaidie nifanyeje kupunguza hali hii maana nahisi kabisa ninaelekea kuachwa, pia umasikini utanikuta, kwani siwazi kitu kingine kwa muda mrefu zaidi ya hicho. Nisaidie kwani nami natamani niwe nafikiria zaidi kuhusu biashara na maisha mengine zaidi ya haya yaliyotawala mawazo yangu.
Jibu: Mawazo kuhusu kujamiiana yanaweza kuwa na nguvu kwa watu wengi, na inaweza kuwa ni jambo linaloathiri akili na maisha yao ya kila siku. Ili kumaliza tatizo lazima ujue ni kwa nini mawazo hayo yanazidi kuingia akilini mwako. Kuelewa chanzo cha mawazo haya ni hatua ya kwanza kuelekea kudhibitiwa kwake. Unaweza kujaribu kuandika hisia zako pamoja na mawazo haya ili kupata ufahamu zaidi jinsi yalivyotawala akili yako.
Ukibaini onana na mtaalamu wa saikolojia aliye jirani na wewe ili akupe ushauri wa mara kwa mara na wa karibu, kwani siyo jambo litakaloisha kwa kujadili mara moja. Inawezekana umepata shida kwenye afya yako ya akili (siyo kwa ubaya na ni kawaida kabisa).
Kama ulikuwa unafanya mazoezi ya kawaida na mara moja kwa siku. Ongeza muda wa kufanya mazoezi na iwe mara mbili kwa siku, kwani yanaweza kuhamishia mawazo yako kwenye shughuli nyingine, badala ya kujihusisha na mawazo ya kujamiiana.
Unaweza pia kutafuta shughuli ya kufanya ya kutumia akili kama vile kusuka watu, kushona, kusuka ukili na kufuma vitambaa.
Si vibaya pia kujadili suala hilo na watu unaowaamini zaidi ya mmoja, pengine mjadala huo ukakupa mwanga wa nini cha kufanya. Pia kuichukia hali hiyo kunaweza kuwa tiba ya changamoto uliyonayo.
Kwa kuwa umeshajua hilo ni tatizo, ungana na mawazo ya wengine kulitokomeza, bila kumsahau rafiki yako kumueleza kwa uwazi kuwa unawaza zaidi masuala hayo, ili naye akusaidie kuachana nayo. Si rahisi, lakini ukijitahidi utafanikiwa.
Sielewi maumbile ya mke wangu, nahisi anachepuka
Swali: Anti nahisi kuvurugwa. Ninahisi mke wangu ana mwanamume tofauti na mimi, hilo nimeligundua tunapojamiiana, maumbile yake yanakuwa tofauti. Pia tabia zake zimebadilika sana, amekuwa hana hamu ya kuwa karibu na mimi kama zamani. Naomba unisaidie mbinu za kugundua kama mwenzangu amepata mtu mwingine nje ya ndoa yetu takatifu.
Usiogope Antie, nikijua sitomfanya jambo lolote, nitamuacha tu niendelee na maisha mengine, kwani anavyonifanyia naumia sana. Bora nijue na niachane naye niwe na amani, kwani nikimuuliza anakataa.
Jibu: Sababu ulizoeleza kuwa zinakufanya umfikirie vibaya mkeo sizioni kama zina mashiko sana, labda kwa sababu ninasikia kutoka kwako na sijajionea.
Ila kugundua kama mke wako ana uhusiano nje ya ndoa ni mchakato ambao unahitaji umakini wa hali ya juu.
Hatua ya kwanza ni kuelewa mabadiliko katika tabia yake. Mara nyingi, watu wanapokuwa na uhusiano wa siri, huwa na mabadiliko katika mtazamo wao, mazungumzo na pia matumizi yao hubadilika, namaanisha huwa na kipato cha ziada.
Ikiwa umeona mke wako akionyesha tabia zisizo za kawaida, kama vile kuficha simu yake, kuwa na mwelekeo wa kujificha au kuondoka nyumbani bila sababu za maana, hizi zinaweza kuwa ishara za unachokiwaza, ingawa sio uhakika wa asilimia mia.
Kuwasiliana ni muhimu katika ndoa yoyote. Ikiwa unashuku kuwa mke wako ana uhusiano wa nje, ni vyema kuzungumza naye kwa uwazi.
Hii inahitaji ujasiri na busara kubwa. Kila mmoja wenu anapaswa kuwa na fursa ya kutoa maoni na hisia zake. Usijaribu kumlaumu au kumhukumu, badala yake, jaribu kueleza jinsi unavyohisi. Unasema ukimuuliza anakukatalia, hata kama ni kweli unadhani atakukubalia?
Fanya mazungumzo naye kwa uwazi, ikiwezekana mweleze ulichonieleza mimi kuwa ukijua utaachana naye kwa amani kuliko mateso anayokupa sasa ya kuishi kwa hisia. Uwazi katika mazungumzo yenu inaweza kusaidia kuondoa shaka na kuimarisha uhusiano wenu. Usisahau kumueleza kwa nini unawaza hivyo, inawezekana ukapata jibu la kumaliza mashaka yako kutoka kwake.
Kwa ujumla, kuelewa kama mke wako ana uhusiano wa nje ya ndoa ni mchakato wa kuchambua kwa makini njia zake za maisha, tabia, mawasiliano, na hisia. Kila hatua inahitaji uelewa, uvumilivu, na ushirikiano ili kufikia ukweli.
Ila acha nirudi kwako pia, hujasema kama mliwahi kukwaruzana au ulimuonyesha tabia ambazo hakuzipenda, inawezekana mtu akawa na tabia kama nilizozisema hapo awali lakini ni kwa ajili ya kujihami na kujifariji baada ya kumfanyia vitendo vilivyomtia mashaka pia. Pia suala la hisia usilipe nafasi kubwa kwenye maisha kwani linaweza kuzidisha tatizo.