Athari utitiri bandari kavu zinahitaji mikakati
Bandari Kavu ya makasha matupu iliyopo barabara ya Mandela eneo la Veternary, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam
Utitiri wa bandari kavu (ICD) jijini Dar es Salaam umechochewa na kukua kwa shehena katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na dhamira ya Serikali kuongeza ufanisi wa biashara.
Kwa nadharia, ICD ni suluhisho la kupunguza msongamano bandarini na kuharakisha mzunguko wa mizigo, lakini kwa vitendo, kutokana na wingi wake katikati ya makazi na miundombinu rafiki kwa malori mazito, faida hizo hugeuka kuwa mzigo wa kiuchumi kwa umma.
Ni wazi kuwa barabara kubeba mzigo uliozidi uwezo wake kwa kuwa barabara nyingi za mijini hazikubuniwa kwa mzunguko wa mara kwa mara wa malori ya makontena yenye tani nyingi.
Matokeo yake ni husababisha ufa, mashimo, ajali na kuharibika kwa haraka kwa tabaka la lami. Gharama za matengenezo hutumika fedha za umma ambazo zingeweza kuelekezwa kwenye shughuli nyingine za kimaendeleo.
Hali hii huwa ni mzunguko unaojirudia miundombinu kuharibika mapema, bajeti kupangwa, na wananchi hulazimika kubeba mzigo wa kodi na usumbufu wa barabara zisizo salama.
Hatari kwa usalama wa raia pia imeongezeka. Uwepo wa ICD karibu na makazi ya watu unaweka jamii katika tishio la ajali za malori na hatari ya makontena kuanguka wakati wa upakiaji au usafirishaji.
Ajali hizi hazihesabiki kwa majeraha pekee, hupimwa kwa kupotea kwa nguvu kazi, gharama za matibabu na fidia, pamoja na msongo wa kisaikolojia kwa familia.
Pamoja na hayo, ni ukweli kuwa foleni ndefu zinazochochewa na malori kuingia na kutoka ICD ni hasara ya moja kwa moja ya muda, kwani ni rasilimali isiyorejesheka. Muda unaopotea barabarani ni uzalishaji unaopotea, wafanyakazi huchelewa kazini, mizigo hufika kwa kuchelewa, mafuta huungua bila tija, na gharama za uendeshaji hupanda.
Zaidi, ucheleweshaji huu unaleta hasara kwa biashara ndogo ndogo, huathiri usambazaji wa bidhaa muhimu, na kupunguza ushindani wa biashara kutokana na ucheleweshaji wa malori na bidhaa sokoni.
Kwa wafanyabiashara wadogo, ucheleweshaji huu hupunguza mauzo na mzunguko wa fedha, kwa kampuni kubwa, huongeza gharama za ugavi na kudhoofisha ushindani. Mwishowe, mzigo wa gharama hizi unapelekwa kwa mlaji kupitia bei za juu, hivyo kuathiri watumiaji wa mwisho.
Changamoto hii inahitaji uamuzi thabiti ya kiuchumi na mipango miji yenye nidhamu kwa kutenga maeneo mahsusi ya ICD nje ya makazi ya watu, kuratibu ratiba za malori zisizokinzana na saa za kilele, kuwekeza kwenye miundombinu rafiki kwa mizigo mizito, na kuhamasisha matumizi ya reli.
Hatua hizo zitapunguza gharama za matengenezo ya barabara, zitapunguza ajali na foleni, zitarejesha muda wa uzalishaji, na hatimaye zitaboresha tija ya uchumi wa jiji bila kuua ufanisi wa biashara.
Aidha, kuhimiza matumizi ya reli na vituo vya kimkakati nje ya jiji kama bandari kavu ya Kwala kutapunguza shinikizo kwa barabara za mijini.
Mji unaoendelea si ule unaorundika shughuli bila mpangilio, bali ni ule unaopima kwa umakini gharama zake kwa umma na kuchagua kwa busara suluhisho yanayowanufaisha wote