Benki zifanye haya kuleta unafuu kwa Wateja

Wiki iliyopita tuliangazia ni namna gani benki kupata faida ni vizuri kwenye uchumi, pia kwa wateja wake. Pia tuliona kuwa ni vema sasa benki kupunguza gharama za huduma kwa wateja ili faida kubwa inayopatikana iweze kuleta tija kwa wateja pia.

Hoja ya gharama za kibenki kuwa kubwa ni ya muda mrefu na kilio cha watumiaji wengi wa huduma za kibenki.

Ikumbukwe kuwa tozo za huduma za kibenki sio za kificho kwa wateja wake. Ni takwa la kisheria kuweka wazi gharama ambazo benki inatoza kwa wateja wake. Kuhakikisha kuwa benki zinatimiza takwa hili, benki huwa zinachapisha kwenye magazeti yanayosomwa na watu wengi na pia katika tovuti za benki husika gharama zao za tozo.

Tozo za benki zinatokana na huduma zinazotozwa kwa mteja kuwa na akaunti ya kibenki (akaunti ya akiba ama ya biashara, ama akaunti ya fedha za kigeni). Pia zinatokana na matumizi ya mashine za kutoa ama kuweka fedha (ATMs), matumizi ya huduma za kibenki kupitia simu ama programu za kibenki za simu, intaneti, ama kupitia huduma za wakala.

Kwa utafiti uliofanywa mwaka 2015, ni kuwa kulikuwa na ukuaji wa tozo zinazotokana na matumizi mbalimbali na kuwa faida inayotokana na tozo hizi inachangia kwa kiasi katika upimaji wa faida ya benki kupitia kiwango cha faida kwenye amana za kibenki na kiwango cha faida kwenye mtaji uliowekwa na wanahisa wa benki.

Gharama za kibenki pia zinaongezeka kwa idadi ya tozo na pia ongezeko la tozo kwa kila mwaka. Tafiti nyingi sehemu mbalimbali duniani zinaonyesha pia kuwa tozo za huduma kwa wateja zinachangia kwa kiasi kikubwa faida za benki.

Gharama za kibenki ni nyingi na ghali pia. Kwa mfano kwenye benki nyingi kwenye akaunti za akiba ambazo hutumiwa na watu wengi, ukifungua akaunti kuna gharama utatozwa ukipewa kadi.

Benki pia zinatoza kiwango fulani kila mwezi kwa ajili ya kuhudumia akaunti yako. Manthalani kama una akaunti ya akiba na ukaitumia mara moja tu kwa kila miezi mitatu benki itakuchaji kiasi fulani kwa kuwa na hiyo akaunti ambayo ina akiba yako.

Ukiwa unahitaji kujua salio la fedha ni gharama. Ukiangalia kupitia simu ama mashine za kuweka na kutoa fedha (ATMs) ni gharama pia.

Ikiwa umeenda kwa mhudumu wa tawi la benki kuulizia salio la akiba yako utachajiwa zaidi. Mara nyingine wenye programu za simu za kibenki pamoja na kuwa wanatumia gharama za internet wanachajiwa zaidi wanapoangalia salio la akaunti zao. Ikiwa umepoteza kadi yako au imeisha muda wake wa matumizi utachajiwa pia.

Kwenye akaunti hiyohiyo ya akiba, ukiwa unatoa kiwango chako ulichokiweka kupitia mashine za fedha kuna gharama za kulipia. Ukihamisha kwenda kwenye simu yako ni gharama. Mfano Ukihamisha Sh100,000 kupitia programu ya simu ya benki unaweza kuchajiwa zaidi ya Sh7,500. Ukitoa fedha kupitia ATM unaweza kutozwa hadi Sh1,800 na zaidi kama unatoa kwenye ATM ya benki nyingine.

Utalipia zaidi kama utatoa fedha kwenye kaunta ya kwenye tawi la benki. Ukiangalia gharama hizi ni kubwa na ndizo akaunti zinazotumiwa na watu wengi na bila uelewa mkubwa wa gharama, ingawaje zinawekwa wazi, ama kutambuliwa. Na hata hivyo, si rahisi kukwepa hizi gharama. Hii inafanya matumizi ya huduma za kibenki kuwa chini.

Mfano mtu anayelipwa mshahara wa laki 2 kwenye akaunti yake ya benki, anaweza kujikuta ametumia Sh15,000 kwenye makato ya benki kama hatakuwa na uelewa mzuri wa namna anavyoweza kupunguza makato hayo. Kwa mwaka anaweza kujikuta amelipia karibia Sh200,000, kiwango ambacho ni sawa mshahara wake wa mwezi kwa huduma za kibenki.

Nchi nyingine kumekuwa na mabaraza ya kulinda haki za watumiaji wa huduma za kifedha ambayo kwa kiasi kikubwa husaidia kusikiliza na kuchambua hoja za wateja na kuwasilisha kwa watoa huduma na taasisi za uthibiti, lengo likiwa kupata huduma nzuri na kwa gharama nafuu.

Kwa Tanzania, baraza la watumiaji wa huduma za kifedha ni muhimu sana. Pia elimu ya kifedha kwa watumiaji wa huduma za kibenki ni muhimu zaidi ili kuweza kuelewa ni namna gani wanaweza kuchagua huduma ambazo hazina makato mengi na hivyo kutumia akiba kidogo inayopatikana kutumia kwenye mahitaji mengine.

Ukiangalia takwimu, zaidi ya theluthi moja ya faida ya benki inatokana na tozo za huduma hizi, ni vema kwa benki kuangalia namna ya kupunguza gharama za huduma ambazo zinaathiri mteja mdogo. Hili jambo haliwezi kufanyika kwa muda mfupi, bali kwa mipango ya muda mrefu.

Benki zinaweza kuondoa kabisa gharama za kutunza akaunti ya akiba. Kuweka kiasi cha miamala ambayo inaweza kufanyika bure, kwa mfano kufanya miamala walau miwili kwa mwezi na kuangalia salio walau mara mbili kwa mwezi kuwa bure.

Benki zinaweza pia kupunguza gharama za kutuma fedha kwenye mitandao ya simu kwa sababu imekuwa ni njia nzuri zaidi ya kufanya malipo, na kusafirisha fedha hasa vijijini.

Ni matumaini ya wengi kuwa mikakati ya kupunguza gharama kwa wateja itasaidia kuleta shindani wa kutosha kwenye soko, na itafanya baadhi ya benki hasa makubwa kuweza kupata wateja wengi zaidi na amana za kutosha.