Faida kubwa ya mabenki ipunguze gharama kubwa za huduma zao

Jambo kubwa wiki hii ni ripoti ya ufanisi wa mabenki kwa mwaka 2023, kama ambavyo zilitolewa na mabenki mbalimbali. Ripoti karibu nyingi zinaonyesha ongezeko la faida kwa mabenki, hasa benki kubwa ambazo ni NMB, CRDB Bank na NBC.

Hizi benki ni kubwa kwa namna nyingi kama vile idadi ya wateja, matawi, amana za wateja, mikopo pamoja na jumla ya mali za wateja. Benki kupata faida ni jambo linalotarajiwa na ni jambo zuri kwa uchumi, na kwa wawekezaji.

Kwa jumla benki 20 kwa ukubwa sokoni kwa mwaka 2023 zimetengeneza faida ya zaidi ya Sh1.5 trilioni. Haitarajiwi kabisa taasisi kama benki ipate hasara kwa sababu benki ni taasisi ya kifedha ambayo ina wataalamu wa kutosha na kudhibitiwa mwenendo wa uendeshaji wake na Benki Kuu.

Benki inakopesha wafanyabiashara ambao lengo lao ni kupata faida, walipe mikopo na riba. Hivyo basi ni jambo linalotegemewa kuwa benki iendeshwe kifaida pia.

Benki kupata hasara kubwa au mfululizo kila mwaka inaashiria kuwa benki inaweza kutohimili kiwango cha chini cha mtaji kinachotakiwa na hivyo kuwa na hatari ya kutoruhusiwa kuendelea kufanya biashara ya kibenki.

Ikitokea hivyo ni pigo kwenye uchumi, na hivyo wamiliki wa benki wanahakikisha wanatumia njia mbalimbali kuweza kutengeneza faida hata kama ni kidogo.

Hata hivyo, kwa hali ya kawaida benki pia hazitarajiwi kupata faida kubwa sana kwa sababu ni watoa huduma ambao wanaathiri watumiaji wengi. Bidhaa za kifedha zinatumiwa na umma na hivyo zinapaswa kuwa ni rahisi kutumiwa na watu wengi.

Pia huduma za kibenki zina umuhimu mkubwa sana kwenye ukuaji wa uchumi na uchumi wa mtu mmojammoja. Ni kwa sababu kuna gharama za kupata huduma za kibenki ambazo mtu mmojammoja analipia, pia riba za mabenki zimelalamikiwa kuwa kubwa.

Upatikanaji wa faida usiowiana katika soko la mabenki unaashiria pia kuwa hakuna ushindani wa kutosha katika sekta ya kifedha. Pia inaashiria kuwa wateja wa benki hawana namna ambavyo wanaweza kuchagua huduma nafuu kwenye mabenki mengine bila kulipa gharama ya ziada.

Mchanganuo wa amana za mabenki mengi unaonyesha kuwa kuna ongezeko chanya. Ongezeko hili ni zuri kwa sababu inaonyesha kuwa kumekuwa na mwako wa wananchi na biashara mbalimbali kutumia huduma za kifedha kuweka amana.

Pia kuna ongezeko la mali za benki, ikiwemo mikopo inayotolewa na mabenki. Mikopo inasaidia upatikanaji wa ajira na pia kuongeza uzalishaji kwenye uchumi, jambo ambalo ni zuri.

Mojawapo ya viashiria vya uchumi ni pamoja na ongezeko la mikopo kwenda sekta binafsi. Ni vizuri mikopo kuongezeka, lakini ni vizuri zaidi kujua ni mikopo ya aina gani imeongezeka, ni ya muda mfupi au muda mrefu.

Ni jambo jema kuwa mabenki yameweza kupunguza mikopo chechefu ambapo mabenki makubwa wameonyesha kuwa urudishwaji wa mikopo sio tatizo kubwa lisilohimilika.

Mapato ya mabenki hutokana na shughuli mbalimbali ambazo kubwa zaidi ni mapato ya riba na mapato yasiyo na riba. Mapato ya riba ni mapato yanayotokana na shughuli za utoaji wa mikopo.

Mapato ambayo siyo ya riba ni yale yanayotokana na malipo ya gharama mbalimbali ambazo wateja wanalipia. Inawezekana ikawa ni shughuli za huduma kama za bima, huduma za ATMs, shughuli za kutuma fedha na kuhamisha fedha kutoka benki kwenda kwenye mitandao ya kifedha na kadhalika.

Ni vizuri pia kujua kuwa mabenki ili kupata faida yanapunguza pia gharama za uendeshaji kwa kutumia mbinu mbalimbali.

Hivyo basi, faida ya mabenki ni matokeo ya mambo mbali mbali ambayo benki inayafanya ili kuweze kufikia malengo yaliyowekwa. Hata hivyo tunategemea kuwa kiwango kikubwa cha faida kinatokana na ukuaji wa mapato, na sio upunguzaji wa gharama za uendeshaji. Mabenki pia yanaonyesha kutumia vyema huduma za kidijitali kwa sababu ongezeko la matawi wala idadi ya wafanyakazi.

Mchanganuo wa haraka wa mapato yasiyo na riba, zimechangia kwa kiasi kikubwa zaidi ya asilimia thelathini ya mapato yote ya kibenki, kwa benki zilizo nyingi. Hii inaweza kumaanisha kuwa kuna gharama nyingi ambazo zingeweza kupunguzwa, hasa na mabenki makubwa katika utoaji wa huduma, zikawanufaisha watu wengi na hapo hapo bado benki ikawa ina tija.

Kwa mfano gharama za miamala ya kibenki zimekuwa ni kubwa, pia gharama za mikopo ya kibenki, hasa mikopo binafsi na ile ya kibiashara. Kwa mfano gharama za kuhamisha fedha benki kwa watu wenye miamala midogo midogo ni kubwa sana. Gharama za kutoa fedha benki au kwenye ATM nazo ni kubwa.

Ukuaji wa faida za kibenki pengine unatoa mwanya wa kuangalia namna wateja wa mabenki wanavyoweza kunufaika na ukuaji wa faida za kibenki. Kiashiria kizuri kitakuwa ni kupungua kwa riba ya mikopo na pia kupunguza gharama za kufanya miamala mbalimbali ya kibenki, pamoja na malipo ya huduma nyinginezo.

Kiashiria kingine ni kuongezeka kwa uwekezaji wa mabenki ili kufikisha huduma sehemu nyingi zaidi, hasa vijijini. Inatarajiwa pia kuwa benki ambazo zinapata hasara wakati nyingine zikiwa na ukuaji mkubwa, kuangalia namna nzuri ya kuboresha huduma zao ili ziweze kukidhi mahitaji wa wateja, kwani wateja pia wasingependa kuona benki yao inapata hasara.