CCM imekalia kuti kavu kwa wenyeviti hawa
Naweza kuilinganisha hali ya wenyeviti wa Serikali za mitaa na vijiji hapa nchini ‘waliogoma’ kuitisha mikutano ya wananchi bila sababu za maana, sawa na donda ndugu lisilotii na kusikia aina yoyote ya dawa!
Katiba inafafanua kuwa Serikali za Mitaa ni vyombo vya wananchi vilivyopo katika ngazi ya msingi ya Serikali. Huundwa, kuendeshwa, kusimamiwa na kuwajibika kwa wananchi wenyewe.
Hivyo basi Serikali za Mitaa zimeundwa kwa mantiki ya kuwawezesha wananchi, wanaume kwa wanawake, kushiriki katika masuala ya siasa, uchumi, upatikanaji wa huduma na utawala katika maeneo yao.
Kwa ujumla ni muundo ambao unawawezesha wananchi kuwa na udhibiti wa maamuzi ya wawakilishi waliowachagua.
Kwa mtazamo huu wa kikatiba, Serikali za Mitaa ni fursa kubwa kwa wanajamii kukuza demokrasia na ushiriki wao katika maendeleo ya maeneo yao.
Ni vyema ieleweke kuwa Serikali za Mitaa si wakala wa Serikali Kuu, bali ni serikali kamili zenye mamlaka kisheria.
Kwa mujibu wa Katiba, wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali inapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi.
Kwa tafsiri hiyo hapo juu, ilikuwa haitegemewi kuweko na serikali yoyote iwe ya mtaa au kijiji chini ya mwenyekiti wake aliyechaguliwa na wananchi wenyewe, akae miaka miwili au mitatu pasina kuitisha mkutano hata mmoja.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa au kijiji, hana hiyari ya kuitisha mkutano mkuu wa eneo lake la utawala lah, bali analazimika kufanya hivyo kila baada ya miezi mitatu.
Hakuna siyejua kwamba, kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wa serikali za mitaa na vijiji, kazi za mkutano mkuu wa kijiji/mtaa ni pamoja na kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijiji kama itakavyotolewa na serikali ya kijiji.
Jukumu jingine la mkutano mkuu huo wa kijiji ni kupokea na kujadili taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za kijiji ya tangu mkutano uliopita, na hapa kiukweli kwa uzoefu nilionao wa kuhudhuria mikutano mingi ya vijiji, ndipo unapoishia mkutano wenyewe.
Kwa kuwa wananchi wa kijiji/mtaa wanajua vyanzo vingi vya mapato kwenye maeneo yao, na baadhi ya wajumbe wa kamati za fedha hawataki kujiingiza wala kuingizwa kwenye ‘dhambi’ ya ulaji fedha, taarifa za ubadhirifu huvuja mapema na kufanya wananchi wasubiri kwa shauku ajenda hiyo muhimu ya mapato na matumizi, pengine kwa lengo la kutaka ‘kumsulubu’ mwenyekiti.
Kwa uchunguzi wangu mdogo nilioufanya wakati naandaa uchambuzi huu, zipo baadhi ya halmashauri nchini zenye majimbo mawili ya uchaguzi na kila jimbo lina vijiji vinavyokadiriwa kufikia 40-50, na nusu kati ya idadi hiyo, inaelezwa kuwa wenyeviti wake wa vijiji hawajui msamiati wa ‘kuitisha mikutano.
Sielewi hao wenyeviti wa serikali za vijiji hivyo wanakwenda kujadili nini kwenye Baraza la Maendeleo la Kata (BMK) ikiwa hakuna mikutano yoyote inayoitishwa kwenye vijiji hivyo.
Lakini kubwa zaidi ambalo hata baadhi ya wananchi kwenye vijiji hivyo wanahoji, ni uhalali wa viongozi hao kuendelea kusalia mamlakani.
Nadhani hapa ndipo mahala panapohitaji Waziri wa Tamisemi Mohamed Mchengerwa, kuingilia kati na hatimaye kupatikane ufumbuzi, vinginevyo kama mazingira ya uchaguzi mwakani yakiepukana na figisufigisu za wagombea kupita bila kupingwa, CCM ijiandae kupoteza vijiji na mitaa mingi yenye viongozi wa kalba hii.
CCM inaweza kupoteza pia viti vingi vya Serikali za Mitaa na viongozi wake wasiamini kitakachotokea, licha kwamba Serikali Kuu chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wake Dk Philip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, imekuwa ikiwajibika vema kwa wananchi wake.
Ukiachilia mbali Waziri wa Tamisemi, sijui viongozi wa CCM kuanzia ngazi za matawi, kata na hata kamati za siasa za wilaya, zinafanya nini kuwashurutisha wenyeviti hao wa serikali kwa mujibu wa miongozo yao kuitisha mikutano katika maeneo yao.
Hivi viongozi wa CCM ambacho sehemu kubwa ya wenyeviti wa serikali za vijiji na mitaa hapa nchini iliwadhamini na ‘wakapita’ bila kupingwa, hawajui mchezo wao ndiyo mauti yao?
Basi kama CCM na viongozi wake wamelala na mpaka sasa hawajui kwamba, mchezo huu wa kutoitisha mikutano ya vijiji na mitaa wanaoucheza wenyeviti utasababisha mauti yao, wandelee ‘kupandisha mabega na kurelax’ kwa lugha ya Mchengerwa!, ila wasinione mchawi!
Rashid Mtagaluka ni mwandishi wa habari na anapatikana kwa simu 0784 43 85 46. [email protected]