Kinana azitaka taasisi za kijamii zikomalie elimu ya ujasiriamali

Muktasari:

  • Kinana amesema endapo taasisi za kijamii zitajikita kuhamasisha elimu ya amali (ufundi), vijana wengi watapata utaalamu katika fani mbalimbali ambao utawawezesha kujiajiri, kuajiri wenzao na hata kuwa na sifa ya kuajiriwa katika maeneo mbalimbali ya fani walizozisomea na kujifunza.

Arusha. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) - Bara, Abdulrahman Kinana amezihimiza taasisi za kijamii kuweka mkazo katika elimu ya ufundi na ujasiriamali, ili kupata mwarobaini wa tatizo la ajira na kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali.

Kinana ameyasema hayo leo Jumapili Desemba 24, 2023 jijini Arusha, alipokuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa 10 wa Jukwaa la Vijana wa Kiislamu Mkoa wa Arusha (Juvikiba).

Amesema endapo taasisi za kijamii zitajikita kuhamasisha elimu ya amali (ufundi), vijana wengi watapata utaalamu katika fani mbalimbali ambao utawawezesha kujiajiri, kuajiri wenzao na hata kuwa na sifa ya kuajiriwa katika maeneo mbalimbali ya fani walizozisomea na kujifunza.

Mwenyekiti wa Juvikiba, Kassim Degega amesema lengo la jukwaa hilo ni kuwasaidia vijana kujikwamua na umasikini lakini pia kuisaidia jamii.

Degega amesema wanakusudia kujenga kituo cha Waislamu katika eneo la Nduruma Mkoa wa Arusha ambapo kutakuwa na shule za ufundi, kituo cha afya na sekondari.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Islamic Foundation, Arif Nahd amesema ni muhimu Waislamu kujitokeza kuchangia maendeleo ya Waislam na Uislam.

Mkuu wa kitengo cha Huduma za Kiislamu katika Benki ya KCB ambao ndio wadhamini wa tukio hilo, Amour Muro amesema benki hiyo ina huduma ya Sahl  ambayo inafuata sheria za Kiislamu na amewataka vijana wa Kiislamu na wasio Waislam kujiunga.