Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Changamoto ya Barabara ya Kilwa ifanyiwe kazi

Barabara ya Kilwa, hasa kipande kinachotoka Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe, imegeuka kuwa chanzo kikuu cha mateso kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

Ingawa tayari miezi mitano imepita tangu kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa njia nne ya barabara hiyo, hakuna dalili zozote zinazoashiria mwanzo wa ujenzi huo, licha ya ahadi kuwa mradi ungeanza baada ya mchakato wa maandalizi kukamilika.

Hili ni jambo la kusikitisha na linaacha maswali mengi kuhusu dhamira ya kweli ya kutatua tatizo hili linalogharimu maisha, muda na uchumi wa Taifa.

Kwa muda mrefu sasa, barabara hii imekuwa mzigo kwa watumiaji wake, kutokana na msongamano mkubwa wa magari, ajali za mara kwa mara na upotevu wa muda unaokadiriwa kufikia saa tatu hadi nne kwa safari ambayo haitakiwi kuzidi dakika 30.

 Hili si tatizo jipya, ni tatizo linalojulikana vizuri na mamlaka husika, na zaidi ya yote, ni tatizo linaloongezeka kila siku.

Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kupitia kwa Meneja wake wa Mkoa wa Dar es Salaam, imethibitisha kuwa, ujenzi utaanza ndani ya mwezi huu.

Hata hivyo, kauli hii imekuja baada ya kusuasua kwa muda mrefu na inaacha wasiwasi mkubwa kwa wananchi waliopoteza imani kutokana na kutotekelezwa kwa ahadi za awali.

Kwa hali ya sasa, haitoshi kutoa ahadi tu, bali wananchi wanahitaji kuona vitendo. Mradi huu uwe ni wa kipaumbele cha kitaifa, kwa sababu Barabara ya Kilwa si ya wakazi wa Mbagala na Kongowe pekee, bali ni lango kuu la kiuchumi linalounganisha Dar es Salaam na mikoa ya Lindi, Mtwara na hata nchi jirani kupitia Bandari ya Mtwara.

Ucheleweshwaji wa miradi ya barabara una athari kubwa kwa pato la Taifa. Msongamano wa magari unamaanisha muda wa kazi unapotea, gharama za usafirishaji zinaongezeka, bidhaa hufika sokoni zikiwa zimechelewa au kupoteza ubora na ajali husababisha ulemavu au vifo vinavyoweza kuepukika.

Haya yote yakiunganishwa yanaonesha kuwa kuchelewesha ujenzi huu ni sawa na kuruhusu Taifa kuvuja mapato bila sababu ya msingi.

Barabara hii ni miongoni mwa zinazobeba malori ya mizigo kutoka viwanda vya Wilaya ya Mkuranga na maeneo ya Pwani, ni dhahiri kuwa ukarabati au upanuzi wake haupaswi kucheleweshwa tena.

Serikali imeshathibitisha kuwa viwanda ni injini ya uchumi wa viwanda, lakini bila miundombinu madhubuti ya usafirishaji, dhamira hiyo haiwezi kufikiwa.

Kwa mantiki hiyo, uboreshaji wa barabara ya Kilwa ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya uchumi wa viwanda.

Ni muhimu kwa mamlaka kama Tanroads na Wizara ya Ujenzi kutekeleza mikataba kwa wakati na kuhakikisha kuwa makandarasi wanawajibishwa. Visingizio vya maandalizi ya malipo ya awali haviwezi kuwa sababu ya kuchelewesha mradi kwa miezi mitano, hasa wakati hali ya barabara hiyo ni mbaya kiasi cha kuhatarisha maisha ya watu kila siku.

Hali ilivyo sasa inatoa taswira ya dharura. Wananchi wameshachoka na mateso ya kila siku.

Kila ajali inayotokea, kila biashara inayopotea, kila mtoto anayepata adhabu kwa kuchelewa shuleni ni ushahidi wa ukosefu wa usimamizi makini.