Edward Ngoyai Lowassa: Mapito yako ni mafunzo kwetu

Edward Lowassa, kesho tunakuhifadhi katika nyumba yako ya milele, nyumbani kwako katika kijiji cha Ngarash Wilaya ya Monduli mkoani Arusha. Unaagwa na wote, waliokupenda na ambao hawakukupenda, kwani kwao wote ulikuwa na maana kubwa kwenye maisha yao.

Waliokupenda walipata mlezi, baba, kiongozi na ‘mentor’. Wasiokupenda walipata kitu cha kupinga na sababu ya harakati zao. Hayo ndiyo maisha ya wanadamu, lazima uwe na wanaokupenda na wasiokupenda hata kama hawana sababu ya kutokukupenda. Kuna waliokupenda, basi tu wanakupenda kama mwanadamu na kuna ambao hawakukupenda kwa sababu ambazo kwao zina maana kubwa.

Kila mwanadamu ana makundi yote haya. Wewe mwenzetu ilikuwa ni ziada kidogo maana waliokupenda walikupenda kweli-kweli na waliokuchukia walikuchukia kweli-kweli.

Hili ni funzo kubwa kwa tunaobaki duniani. Hata hivyo, haijalishi. Wote kabisa wamesikitishwa na kifo chako, kwani hakuna anayebisha kuwa umeacha urithi (legacy) katika maendeleo ya siasa, uchumi na jamii ya Watanzania.

Urithi wako ni mazungumzo yamegubika msiba wako. Kila mtu akijitahidi kueleza mema yako, ndiyo mema tu. Ndiyo utamaduni wetu huo na unajua. Mema yako ni mengi kwa Taifa letu na wengi wameyaeleza kwa namna tofauti-tofauti. Mimi nitakukumbusha machache tu, maana mengine wewe mwenyewe umeyasahau. Ni wajibu wetu kukumbusha, Edward.

Katika kipindi cha miaka 10 ambayo tulikuwa wote katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nilikufahamu kwa kiasi changu nilichostahiki. Mengine nilikufahamu kwa kuhadithiwa tu na watu uliokuwa nao karibu zaidi. Katika miaka hiyo 10 ambayo mimi na wewe tulikuwa wote bungeni, miaka miwili hivi ulikuwa Waziri Mkuu. Ulikuwa Waziri Mkuu kweli-kweli.

Nakumbuka sisi wabunge wa upinzani tukikaa upande kinzani nawe, tukitazamana. Ulikuwa ukikaa bungeni, ukigeuka kutazama nyuma yako mawaziri wanatetemeka hasa. Hapakuwa na utoro usio na sababu wa mawaziri bungeni. Hakukuwa na kujibu maswali ya wabunge kwa matani-matani. Ulikuwa ‘disciplinarian’ kiasi mawaziri walikuwa wakilaumu kwenye ‘corridors’ za Bunge ulikuwa kama mnyapara.

Edward, ulikuwa mkali sana. Kwa nafasi yako ilipaswa kuwa hivyo. Nikiwa naandika tanzia hii, navuta kumbukumbu za namna tulikuwa na miaka miwili mizuri ya siasa za Bunge. Nidhamu ni urithi wako mkubwa kwa sisi wanasiasa tuliobakia.

Jambo moja watu wengi hawalijui sana ni kuwa ulikuwa mwanademokrasia. Uliheshimu nafasi ya vyama vya upinzani katika siasa za Bunge. Tukio moja ambalo hupenda kulihadithia mara kwa mara ni lile la namna uliomba ruhusa ya viongozi wa upinzani, ili Serikali itumie fedha za akiba ya dharura kutekeleza uamuzi wa Umoja wa Afrika kuweka mambo sawa kule Shirikisho la Comoro.

Zitto afichua uhusiano wa ACT Wazalendo, Lowassa

Jumapili moja, sijui kama unakumbuka, ulituita (Kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed, Naibu Kiongozi wa upinzani bungeni, Dk Willibrod Slaa na mimi nikiwa Katibu wa Wabunge wa upinzani wakati huo).

Ulituita ofisini kwako, Magogoni, Dar es Salaam kutueleza kuwa Umoja wa Afrika umetoa agizo Tanzania kuongoza hatua za kijeshi kumwondoa Kanali Mohammed Bakari, aliyekuwa amejitangazia Jamhuri yake ya Kisiwa cha Anjoan. Lakini AU haikuwa imetoa fedha mpaka muda ule. Majeshi yalikuwa tayari na Rais wetu alikuwa Mwenyekiti wa AU. Ulituambia Serikali ya Ufaransa ilikuwa inajaribu kuleta chokochoko kutumia ombwe lile la majeshi ya Afrika kuchelewa.

Ukaomba ruhusa yetu kuwa Tanzania itumie fedha za dharura kwenye bajeti kutekeleza ‘mission’ ile na AU wakiwa tayari watarejesha fedha zile. Serikali ingeweza kutumia fedha kinyume cha sheria bila kuomba kibali chetu na ulijua kuwa tusingefanya lolote.

Lakini ulitambua kuwa shughuli ile ilikuwa ni ya hadhi ya Taifa, lakini vilevile tungekuwa na haki ya kuhoji bungeni kukiukwa kwa taratibu za bajeti.

Ulifanikiwa mambo mawili makubwa, moja ulihakikisha hatuhoji, kwani sura imeumbwa na aibu kwa kutushirikisha kule. Pili ulijenga imani kwamba unatuheshimu – mwanadamu gani asiyependa kuheshimiwa? Ulijishusha, ili kufanikisha jambo nyeti na ulifanikiwa.

Hili ni somo kubwa kwa viongozi wenye mamlaka na madaraka kwamba, hautakuwa na madaraka nusu iwapo ukishirikisha wengine, tena wa upinzani katika suala nyeti la Taifa.

Nilipenda uwezo wako wa kuamua na kusimamia maamuzi yako. Nakumbuka siku moja ulizungumza bungeni kuhusu kufanya maamuzi, ukisikitika kuwa tumekuwa na nchi ambayo kila mtu analalamika. Leo hii Tanzania ina chuo kikuu kikubwa kwa sababu ya uwezo wako wa kusimamia uamuzi.

Nakumbuka tulivyowananga bungeni pale Rais wako alipotamka kujenga chuo kikuu kipya cha Dodoma. Tulihoji kwa nini mjenge chuo kipya, ilhali vyuo vilivyopo vina hali mbaya. Ulitujibu kuwa ‘tutajenga chuo kikuu kipya cha Dodoma na ndani ya miezi tisa watoto watadahiliwa’.

Tulikubishia. Ulitu ‘prove wrong’. Siku moja aliwaita wakuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii, alinihadithia namna alivyosimama kidete kuhakikisha kuwa Udom inaanza. Warasimu wa Serikali walipojaribu kukuchelewesha kwa kutumia michakato ya manunuzi, uliwaambia walete barua zao za kujiuzulu, ili Rais ateue watu wengine watakaoweza kufanya nao kazi kufanikisha azma yake ya kujenga chuo kikuu kikubwa.

Kila mfuko wa hifadhi ya jamii ulikabidhiwa eneo la ujenzi na leo hii tuna wanafunzi zaidi ya 20,000 wanapata maarifa na vilevile mji wa Dodoma ulibadilika kabisa kimaendeleo.

Umetangulia mbele ya haki, lakini urithi wako unaishi kwa muda mrefu. Nakukumbusha, lakini kuwa Serikali haijalipa madeni iliyochukua kujenga Udom.

Ni wazo jema Serikali kufikiria kuuita ukumbi mkubwa wa mihadhara pale Udom kwa jina lako. Ukumbi wa Chimwaga uitwe Edward Lowassa Chimwaga Hall kama kumbukumbu ya jitihada zako za kusimamia maelekezo ya Rais wako na Serikali yako.

Uamuzi wako wa kutoka CCM mwaka 2015 na kugombea urais kupitia Umoja wa Vyama vya Upinzani – Ukawa ndiyo mjadala mkubwa tangu umepoteza maisha.

Wenzako wa CCM wanakukumbatia – ni haki yao maana hatimaye ulirejea nyumbani. Lakini pia wale uliokaa nao miaka michache wanakulilia.

Ni ukweli usiopingika kuwa ulipotoka CCM ulipata faraja na tuliona tabasamu lako na sura ikinawiri. Ulikuwa ni uamuzi muhimu katika kukomaza demokrasia. Ulifanya jambo kubwa la maana katika saikolojia ya Watanzania kwamba, inawezekana kabisa chama kingine kushika usukani wa nchi yetu.

Uliweka rekodi ya kuwa mgombea wa upinzani ambaye ulipata kura nyingi zaidi katika kinyanganyiro cha urais wa Tanzania kuliko mgombea mwingine yeyote aliyepata kutokea mpaka sasa. Uliwezesha majiji yote Tanzania kuongozwa na vyama vya upinzani.

Kwamba uliweza kutoka katika hali ambayo watu walikukimbia, wakiogopa kuhusishwa na wewe mpaka mahali kila mtu alikukimbilia na kupata asilimia 40 ya kura zilizotangazwa ni mafunzo ambayo tusipojifunza tutakuwa mahayawani. Ulikuwa mwamba Edo na ulionyesha umwamba wako.

Namna gani vyama vya upinzani vilitumia kazi hiyo kubwa uliyofanya kujiimarisha zaidi ni jambo ambalo ni mjadala wa siku nyingine.

Tulipokutana Zanzibar kwenye mkutano uliozaa Azimio la Zanzibar la mwaka 2018 kudai demokrasia, ulitueleza masikitiko yako kuwa vyama vya upinzani hatujiandai kushika dola. Ulituasa kuimarisha vyama vyetu na kushirikiana kwa dhati kupitia mazungumzo.

Ulisisitiza mazungumzo kama jambo muhimu katika demokrasia. Miezi michache baadaye uliamua kurejea CCM.

Huna baya Edward, ulifanya wajibu wako. Mapito yako haya ni mafunzo makubwa kwetu. Tangulia Edo. Tangulia EL. Nenda huko na tabasamu lote.

Kwani umevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo umeumaliza, imani yako umeilinda.