Lowassa alivyotinga kimafia Chadema bila walinzi

Edward Lowassa akiwa katika Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema alipojiunga na chama hicho Julai 2015

Muktasari:

  • Mnamo Julai 25, 2015, Edward Lowassa, waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, alishtua ulimwengu wa siasa kwa kuondoka CCM na kujiunga na Chadema. Hilo lilitokea baada ya kutofaulu katika mchujo wa CCM na hivyo akaibukia katika kikao cha Kamati Kuu cha Chadema.

Dar es Salaam. Miongoni mwa mambo yaliyoushangaza ulimwengu wa siasa na kuacha kumbukumbu isiyofutika, ni kitendo cha Edward Lowassa kuondoka kwenye chama alichokulia na kujiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Ni jambo ambalo halikutarajiwa na lilifanyika kwa siri hadi pale alipotua kwenye Kamati Kuu ya chama hicho usiku bila walinzi wake.

Mwandishi wa habari wa Mwananchi, Edwin Mjwahuzi ambaye ndiye pekee aliyekuwa kwenye eneo la Hoteli ya Ledger Bahari Beach wakati huo, amesema baada ya kutaarifiwa na msiri wake alifika hapo kwa pikipiki usiku na kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

“Bahati nzuri kila upande ulidhani nimeitwa na upande wa pili; yaani Chadema walidhani nimeambiwa na Lowassa na watu wa Lowassa walidhani nimeitwa na Chadema, hivyo sikubughudhiwa.

“Kilichonistaajabisha sikuwa nimewahi kumwona waziri mkuu mstaafu anatembea bila walinzi wake. Siku hiyo walikuwa wawili, yeye na dereva wake binafsi,” amesema.

Hiyo ilikuwa baada ya Kamati Kuu ya CCM kutangaza majina matano ya waliopitishwa kwenye  mchujo katika halmashauri kuu bila ya jina la Lowassa kuwemo, ndipo likaibuka swali; atatoka au hatoki?

Katikati ya mtanziko huo, ndipo jibu likapatikana, akatoka na kujiunga Chadema, iliyokuwa ndani ya Ukawa.

Ilivyokuwa

Usiku wa tukio Julai 25, 2015, Lowassa alihudhuria rasmi kikao cha Kamati Kuu ya Chadema ili kutambulishwa na kujadiliana mikakati ya kuing’oa CCM madarakani.


Edward Lowassa alipotinga kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kutambulishwa Julai 25, 2015


Kikao cha Kamati Kuu kilianza saa 9.30 alasiri katika Hoteli ya Ledger Bahari Beach, Dar es Salaam ambacho wajumbe wa Kamati Kuu walikuwa wamearifiwa siku moja ghafla kwa kupigiwa simu, bila kuambiwa ukumbi wala madhumuni, zaidi ya kuambiwa wanatakiwa Dar es Salaam siku hiyo.

Wakati kikao kikiendelea, Lowassa aliwasili katika lango la kuingia kwenye hoteli hiyo saa 3.02 usiku akiwa ndani ya gari jeusi aina ya Toyota Lexus, akiwa amevaa suti nyeusi na shati jeupe. Alipokewa na viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe.

Baada ya hapo aliongozwa kuelekea chumba cha wageni mashuhuri (VIP) na kukutana na viongozi wachache wa chama hicho wakiwamo Mbowe na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohammed.

Mazungumzo hayo yalidumu kwa takribani dakika 18 na ilipofika saa 3.20 usiku, walitoka na kuingia katika ukumbi kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Chadema.

Lowassa alishiriki kikao hicho kwa takriban dakika 98 na ilipofika saa 4.58 usiku, alitoka katika ukumbi huo akisindikizwa na Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa, Makamu Mwenyekiti (Bara), Profesa Abdallah Safari, Mohammed na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu, ambao baadaye walirejea ukumbini kuendelea na kikao.

Hakuna upande wowote uliotaka kuzungumzia hali hiyo usiku huo, hadi siku iliyofuata ulipoitishwa mkutano wa wanahabari na kutangaza Lowassa kujiunga Chadema na Ukawa.

Habari za ndani

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilisema baada ya Lowassa kuwasili na kutambulishwa kwa wajumbe, alipewa nafasi ya kuzungumza.

Miongoni mwa mambo anayodaiwa kuwagusia ni pamoja na ukweli juu ya kashfa ya Richmond ambayo ilimlazimu kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008.

Pia, inaelezwa kuwa wajumbe walitaka kujua utajiri wake na baada ya kupewa majibu, walijadiliana jinsi ya kuiangusha CCM katika Uchaguzi Mkuu.

Saa 18 baada ya Lowassa kutambulishwa katika Kamati Kuu ya Chadema, viongozi wengine wa Ukawa waliitisha mkutano wa wanahabari siku iliyofuata na kumkaribisha rasmi katika harakati za uchaguzi uliokuwa na hamasa kubwa.

Viongozi hao walimtetea Lowassa na kusema hakuna aliyewahi kuthibitisha tuhuma dhidi yake na kuwa mfumo wa CCM ndiyo wenye matatizo ya rushwa na si mtu.

Profesa Ibrahim Lipumba alisema suala la ufisadi ni mfumo na si la mtu mmojammoja.

“Sisi tunaponda ufisadi na mfumo wa kifisadi na chanzo kikubwa cha ufisadi ni mfumo ndani ya CCM, kwanza tuing’oe CCM, hapo ndipo tutakapoweza kuondoa ufisadi na kujenga msingi wa kupambana na ufisadi na rushwa iliyopo.

“Lowassa alikumbwa na tuhuma za ufisadi mwaka 2008, leo ni 2015 lakini ufisadi umeongezeka au umepungua? Lowassa hayupo serikalini, Akaunti ya Tegeta Escrow imetokea wakati gani, Lowassa alikuwapo? Tatizo ni mfumo na jambo la kwanza ni kuing’oa CCM,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji ambaye baadaye aliteuliwa mgombea mwenza wa Lowassa, alihoji: “Mbona CUF iliwahi kupigana na kuuana na CCM mwaka 2000 lakini leo wameunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa?

“Makaburu waliuana wakamfunga Mandela (Nelson) lakini alitoka gerezani na kukaa chini akazungumza nao, kipi cha ajabu? Msumbiji walipigana vita miaka 18, lakini walikubaliana, basi kama Lowassa anakubali kwamba Ukawa ni muhimu kwa Watanzania, amezinduka na kuona hata bora aende Ukawa akafanye mabadiliko.”

Dk Emmanuel Makaidi alisema kama Lowassa angekuwa mbaya kiasi hicho, basi angekuwa amekwisha shtakiwa kama ilivyo kwa viongozi wengine ambao tayari wameshahukumiwa vifungo kwa matumizi mabaya ya madaraka au rushwa.

James Mbatia alisema Ukawa inamwalika kila Mtanzania aliye tayari kuuondoa mfumo kandamizi na dhalimu wa CCM na kwamba watashirikiana naye kujenga Taifa imara na Lowassa ni miongoni mwa wanaokaribishwa.