Hakuna daktari, mchungaji au mganga wa tiba ya ndoa

Ndoa nyingi zimevunjika kutokana na wanandoa kutojiamini na badala yake wakaamini miujiza au ushirikina.
Hakuna muujiza kwenye ndoa zaidi ya wanandoa wenyewe. Hakuna ushirikina unaoweza kuimarisha ndoa. Wahenga walisema; hakuna dawa ya mapenzi. Kama ipo si nyingine ni uaminifu, upendo, utayari, usiri, uwajibikaji, matendo, na maneno mema baina ya wahusika.
Tumeweka ushirikina na ushauri pamoja kutokana na uzoefu wetu. Tunajua. Kuna wanandoa walioishiwa hadi kuamini kuwa maombi, tunguli, n.k. vinaweza kuokoa ndoa ambazo wameziua tokana na ujinga na upumbavu wao.
Tangu tumeoana, hakuna kitu tulichojiepusha nacho kama kuweka mambo yetu ya ndani siyo nje tu ya nyumba yetu bali nje ya chumba chetu cha kulala ambayo ndiyo makao makuu ya ndoa yetu. Haiingii mtu yeyote humo isipokuwa watoto wetu wachanga tu.
Siri za humo hazitoki hata kwa viboko. Hivyo, unapoanza kuingiza mashoga kwenye chumba chako cha kulala na baadaye kwenye kitanda chako ujue unamtafuta na kumtengeneza mchawi au wachawi wa ndoa yako.
Tusisitize mambo makuu yafuatayo:
Mosi, ndoa yako ni siri yako binafsi asiyopaswa kujua mtu yeyote. Ndoa siyo gazeti wala kitabu ambacho unaweza kusoma na wenzako. Ndoa yako ni siri kuliko hata nguo zako za ndani, maana huwa unazinunua au wengine kuzianika zikaonekana. Ndo ani kama moyo wako. Anayeweza kuuona ni daktari wako pekee na Mungu aliyeuumba.
Pili, chumba chenu cha kulala ni sehemu ya siri asiyopaswa kuijua wala kuingia mtu yeyote isipokuwa wawili nyinyi. Hivyo, wale wanaowaruhusu mashoga au wasichana wao wa kazi kuingia kwenye chumba chao cha kulala ni makosa makubwa.
Tatu, matatizo yako ya ndoa yanapaswa kutatuliwa na wawili. Kwanini iwezekane kuyatengeneza mshindwe kuyatatua? Ushauri wa mashoga na marafiki hausadii. Hawajui thamani ya ndoa yako. Na lolote baya likitokea, wao hawatakuwapo.
Kitanda usicholala hujui kunguni wake. Hapa lazima usiri uwepo na si usiri tu bali hata hofu na kutomwamini mtu yeyote. Hata inapotokea ukapata ushauri, lazima uupime kwa kuangalia thamani ya ndoa yako na si mawazo ya aliyekupa ushauri. Kupewa ushauri ni jambo moja na kulifanyia kazi ni jambo jingine.
Hakuna anayefungwa na ushauri wa mtu yeyote. Kupanga ni kuchagua. Unapopanga au kuchagua, fanya hivyo vizuri ukijua wazi. Ndoa yako ni sawa na kaburi. Tunatoa mfano huu siyo kwa sababu ya kukutisha. Tunataka upate ujumbe kama ulivyokusudiwa.
Hebu piga picha mtu anapokufa. Kuna mtu anaweza kumsaidia kukaa kwenye kaburi lake? Msaada pekee hapa ni kumchimbia kaburi na kumuingiza wakimuacha mhusika aingie na kuishi kwenye kaburi lake. Unaweza kuugua au kuhisi njaa na kupata msaada lakini si kwenye kaburi. Samahani kwa kutoa mfano wenye majonzi ingawa ndiyo hali halisi.
Huu ndiyo ubinadamu tunaopaswa kuukubali katika maisha yetu. Maisha ni safari ndefu yenye kona, mabonde na mito, milima. Hakuna Daktari, mchungaji, mganga, fundi wa ndoa wala mwalimu bali wanandoa wenyewe kuwa tayari kuilinda ndoa yao, kujifunza, kufundisha, kujielimisha, na kuelimishana. Tumeyaona. Tumeyapitia.