Prime
Hii tofauti kati ya wastaafu wa nchi moja inakujaje?
Ni wakati sasa wote tukae chini na kujadiliana kikweli kweli bila unafiki kwa nini yule George Orwell alisema kwenye tamthiliya yake ya 'Shamba la Wanyama' kuwa wanyama wote wako sawa lakini kuna wanyama wengine wako 'sawa' zaidi kuliko wengine!
Tufungue macho kikweli kweli tumuangalie huyu mstaafu wa Taifa ambaye ndiye ameijenga nchi hii mpaka kufika hapa ilipo kwa kwa kujenga madaraja, barabara, shule na hospitali kwa mikono, jasho na damu yake mwenyewe.
Ameilinda na kuipigania nchi yetu na zile zilizotuomba tuzisaidie kupambana zipate Uhuru wa kweli wake zenyewe kama sisi.
Hakika Baba wa Taifa letu hili naye angependa kuwa na makoloni kama wale akina naniliu.
Leo na sisi tungekuwa sio haba, tungekuwa na 'makoloni' Msumbiji, Zimbabwe, Uganda na kwing-ineko. Bahati yao!
Inasikitisha sana kwamba mstaafu huyu wa kima cha chini aliyefanya kazi ya kutukuka ya kuijenga nchi na kuilinda kwa jasho, damu na hata uhai wake, mpaka leo miaka 64 baada ya Uhuru na baada ya kustaafu' anapata pensheni ya mwezi ya shilingi laki moja na elfu hamsini ! Ni aibu.
Rudia tena, ni aibu. Yaani mtu aliyeijenga na kuilinda nchi yake huku mshahara wake ukikatwa 'Lipia Upatacho' PAYE, ili watoto wa Taifa hili wasome bure na kutibiwa bure, leo asante ya Taifa lake kwake ni kumlipa pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini kweli?
Yaani hawa tuliowasomesha bure Kwa 'Pay As You Earn zilizokatwa kwenye mishahara yetu, ambao leo wako kwenye nafasi 'zinazoeleweka' wanajikausha na kuishia kumfanya mstaafu apokee shilingi laki moja na elfu hamsini. miaka 64 baada ya Uhuru? Nauliza mara tatu, kweli? Kweli? Kweli?
Ilitegemewa kwamba, wastaafu wenyewe hawa wa kima cha chini, kama sio cha chizi sasa, na ambao sasa wamebaki wachache tu basi Taifa lingechukua hatua za haraka na utashi wa kweli wa ku-waboreshea' kweli ustaafu wao, angalau Kwa shilingi Laki Tano Kwa Mwezi. Inawezekana. Ni Utashi TU.
Taifa na mifuko kibwena ya wastaafu, imeshindwa kuwapa na hata matibabu ya bure wazee wa Taifa hili.
Ahadi ya matibabu ya bure imeishia kuwa maneno ya kanga tu, tena zile rejekti na afya zao zimeshia kuwa jukumu la watoto wao wenyewe ambao bado wanatafuta ajira kwa kurunzi huku wabunge wao wakikazana kuwataka wajiajiri. Cha ajabu sasa ni kuwa nchi imekuwa kama shamba la wanyama, kweli aliloandika Orwell kwenye tamthili ya yake kuwa wanyama wote ni sawa lakini kuna wanyama wengine wako sawa zaidi kuliko wengine. Ni kweli.
Sasa wapo 'wanyama' wanaopata asilimia mpaka 80 ya wanayopata mema ya shamba letu la wanyama walio madarakani.
Fasta inapitishwa kanuni ya kuwalipa wenza wao pande, sio kipande, cha keki ya Taifa. Mwenza wa Mstaafu? Ndio nani?
Mstaafu wetu wa kima cha chizi ambaye wajukuu zake sasa wanakimbizana na kikokotoo, anaishia ku-lalama na shilingi laki moja na elfu tano yake kwa mwezi lakini ameahidiwa kupata shilingi milioni tano na laki tano akiwa maiti, mkazi wa Kinondoni, sio akiwa mzima. Mwe, tena!
Ni kweli mlifanya kazi kubwa ya kukaa ofisini kwenye kiyoyozi mkisoma faili hili na kuingia mkataba Ile lakini mstaafu huyu wa kima cha chini ndiye aliyechimba mitano, alihakikisha zege hali lali na ndiye ali-yeweka lami na ndiye aliyemtoa bali nduli Amin. Mbona kwenye mema ya nchi mmemsahau? Narudia tena, mbona kwenye memba ya shamba la wanyama mmemsahau?
Waheshimiwa, waheshimiwa, waheshimiwa, nawaita mara tatu. Mpeni mstaafu hizo milioni tano mnazomuahidi kumpa akiwa tayari mkazi wa Kinondoni, Rubengera au wapi sijui, apoze masaibu yake kweli Sio haya maneno ya kanga rejekti. Ndugu zake zake watamzika bila milioni tano yake iliyo kwenu mnayomringishia!
Shamba letu la wanyama linapaswa kuwa letu sote na hakuna haki ya wanyama wengine kuwa sawa zaidi kuliko wengine! Yanyoosheni haya.
0754 340606 / 0784 340606