Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hongera kwa INEC kuweka sawa uwanja wa kisiasa

Kwa muda mrefu, mijadala ya kisiasa Tanzania imekuwa ikitawaliwa na malalamiko ya kutokuwapo kwa uwanja sawa wa ushindani katika siasa.

Mara nyingi, vyama vikubwa vyenye rasilimali na nguvu za kifedha vimekuwa vikihusishwa na nafasi kubwa ya kunufaika, huku vyama vidogo vikibaki nyuma vikikosa uwezo wa kushindana kwa usawa. Hali hii imefanya wanasiasa wengi na wachambuzi wa masuala ya uchaguzi kuutaja uwanja wa siasa wa Tanzania kama “uwanja tenge.”

Lakini safari hii, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeanza kuchukua hatua za kurekebisha kasoro hizo. Hatua yake ya hivi karibuni ya kuwawezesha wagombea wote wa kiti cha urais kwa kuwapatia gari, dereva na mlinzi wa serikali ni jambo la kupongezwa kwa dhati.

Ni hatua ndogo, lakini yenye maana kubwa kwa mustakabali wa demokrasia nchini. Hatimaye, wagombea wote 17 wa urais sasa wanapata fursa sawa ya kuzunguka nchi nzima na kuwasilisha sera zao kwa wananchi. Kwa miaka mingi, uchaguzi nchini Tanzania umekuwa ukifananisha na mashindano ya kugombea nyama kwa kutumia visu vya makali tofauti.

Wale wenye kisu kikali, huambulia minofu, huku vyama vidogo vikibaki na mifupa. Hali hiyo haikuwa ya haki na kwa kiasi kikubwa ilipunguza imani ya wananchi katika mfumo wa kidemokrasia.

Kwa mara ya kwanza, hatua ya INEC inasaidia kupunguza pengo hili. Kwa kugawa magari ya kisasa aina ya Landcruiser GX VXR, pamoja na madereva na walinzi kwa wagombea wa urais ambao sasa wana uhakika wa kufika kila kona ya nchi bila changamoto kubwa za kifedha. Hili ni jambo la kupongezwa, hususan kwa vyama vidogo ambavyo awali vilikuwa vikihaha hata kupata fedha za kulipia fomu za kugombea, sembuse gharama za kampeni kubwa.

Hata hivyo, changamoto bado ipo. Gari pekee bila mafuta ni kama jiko bila kuni. Vinginevyo, magari hayo mazuri yatabaki maonesho bila kufanya kazi iliyokusudiwa.

Pamoja na pongezi hizi kwa INEC, swali linalojitokeza ni: vipi kuhusu vyombo vya habari? Kama wagombea wamewezeshwa, je, media nayo imewezeshwa ili iweze kuwafikia wananchi wote?

Ukweli ni kwamba, bila uwezeshaji wa vyombo vya habari, bado tutaendelea kushuhudia upendeleo usio rasmi. Vyama vyenye nguvu na uwezo wa kifedha vitaendelea kutawala anga za habari, wakati vyama vidogo vikibaki gizani. Moja ya wagombea tayari ana chombo kikubwa cha habari cha serikali na msaada wa miundombinu ya dola, jambo linalompa faida kubwa dhidi ya wenzake.

Hili likiachwa, itakuwa sawa na kurekebisha upande mmoja wa uwanja huku upande mwingine ukibaki na mashimo.

Hivyo basi, serikali na wadau wa uchaguzi wanapaswa kuziwezesha pia media zetu. Waandishi wa habari, wahariri na watayarishaji wa vipindi wanahitaji rasilimali ili kufanikisha kazi ya kuwahudumia wagombea wote 17 bila upendeleo.

Bila msaada huu, maudhui ya habari yatabaki yakimilikiwa na wachache wenye uwezo, hali itakayopotosha taswira ya demokrasia. Ni jambo la kutia moyo kwamba Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, ameahidi tume kushirikiana na vyombo vya habari kwa karibu. Ameeleza kuwa tume itatoa taarifa sahihi na kwa wakati, na pia kuzindua mfumo wa kusajili vyombo vya habari na kutoa vitambulisho rasmi kwa waandishi.

Hatua hii itasaidia kuhakikisha kuwa habari zinazotolewa ni za kuaminika na zinapatikana kwa usawa. Hata hivyo, kusajili vyombo vya habari pekee hakutoshi.

Kile kinachohitajika zaidi ni uwezeshaji wa kifedha na kiufundi ili kuhakikisha vyombo vya habari vinakuwa na uwezo wa kurusha habari za kampeni kutoka kila pembe ya nchi. Hapo ndipo wananchi wataweza kufanya kile kinachoitwa “an informed decision” uamuzi sahihi unaotokana na kupata taarifa kamili na za pande zote.

Kwa ujumla, hatua ya INEC ya kuanza kusawazisha uwanja wa siasa ni mwanzo mzuri wa safari ndefu kuelekea uchaguzi wa haki na huru.

Lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Pamoja na magari, wagombea wanahitaji rasilimali nyingine kama mafuta, vifaa vya kampeni na usaidizi wa kiufundi.

Vyombo vya habari navyo vinapaswa kupewa nafasi na rasilimali ili kuwasikilizisha Watanzania sauti za wagombea wote bila upendeleo.

Iwapo serikali na tume wataendelea kuchukua hatua za aina hii, Tanzania inaweza kuanza kufanana na nchi zenye mifumo imara ya demokrasia kama za Scandinavia na Nordic, ambako wagombea wote hupewa nafasi sawa na wananchi hufanya uamuzi kwa kuzingatia sera na siyo uwezo wa kifedha wa chama.

Ni matumaini yetu kwamba, hatua hii haitakuwa ya pekee, bali itakuwa chachu ya mageuzi ya kudumu yanayolenga kujenga demokrasia yenye usawa, haki na uwajibikaji.