Kiki zinavyopoteza imani za mashabiki kwa wasanii

Muktasari:

  • Kiki imekuwa jambo la kwanza linalopewa kipaumbele na baadhi ya watu maarufu, hasa kwenye Tasnia ya Burudani nchini, wakiamini kuwa ni njia ya kusukuma kazi zao ziende kirahisi.

Dar es Salaam. Kuna msemo usemao msanii ni kioo cha jamii, hii ni kutokana na wanayofanya kutazamwa zaidi na mashabiki wao, huku mengi yakiigwa kutoka kwao. Kioo hiki kimekuwa tofauti miaka ya hivi karibuni, kwani wasanii wamepoteza uaminifu kwa jamii kutokana na baadhi ya matendo wanayofanya kujaa uongo na maigizo.

Kiki imekuwa jambo la kwanza linalopewa kipaumbele na baadhi ya watu maarufu, hasa kwenye Tasnia ya Burudani nchini, wakiamini kuwa ni njia ya kusukuma kazi zao ziende kirahisi.

Tanzania siyo ajabu msanii kujizushia kifo, ajali, ugonjwa, ugomvi, na mengineyo. Ili jina lake lizungumzwe. Kama ilivyotokea Feb 2, 2020 kwenye kiki ya msanii wa muziki wa singeli Meja Kunta, baada ya meneja wake G Maker kutangaza msanii huyo amefariki dunia kwa ajali, akielekea katika tamasha la muziki mnene jijini Tanga.

Tukio hilo lilizua taharuki kwa mashabiki wa msanii huyo kabla ya kujua kuwa taarifa hizo za uongo zililenga kuwa kiki. Kutokana na kiki hiyo Feb 7,2020, Meja aliomba radhi, huku akisema kuwa kifo ni kitu cha kawaida.

Si Meja tu yapo matukio mengine. Msanii Baba Levo siku za hivi karibuni alimtuhumu Harmonize kwa kumpiga na kumsababishia maumivu sehemu za mwili wake, tukio hilo linaweza kuwa la kweli lakini kwa tabia za baadhi ya  watu maarufu limepelekea kuibua mitazamo mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, wapo wanaodai ni kiki.

Chino Kidd na Marioo wanadaiwa kuwa kwenye migogoro, kama Chino alivyoieleza Mwananchi kuwa chanzo cha mgogoro wao ni baada ya Marioo kushindwa kufika kwenye ‘pati’ yake. Mgogoro huu pia wapo wanaodai huenda ukawa kiki.

Mwezi uliopita Mwananchi ilifanya mazungumzo na mchekeshaji Kago, anayetamba na msemo wa 'bado hujasema, kati ya vitu ambavyo mchekeshaji huyu alizungumzia ni mgogoro wake na mwanamuziki Mavokali, kwa kusema kuwa hawakuwa na mtatizo yoyote badala yake walifanya kiki ya kusukuma ngoma ya Mavokali 

Ilivuja video kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mchekeshaji Tin White akigombana na mwanamuziki Yj Kiboko, bado watu wakadai huenda ni kiki. Lipo tukio la mwanamuziki Nandy kupokea Dm kutoka kwa mwanamuziki wa Marekani Usher lakini wapo waliodai huenda ikawa siyo tukio la kweli likawa kiki ya kusogeza wimbo.

Feb 12 Producer wa muziki nchini Master J alionekana kuchukizwa na baadhi ya watu wenye tabia ya kupiga picha na video misibani, kisha kuweka kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii. Inawezekana kati ya ‘wanaoposti ‘ matukio hayo wakawepo wenye huzuni kweli, lakini kutokana na kiki ambazo baadhi ya watu maarufu wamezoea kuzifanya inapelekea kila wafanyacho kionekane kina mlengo wa kutafuta kiki.

Si hivyo tu yapo matukio mengi yanayofanya jamii ipoteze imani kwa watu maarufu hasa waliopo kwenye upande wa burudani.

Hivyo basi wasanii wana kila sababu ya kuhakikisha wanarudi nyuma na kuangalia walipokosea ili kufuta mitazamo ya kiki iliyopo kwenye vichwa vya mashabiki wao, kwani tayari jamii haitaki kuamini wanayofanya na kuamini kila wakifanyacho kinaongozwa na maigizo.