Kilio cha mstaafu kihamie kwenye ubunge wa kuteuliwa
Baada ya miaka 20 ya kuomba na kubembeleza kupewa nyongeza ya pensheni kwa wastaafu wa kima cha chini walioijenga nchi kwa jasho na damu, hatimaye kimesikilizwa na kufanyiwa kazi.
Ingawa si kama walivyotegemea wastaafu hao ya kuongezwa shilingi alfu hamsini kwa miaka 20 ambayo mpaka ‘Njaanuari’ hii nyongeza hiyo bado iko kwenye makaratasi badala ya mifukoni mwao, mstaafu ameona hili lingine alipigie kelele.
Kuna hizi nafasi za ubunge wa kuteuliwa anazokuwa nazo mheshimiwa anayechaguliwa na wananchi kuiongoza nchi yetu njema ya Tanzania.
Mstaafu wetu hana hakika kama ziliongezwa au la, lakini anakumbuka mheshimiwa anayeteuliwa kuiongoza nchi anazo nafasi 10 za kuwachagua watu anaoona wanafaa kwenye kazi ya kumsaidia katika kuiongoza na kuijenga nchi. Nafasi 10 za wabunge wa kuteuliwa.
Hawa wanaweza kuwa walishindwa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea ubunge, ingawa mshahara wa milioni 14 kwa mwezi unawafikirisha!
Wapo pia wale ambao hawapendi kuwaahidi watu mambo ambayo hayako kwenye uwezo wao, bali na wao hulazimika kuomba kunakohusika ili walivyoahidi vitekelezwe.
Mstaafu wetu ameona apaze sauti kwa mheshimiwa atakayechaguliwa na wananchi wa nchi hii mwaka huu wa uchaguzi mkuu kwenye zile nafasi zake 10 alizowekewa za kuwateua anaowaona watamsaidia kwenye kuiongoza nchi yetu, japo si wabunge bali hata marafiki zake aliosoma nao shule, atenge nafasi mbili kwa ajili ya wastaafu, mwanamume na mwanamke, wawe wabunge wa kuteuliwa. Inawezekana.
Ni utashi tu na nchi hii ni yetu sote. Kwenye nafasi zake 10 za kuteua wabunge, mheshimiwa wetu atenge nafasi mbili kwa ajili ya wastaafu wawili, mwanamke na mwanamume, kuingia bungeni waweze kusema yale yote yanayowasibu wastaafu wa Taifa kwa karibu zaidi na kwa sauti zaidi.
Mstaafu wetu anapenda kuamini kungekuwa japo mstaafu mmoja bungeni tangu awamu mbili zilizopita, nyongeza ya pensheni ya wastaafu isingechukua miaka 20 ili kuipata.
Ndiyo, matibabu ya bure yangekuwepo kwa wastaafu, benki ya wastaafu inayotoa mikopo yenye riba nafuu kwao ili kuwasaidia ingeanzishwa na wale wastaafu ambao hawakupata kuajiriwa lakini waliweza kulisha Watanzania walioajiriwa kwa kilimo walichofanya nao wangefanyiwa utaratibu fulani ili kupata ‘kifuta jasho’ cha kuwasaidia, tofauti na sasa ambako kelele zote zipo kwa wastaafu walioajiriwa kama vile nchi hii haijapata kuwa na wastaafu wakulima.
Wabunge wastaafu wa kuteuliwa watakaoteuliwa watakuwa na kazi moja tu kubwa ya kupiga kelele bungeni ili kuhakikisha wastaafu wenzao wakulima wanakatiwa kipande cha keki ya Taifa wanachostahili kwa kuweza kuwalisha wananchi wakati nchi inapambana kupata uhuru wake na wakati wa kuijenga nchi kwa jasho na damu la ulimaji wao. Tuifufue ile ‘matibabu ya bure’ kwa wazee wa miaka 60 na kuendelea. Wanastahili. Wao hawana hata hiyo ‘Laki si pesa’ tangu tupate uhuru.
Bungeni tunao wabunge wa kuchaguliwa na wa kuteuliwa, wanaosimamia mambo ya wanawake, wanaosimamia mambo ya vijana na hata wanaosimamia mambo ya watoto.
Hakuna mbunge wa kuchaguliwa au wa kuteuliwa ambaye yuko bungeni kwa ajili ya kuzungumzia wastaafu tu.
Waliopo huwa wanatoa hoja tu zinazohusu wastaafu na mambo yanaishia hapo. Hakuna kinachoendelea. Ni hoja tu.
Mara kadhaa tumependekeza kuwe na jimbo maalumu la wastaafu ambalo wastaafu watatafuta namna yao ya kuchagua wabunge wawili, mwanamume na mwanamke, walio wastaafu kweli ili kwenda bungeni kusimamia mambo yao, kama hili la kupata nyongeza ya pensheni yao baada ya miaka 20 au hili la kufutiwa matibabu yao ya bure kwa wazee wa miaka 60 na zaidi walioijenga nchi, lakini imekuwa hadithi tu.
Mheshimiwa atakayechaguliwa na wananchi kuiongoza nchi alitizame kwa makini hili.
Wabunge wawili watakaoteuliwa kuingia bungeni kusimamia hoja za wastaafu wenzao watakuwa hawafanyi hivyo ili kupata mshahara wa wabunge wa shilingi milioni 14 kwa mwezi. Mstaafu ana miaka 70 na kuendelea, milioni 14 na marupurupu na marapurapu yake inaweza ikawa hata milioni 16 kwa mwezi! Azipeleke wapi? Yeye hata ukimlipa milioni tano kwa mwezi itamtosha, inayofaa kwa waheshimiwa wote wanaoingia bungeni ili kubana matumizi na anayeona ni ndogo aachie mchuma upuyange!
Mstaafu anataka ateuliwe kuingia bungeni akawashe moto kuhusu haki za wastaafu, waajiriwa na wakulima waliojenga Taifa hili ambalo kuna watu wanaonekana kusahau kuhusu hili na sana sana wanataka mstaafu awe mwajiriwa au mkulima aelekee Kinondoni fasta! Na hawajali, wastaafu wenyewe wa kima cha chini waliojenga nchi hii, mpaka ikaonekana kwamba ni Tanzania kweli wako wangapi?
Kwa miaka yake 70 na kuendelea, tunaamini mstaafu mwenzetu atakayeteuliwa atazungumza yale yanayomkabili mstaafu wa Taifa tu na hatazungumza kwa kujilengesha ili ateuliwe! Aende wapi na uzee wake?
Kuna mengi yanayomkabili mstaafu. Ya nyongeza ya pensheni yamekwisha, japo kwa nyongeza ya Sh50,000 baada ya miaka 20. Tuanze kusaka wastaafu wenzetu wawili wateuliwe kuingia bungeni. Inawezekana, ni utashi tu.