Kwa matokeo haya, Waziri Mkenda wajibika

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

Sina budi kuanza makala haya kwa kuipa pongezi nyingi Serikali chini ya jemedari wake, Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo imehamasisha na kuwekeza kwenye elimu.

Mwitikio umekuwa mkubwa, wanafunzi wengi wamejitokeza kuchangamkia elimu ambayo japo inaitwa elimu bure, lakini sio bure kwa maana halisi ya bure, tunalipia sisi walipakodi wa nchi hii.

Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya elimu ikiwemo kujenga madarasa, madawati, vitabu na zana nyingine za kufundishia na kujifunzia.

Pamoja na juhudi zote hizi kubwa zinazofanywa na Serikali, Waswahili wanasema kuwa hakuna kizuri kisicho na kasoro. Bado shule nyingi hasa za sekondari zina uhaba mkubwa wa walimu hasa masomo ya sayansi.

Serikali ya awamu ya nne ilikuja na mpango maalum wa kuwasomesha vijana kwa kozi za muda mfupi ili waje kuziba pengo la uhaba wa walimu wa sayansi.

Bahati mbaya mpango huo baadae ulihujumiwa, hata wale vijana wachache waliomaliza kozi hizo bado hawajaajiriwa na Serikali

Serikali inapotumia pesa nyingi katika kuboresha elimu halafu wanatokea wanafunzi katika shule za serikali kufeli kwa kiwango cha kutisha, inasikitisha sana na kukatisha tamaa wazazi kupeleka watoto wao huko.

Mwanafunzi aliyepata sifuri ni sawa na asiyekwenda shule maana hata cheti hapati, lakini asiyeenda shule ana nafuu maana hakuna gharama yoyote aliyoitumia.

Huyu aliyepata sifuri kuna gharama za walipa kodi na hata za wazazi wake zilizotumika miaka minne akiwa shuleni alikokwenda kuongeza umri wa kuishi na sio kujifunza.

Turudi kwenye mada husika. Ni matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni. Shule inapokuwa na sifuri 474 na daraja la nne 533 tena shule yenyewe ikiwa kilomita chini ya 10 kutoka Ikulu, hilo halipaswi kupita hihivivi bila ya wahusika kuwajibika hasa waziri mwenye dhamana ya kusimamia elimu.

Nimemkumbuka hayati Augustine Lyatonga Mrema,alipokuwa Waziri wa Mambo ya ndani. Lilipokuwa linatokea suala ambalo linaigusa wizara yake mahala, alikuwa halali bila kufika yeye binafsi na kutaka kujua kulikoni, na alikuwa akichukua hatua mara moja kwa kadri ilivyokuwa inawezekana.

Sasa ninajiuliza, kwa shule iliyoko karibu na Ikulu kufelisha wanafunzi kwa kiwango hicho, waziri mwenye dhamana na elimu amechukua hatua gani za haraka kuokoa jahazi? Je, amefika shuleni kujionea tatizo.

Serikali ilipoamua kujenga shule za kata, ilidhamiria kuweka usawa na uwiano wa kielimu katika mikoa yote na kuondoa malalamiko kuwa kuna wananchi wanaopendelelewa kielimu.

Mradi huu wa shule za kata ulipata wapinzani kadhaa ambao hawakuupenda, hasa wale ambao walidhani wao ndio wenye haki ya kupata elimu; waliingiwa na hofu pengine kwa kudhani kuwa watu wengi wakielimika, wao wataporwa nafasi zao za kazi.

Mungu sio Athumani, Serikali iliziba maskio ikaendelea na mradi wake, wapingaji walipoona kuwa upinzani wao wa wazi umeshindwa, wakaja na mbinu mpya ya kuhakikisha wao tu na vizazi vyao wanabakia na haki ya elimu.

Mbinu zenyewe ndio hizi za kuacha watoto wa maskini wanaenda shule kweli lakini wanaondoka na ‘sufuria’. Wakati mwingine inakuwa vigumu kuamini kuwa mtu mwenye dhamana ya kusimamia elimu, mwenye taaluma ya hali ya juu, anaacha hali kuwa kama tunavyoshudia hivi sasa.

Ni kweli waziri amekosa au ameishiwa mbinu za kubuni kuhakikisha hali hii ya kufeli haitokei? Yeye si ndiye anayepanga bajeti ya sekta ya elimu? Bajeti inapopangwa haizingatii makadirio ya idadi ya wanafunzi kwa uwiano wa walimu?

Kama elimu bure maana yake ni kufelishwa watoto wa KItanzania kwa kiwango hicho, bora tuangalie upya. Afadhali mzazi akalipia kidogo kuliko mtoto wake kwenda shule na kutoka na sufuria!

Mwezi uliopita niliangalia kipindi cha Malumbano ya hoja ambapo Viongozi wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi ( Tamongsco), walikuwa wakilumbana na wadau wa elimu.

Mwenyekiti wa chama hicho wakati anajibu swali kuhusu ada zinazotozwa na shule binafsi, alisema kuwa ada wanayotoza wao iko chini ya ile inayopangwa na Serikali kwenye shule zake.Nakumbuka alisema kuwa bajeti ya Serikali kwa kila mwanafunzi ni zaidi ya Sh4 kwa mwaka, wakati wao wanatoza chini ya hapo.

Mwenyekiti akashauri kwa kuwa shule binafsi wana miundombinu bora ya kuweza kuchukua wanafunzi wengi, Serikali ihamishe wanafunzi kutoka katika shule zake ambazo zimezidiwa iwapeleke shule binafsi na kuwalipia hata kwa Sh200,000 kila mwanafunzi wao wako tayari kuwapokea. Huu ni ushauri kuntu sana kwa Serikali, lakini nani anasikiliza?