Haki, ukweli, uhuru na usawa hujenga amani na umoja
Muktasari:
AMANI na umoja katika nchi, siyo mambo yanayoletwa kwa kutamani, kutumia mabavu, uzaini, hadaa, dharau, vitisho, ukubwa, ngomba na nyimbo.
AMANI na umoja katika nchi, siyo mambo yanayoletwa kwa kutamani, kutumia mabavu, uzaini, hadaa, dharau, vitisho, ukubwa, ngomba na nyimbo.
Ni vitu vinavyohitaji mkataba wa kijamii na maridhiano kati ya wanajamii, ili viweze kuwepo na kudumu miaka mingi baada ya walio hai leo, kuwa wamekwishakufa na kusahaulika.
Dhana za haki, ukweli, uhuru na usawa zilizaliwa siku nyingi kabla ya ujio wa televisheni za dijito, simu za mkononi, intanenti na vikorombwezo vingine vya teknolojia za mawasiliana na habari.
Zilikuwa ni zama za kina Rousseau, Locke na kina Karl Marx na wenzie, ambapo teknolojia ya uchapishaji ndiyo kwanza ilikuwa ikionekana kuwa kitu kipya. Wakati maneno ya wanafalsafa yalithaminiwa zaidi, kuliko ya watawala na mangimeza.
Dhana hizi zimetumika kwa miaka mingi kabla watu hawajajijua walipo, hawajajitambua nguvu na uwezo wao na walipokuwa wakifunikwa na shuka na mblanketi ya kisiasa na kiutapeli hali ya kwamba ni saa sita mchana kama vile wamelala.
Ninaamini kwamba, katika miaka hiyo kabla mtu hajafungua mdomo kuongelea lolote kuhusu sheria, haki, usawa, uhuru, ukweli na mambo kama hayo, kwanza ingelifaa ajitoe kwenye zama za giza na ujahilia kisha kujiingiza kwenye zama za teknolojia na vijana.
Bila kujali ni wakati gani tuliomo, iwe baada ya kompyuta au kabla ya kompyuta, ili amani na umoja viwe vitu vya kudumu na kuenziwa katika nchi, kila raia bila kujali nafasi aliyokuwa nayo ni lazima aheshimu vitu vinne vikuu.
Vitu hivyo ni haki za wenzake, uhuru wa wenzake, usawa na wenzake na kuepuka uongo na uzushi dhidi ya wenzake. Na je, hivi tuna uhakika na uzima wa kiakili wa watumishi tulio nao serikalini sikuzote, wakati wote?
Katika hali ambayo siyo siri, kila kitu kiko wazi kwamba kuna imani zinazoamini kwamba, imani nyingine inapendelewa na wao wanaonewa. Hivi kweli, mtu utaweza kuzungumzia kujenga amani na umoja katika mazingira kama hayo?
Kwa nini, tusichukue muda kuwa wawazi na wakweli na kuwapa nafasi wanaohusika kumaliza tofauti zao na mashaka na tuhuma zilizoko kati yao viwe vimezikwa kwanza kwenye kaburi la sahau, ndipo tuzungumzie umoja na amani.
Tukiyapitia masuala haya kijuujuu na kufanya kama vile hatuoni walakini, hivi kweli tutawatendea wananchi na nchi hii haki?
Je, kweli inatawala katika habari na taarifa zetu mbalimbali. Idara zinazohusika katika ngazi za chini, je, zinawasilisha ukweli na siyo upotoshaji kwa ngazi za juu na ukweli ukawa ukibaki chini na katikati na kamwe haufiki juu siku zote?
Ni vyema pia kuzichunguza idara na taasisi nyingine nchini na kuona kwamba haziuzi haki, wala haziwaibii watu haki zao, kisha wakawa wakisema uongo. Na kwa kutumia nafasi yao waliyopewa kimamlaka, wakauzika uongo huo kwa hasara ya leo na kesho kwa nchi na watu wake. Na kama kwa bahati mbaya vyombo vya habari vimelemazwa kwa njia moja au nyingine, kweli isigundulike kabisa ?
Inafaa pia kujiuliiza, je, wananchi wana uhuru wa kushiriki katika uamuzi na mipango inayoandaliwa na Serikali yao. Au wao ni wapokeaji toka juu, kwa yote yanayoamriwa kuhusu maisha yao ya kila siku. Na hakuna anayejali kama wanashirikishwa au la?
Nadharia za uhuru, huongelea kwa kiasi fulani uhuru wa mtu binafsi, uhuru wa makundi katika jamii, uhuru wa maeneo katika nchi (madogo kwa makubwa) na uhuru wa nchi nzima. Je, ni kwa kiasi gani wananchi katika nchi husika wanajiona wanafaidi aina za uhuru wanazostahili kuwa nazo bila vikwazo au mikwara?
Itakuwa jambo la busara siyo tu wakati huu wa kuchangia mawazo katika Katiba kutoa michango ya kisheria tu, bali wananchi wapewe fursa pia ya kuchora na kutoa visheni ya je, ni Tanzania ya aina gani ambayo wao, watoto wao, wajukuu na kizazi chao wangelipenda waishi?
Laiti tungelitambua tangu awali, mimi binafsi ningependa kuona tunazungumzia kwanza maadili na visheni ya kimataifa, kabla ya kuzungumzia Katiba. Maana pasipo kuwa na maadili madhubuti, kuwa na katiba peke yake hakuna tofauti ya kuwa na gari bila ya magurudumu.
Vidonda vya amani na umoja
Ili kuhakikisha amani na umoja unaotafutwa vinakuwa ni vitu vya kweli na uhakika, na siyo maneno na danganya toto za kisiasa na kwamba vinapandwa kwenye ardhi yenye rutuba na itakavyovikubali bila tatizo, sasa ni lazima kuanza kubaini vidonda na majeraha yaliyopo na jinsi ya kuyashughulikia ili visijegeuke kuwa ugonjwa mkubwa.
Katika haki, inafaa kujiuliza hivi vyombo vilivyokabidhiwa dhamana ya kuona kwamba haki siyo tu inapatikana, bali inaonekana kutafutwa ili ipatikane na anayeistahili asidhulumiwe ?
Je, kati ya Serikali na raia, kuna anayependelewa katika kupewa haki au upendeleo wa aina nyingine na mwingine kuonewa?
Je, taasisi na watumishi katika idara mbalimbali kama vile zile za polisi, mahakama na ofisi ambatanishi, magereza na uongozi wa nchi kwa ujumla wanaheshimu haki na hawako juu ya sheria na Katiba ?
Je, kuna uwezekano wa kuwa baadhi ya uhuru wa watu unakwaza au kuminywa kwa njia moja au nyingine. Na hata kama watu wana uhuru mkubwa, je, hakuna nafasi zaidi ya kupanua na kustawisha uhuru huo kwa faida ya mtu binafsi na nchi nzima kwa jumla ?
Moja ya kifungu kinachosahaulika sana katika Katiba au kugusiwa kijuujuu ni kile cha...9(d) ambacho kwa Kiingereza kinasema: '(d) that the national economy is planned and promoted in a balanced and integrated manner.'
Wasiwasi wa watu katika kuchangia Katiba Mpya umedhihirisha kuwa hofu ya watu wengi ni kuwa kama mkoa wenu hauna waziri au naibu waziri au waziri mkuu, basi siyo rahisi kuendelezwa! Husahaulika kwa muda mrefu, hasa ukizingatia kwa kiasi kikubwa bado tuna Bunge ambalo chama kimoja tu ndicho chenye sauti inayosikilizwa.
Mara baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi Tanzania kama nchi pamoja na makabila ya asili 120, imejikuta ina makabila mapya mawili: Watawala na Wapinzani. Watawala ndiyo wenye ajira serikalini na katika kila mamlaka na uwakala nchini. Wapinzani na wasio wanachama wa chama tawala hawafikirii kwenye ajira nzito na za maana. Kwa maneno mengine, nchi haina usawa kabisa.
Nia na madhumuni ya insha hii ni kujaribu kuwakumbusha Watanzania kuwa amani na umoja siyo vitu vinavyokuja hivi hivi vyenyewe kwa kutamani tu au kupenda. Ni vitu vinavyopatikana endapo nchi na uongozi wake unasimamia kikamilifu uapatikanaji haki, ukweli, uhuru na usawa kwa kila mtu kwenye nchi husika. Kinyume cha hayo, sioni ni kwa njia gani nchi inaweza kuepuka mihemuko, shinikizo na vurugu za mara kwa mara.
Je, makundi yote katika jamii iwe wazee, wanawake, vijana, watoto kwa watu wazima, walemavu kwa waliokamili, wajane, wanamji kwa wanavijiji, hivi wanaridhika na hali ilivyo na je, wanaona kuna usawa na haki inatendekea kati yao?
Nina hakika kwamba hatuwezi kujenga umoja na amani ya kweli kwa shuruti na amri. Inatupasa wote turudi chini na kutambua hofu, tashwishi, matamanio na maslahi ya kila mmoja wetu, kisha tupeane fursa ya kubadilishana fikra na mawazo kuhusu ni kwa namna gani kwamba mwisho wa siku hakuna miongoni mwetua atakayekuwa mshindwa bali wote tutaibuka kama washindi.
Masuala mbalimbali yanayolikabili taifa sasa ikiwa yatakuwa yakitulizwa kwa amri, vitisho na virungu vya askari, siamini hata kidogo kama vitasaidia kuuzima moto huo unaolipuka mara kwa mara na ukuzimika moja kwa moja.
Kitakachofanyika ni kuufukia moto huo chini kwa chini kama takataka zinavyofanywa kwenye madampo. Ole wenu, siku ukija kulipuka wakati kuna upepo na malori yote ya zimamoto hayana magurudumu wala maji ya kuzimia moto huo !!!
Pepe: [email protected]