Maprofesa bungeni wanapolalamikia uhaba wa wahadhiri

Muktasari:

Kwa sasa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lina wabunge ambao ni maprofesa wasiopungua wanane. Hawa nao walipaswa kuwa vyuoni wakifundisha.

Bunge tayari limepitisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  na kuidhinisha jumla ya Sh1.97 trilioni kutekeleza miradi mbalimbali ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025.

Akiwasilisha makadirio ya bajeti hiyo jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema, vipaumbele kwa mwaka huu wa fedha ni: kuendelea na utekelezaji wa sera na mitalaa, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini.

Vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (amali na amali sanifu), kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu.

Vipaumbele vingine ni pamoja na kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu; na kuendeleza utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu, huku Serikali ikinuia kuendelea na utekelezaji wa sera na mitalaa, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini.

Wakati tunashangilia bajeti iliyotuna, suala la uhaba wa wahadhiri wa vyuo vikuu limekuwa kuwa mwiba katika tafakuri juu ya ubora wa elimu vyuoni.

La kushangaza ni pale baadhi ya wahadhiri waliokuwa wakilalamikia uhaba wa wataalamu bungeni,  ndio waliokwepa kazi hiyo na kuhamia ‘mjengoni’ kufuatia maziwa na asali.

 Kwa mujibu wa Mbunge wa Muleba Kusini, Dr. Oscar Ishengoma, Chuo Kikuu cha Dar es salaam kina maprofesa 93 badala ya wanaostahili 161.

Takwimu  hizi zimeakisi matokeo ya utafiti wa mwaka 2017 uliofanywa na Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu Tanzania (THTU), ukibainisha kuwa asilimia 53 ya wafanyakazi wa ngazi za juu na zaidi katika vyuo vikuu walikuwa wakifanya kazi kwa mikataba kutokana na kustaafu.

Kufuatia wingi wa wanafunzi vyuoni ambapo kwa kila mwaka takribani wanafunzi 100,000 huhitimu masomo ya elimu ya juu kila mwaka, tuna kila sababu ya kuamini kuwa, kwa uhaba huu wa wahadhiri, wanafunzi hawa wanahitimu  pasipo na ujuzi wa wa kukidhi vigezo kwenye soko la ajira. Tujiulize je, wanaweza kushindana kwenye soko la ajira na wenzao kutoka nchi jirani, ambapo huenda tatizo la maprofesa si kubwa kiasi hicho?

Je, kuna mipango endelevu ya kuongeza wahadhiri bila kuathiri ari ya wengi wao kukimbilia fursa zenye maslahi zaidi ya kufundisha?

Majibu ya maswali yangu haya ni rahisi kwa sababu kila mara waajiri wamesikika wakilaumu ujuzi na maarifa ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini kuwa ni wa kutiliwa shaka.

Tumefika hapa kwa sababu ya kukimbilia takwimu za wingi wa wanafunzi vyuoni pasipo mipango madhubuti ya kuhakikisha miundombinu inawiana na idadi ya wanafunzi pamoja na wahadhiri.

Akizungumza katika moja ya hotuba zake jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani, Rais Samia Suluhu Hassan alionesha kukerwa na hali ya wahitimu kutoonesha weledi kwenye mazingira ya kazi.

Wahadhiri ni wachache kiasi kwamba mwanafunzi aliyetoka na ufaulu wa juu kidato cha sita anashindwa kuonesha weledi anaoutaka Rais, kwani baadhi ya talanta zake hufifishwa na hali ya ufundishaji chuoni.

Ajabu ya maprofesa vyuoni

Jambo la kukera zaidi ni kwamba maprofesa wengi waliolalama juu ya uhaba wa wahadhiri, ni wabunge ambao pengine wangepaswa kuwa katika taasisi hizo ili kuongeza nguvu kazi.

 Inashangaza kwamba wataalamu hawa wako kwenye siasa, wanafurahia neema ya nchi kwa sababu siasa kwa nchi zinazoendelea inalipa zaidi kuliko kazi ya ualimu.

Hivi karibuni nimekuwa na mjadala na mhadhiri mwandamizi katika chuo kikuu kimoja,  nchini ambaye alisema wanazuoni wamekuwa na vikao mfululizo wakibungua bongo namna ya  kufumua mitalaa kwa kila idara ili iendane na mabadiliko yaliyofanywa kufuatia ongezeko la tahasusi 49 katika ngazi ya sekondari.

Alilalamika namna ambavyo vikao hivyo vinavyowapotezea muda mwingi pasipo posho wala motisha ya kujikimu.

“Tuna wakati mgumu. Unajua mhadhiri mwandamizi wa hadhi yangu anapaswa alipwe na apewe stahiki sawa na katibu mkuu wa wizara fulani, lakini kinyume chake ni kama hivi, hata hela ya mawasiliano ni shida, tunajigharamia wenyewe. Kwa hali hii lazima kila mmoja aone umuhimu wa kutafuta mianya inayolipa zaidi hasa kukimbilia kwenye siasa,” alisema mhadhiri huyo.

Malalamiko haya ndio chanzo cha uhaba wa maprofesa nchini. Wengi wameamua kukimbilia nga’mbo kutafuta ahueni ya maisha kwani bado nchi zetu zinazoendelea hazijaweza kuthamini mchango wa wataalamu  hawa.

 Wahadhiri wa vyuo vikuu wanastahili kupewa  motisha stahiki zaidi ya mshahara ambao ni mdogo pia kulingana na mlolongo wanaoupitia katika kukidhi hadhi walizonazo.

Kwa mfano, inachukua takribani miaka tisa kwa mhadhiri msaidizi kukidhi vigezo vya kuwa mhadhiri mwandamizi ili aweze kuwa profesa mshiriki.

Mtaalamu huyu anapaswa pia kuchapisha machapisho yasiyopungua 14 na katika jitihada za kukidhi hivi vigezo,   bado hapewi malipo kwa kazi hizo.

Niliambiwa machapisho wanaoyotoa wahadhiri kwenye majarida ya kimataifa hayalipiwi; ni bure na pengine mchapishaji hulazimika kulipia gharama za uchapishaji pasipo msaada wa chuo husika.

Katika mazingira haya, mhadhiri anyehangaika hivi ikitokea akanusa fursa kwenye shirika kubwa linaloweza kufahamu umuhimu wa talanta yake, hakika lazima akimbie kazi yake.

Tumefika hapa tulipo kwa sababu ya kuthamini siasa kuliko mambo mengine muhimu. Wahadhiri kwenye nchi zilizoendelea hawakimbilii kwenye siasa. Muda mwingi wanakuwa makini kutetea taaluma zao kwa machapisho makubwa, wanafanya tafiti, wanabuni nadharia kwa sababu wanapewa haki stahiki.

Profesa Ladislaus Semali wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania nchini Marekani, alinieleza  chuoni  hapo hakuna mhadhiri anayehangaika na biashara ya baa au kuhangaikia kazi za rejareja.

Ni kwa sababu  hawezi kuupata muda wa kufanya hayo, huku akisisitiza kuwa wahadhiri wa hadhi yake wanalipwa stahiki zao bila tashwishi kiasi cha kuwafanya wajenge upendo wa ndani (intrinsic passion) na taaluma zao.