Mauaji ya Israel huko Gaza yameunganisha Wapalestina

Muktasari:

HATIMAE Israel imekubali kusaini mkataba wa kuacha kuishambulia Gaza baada ya siku nane za mauaji ya wananchi wa ukanda huo wa Palestina. Hii ni baada ya Misri kuwakutanisha Israel na wapiganaji wa Hamas na Islamic Jihad.HATIMAE Israel imekubali kusaini mkataba wa kuacha kuishambulia Gaza baada ya siku nane za mauaji ya wananchi wa ukanda huo wa Palestina. Hii ni baada ya Misri kuwakutanisha Israel na wapiganaji wa Hamas na Islamic Jihad.


Katika mashambulizi hayo wakazi takriban 172 wa Gaza waliuawa, wakiwemo watoto 42, wanawake 11, vikongwe 18 na wanahabari watatu.
Kitoto cha miezi kumi kilikufa. Kingine ni cha miezi 11 pia. Mwanamke mwenye mimba ya mapacha naye aliuawa. Watoto wawili wa shule waliokuwa wakicheza mpira waliuawa. Familia ya Al-Dalou yenye watu 14 ilimalizwa, ikiwa na wanawake wanne na watoto sita.


Madege ya F-16 ya Israel yaliteketeza nyumba, shule, misikiti, ofisi za wanahabari na hata uwanja wa michezo. Alimradi Gaza imechakazwa kwa mabomu. Zaidi ya Wapalestina 11,000 walilazimika kujificha katika majengo ya Umoja wa Mataifa ili kuepuka makombora ya Israel.


Baada ya Israel kukubali kuacha mashambulizi, chama tawala cha Hamas huko Gaza kilitangaza sikukuu. Maelfu ya wananchi wa Gaza walimiminika mitaani wakisheherekea ushindi huku wakipeperusha bendera za Hamas, Islamic Jihad na Fatah. Viongozi wa vyama hivyo walipanda jukwaa moja na kuhutubia umati, kitu ambacho hakijawahi kutokea
Waandamanaji waliwapongeza wapiganaji wa Hamas na Islamic Jihad kwa ushindi. Ni ushindi wa Daudi aliyemkabili Goliathi. Israel ni nchi ya tano ulimwengu kwa nguvu za kijeshi na silaha za kisasa, pamoja na atomiki. Lakini vijiroketi vya Wapalestina viliwakosesha usingizi.
Kwa mara ya kwanza roketi hizo zilifanikiwa kufika hadi Tel Aviv na Jerusalem, kitu ambacho hakijafanyika tangu mwaka 1991 wakati wa vita vya Guba ya Uajemi.


Israel kwa upande wake ilitumia ndege za kivita F-16 pamoja na vifaru na manowari za kijeshi. Waliamua kufuta likizo zote za wanajeshi na wakawaita wanajeshi 30,000 wa akiba. Hata hivyo, wapiganaji wa Palestina hawakusalimu amri.


Huu ndio ushindi uliosheherekewa huko Gaza. Muuza mboga mmoja alisema “Huu ni ushindi wa wananchi wote wa Gaza bila ya kujali itikadi.”
Ni vizuri kuelewa mashambulizi haya yalianzaje na chanzo chake ni nini. Vyombo vya habari vya magharibu vimekuwa vikizungumzia haja ya Israel kujilinda kutokana na maroketi ya Hamas. Israel inazungumzwa kana kwamba ni nchi inayoshambuliwa na maroketi kutoka Gaza.


Ukweli ni kuwa kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu hadi Novemba 6, 2012, Wapalestina 71 waliuawa na 291 kujeruhiwa huko Gaza kutokana na mabomu ya Israel. Wakati huo hakuna raia hata mmoja wa Israel aliyekufa kutokana na maroketi ya Gaza.
Katika hali kama hii, Novemba 4, mwaka huu majeshi ya Israel yalimuua raia Gaza aliyekuwa mgonjwa wa akili.Siku nne baadaye walimuua mtoto wa miaka 13 aliyekuwa akicheza mpira.  


Baya zaidi, tarehe 14 Novemba Israel ilitumia ndege ya kivita kumuua Ahmed Jabari aliyekuwa kamanda wa Hamas.


Ni muhimu kujua kuwa wakati huo Jabari alikuwa akiratibu mkataba wa amani ya kudumu baina ya Hamas na Israel. Kulikuwepo na mazungumzo baina ya Israel na Hamas kuhusu makubaliano hayo, na Jabari alikuwa katika gari akielekea kwa wenzake wa Hamas ili nao wasaini, ndipo bomu la Israel lilipommaliza yeye na msaidizi wake.
Israel walijua fika uratibu huu wa Jabari. Kwani mkataba huo uliwahi kuzungumzwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyau na mawaziri wake tisa walipokutana Novemba 5, mwaka huu. Badala ya kusubiri kusainiwa kwa waraka huo Israel iliamua kumuua mratibu wake Jabari. Matokeo yake ni haya mapigano ya siku nane.


Ni sawa na mashambulizi ya Disemba 2008 wakati Wapalestina 1,400 waliuawa na Israel. Nusu yao walikuwa raia wa kawaida. Kwa upande wa pili Israel ilipoteza wanajeshi 10 na raia watatu. Halafu tunaambiwa eti Israel inajikinga.


Rais Obama anadai eti Israel ina haki ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Wapalestina. Wanataka tusahau kuwa ni Israel ndio iliyovamia na kukalia kijeshi ardhi ya Wapalestina, huku ikiwaua na kuwatesa kila kukicha.  
Ni vizuri kujua sababu ya Israel kuanzisha mashambulizi na mauaji ya Gaza ya hivi majuzi. Netanyau anakabiliwa na uchaguzi tarehe 22 Januari 2013. Hii ni sehemu ya kampeni.


Anataka aonekane kuwa ni mbabe “anayelinda” Israel, badala ya raia wake kuzungumzia matatizo ya kimsingi yanayowakabili kama vile ufisadi wa vigogo na umaskini unaozidi kuongezeka. Kwa maneno mengine, Netanyau anabuni “adui” wa nje ili watu wasahau kuzungumzia migogoro ya ndani.  
Inaonekana mbinu hii ilifanikiwa, ndipo mara tu baada ya Netanyau kuanza kuishambulia Gaza wapinzani wake walisimamisha kampeni dhidi yake, na wakamuunga mkono.


Hata hivyo, ni ndoto kufikiria wananchi milioni 1.7 wa Gaza watakubali kuishi katika hali duni huku wakizingirwa na majeshi ya Israel, wakinyimwa uhuru wa kutembea, uhuru wa kufanya kazi, hata uhuru wa kupokea misaada kutoka nje. Hili ni gereza kubwa duniani.


Suluhisho pekee ni kwa Israel kujitoa kutoka maeneo ya Palestina iliyoyavamia na kuwapa Wapalestina uhuru wao wa kujitawala. Sheria ya kimataifa, uamuzi wa mahakama ya kimataifa na maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yanaitaka Israel ifanye hivyo.
0713-562181