Mitandao ya kijamii fursa ya kushinda umaskini
Muktasari:
- Matumizi ya mitandao kama Facebook, Twitter, WhatsApp, Youtube, Instagram na Telegram hivi sasa ndio njia rahisi kabisa ya kusambaza ujumbe na kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi.
Nguvu ya mitandao ya kijamii inaongezeka kwa kasi katika kupashana habari nchini na duniani kote.
Matumizi ya mitandao kama Facebook, Twitter, WhatsApp, Youtube, Instagram na Telegram hivi sasa ndio njia rahisi kabisa ya kusambaza ujumbe na kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi.
Profesa Jose Van Dijick’s, mtafiti bingwa wa masuala ya habari na mitandao ya kijamii anasema matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii duniani yamewaunganisha mamilioni ya watu kufanya biashara, kujenga urafiki na hata kushiriki pamoja katika masuala ya kisiasa na kijamii.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya DreamGrow inayojihusisha masuala ya mitandao ya kijamii na masoko nchini, Estonia, matumizi ya mitandao ya kijamii yanaongezeka kwa kasi kubwa duniani na ni fursa kubwa ya kufanya biashara.
Dream Grow katika utafiti huo wa Agosti, 2018, inaeleza kuwa ongezeko hilo la watumiaji kila mwaka mbali na biashara, pia linasaidia katika shughuli nyingine za kuwaunganisha watu.
Taasisi hiyo inabainisha kuwa hadi sasa Facebook imewaunganisha watu bilioni 2.2, YouTube watu bilioni 1.9 Instagram bilioni moja na Twitter watu milioni 336.
Kinachohitajika katika mitandao hii ili kuunganisha na mamilioni ya watu ni kuwa na intaneti na kifaa cha mawasiliano iwe simu za kisasa (smart phone) au kompyuta ama tablet.
Mitandao ya kijamii mefanikiwa kuunganisha makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo vijana, wazee, wakulima, wafanyabiashara na wafanyakazi.
Ingawa kuna faida na hasara katika ongezeko hilo la watumiaji wa mitandao ya kijamii, itoshe kueleza kuwa kuna faida nyingi zaidi kama ukitumia vizuri kuliko hasara.
Kasi ya matumizi ya mitandao hii haipo mijini tu, bali hata vijijini kuna matumizi makubwa kwani hivi sasa hakuna jambo kubwa ambalo litatokea mjini na vijijini wasijue.
Ni ukweli ulio wazi kuwa nguvu ya mitandao hii sasa ni zaidi ya runinga, redio na magazeti.
Hapa nchini watumiaji wengi wa mitandao wanaitumia kupashana habari tu na hili limedhihirika katika matukio mengi kama lile la kutekwa na kupatikana mfanyabiashara Mohammed Dewji ambapo tumeona nguvu ya mitandao ya kijamii. Hivyo ni wazi kuwa bado mitandao ya kijamii haijatumika ipasavyo kama chombo cha biashara na kukuza maarifa hapa nchini na kuleta faida kubwa kwa watu.
Mitandao ya kijamii nchini inapaswa kuwa fursa nzuri ya kufanya biashara za aina mbalimbali na kujipatia kipato.
Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya mpaka Desemba 2017 inaonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka kufikia watu milioni 23 ambayo ni sawa na asilimia 45 ya Watanzania wote.
Kutokana na ripoti hiyo tunapata kufahamu kuwa ingawa watumiaji wa mitandao ya kijamii kama Instagram na Facebook hawajafikia milioni 10, lakini kuna fursa ya kuongezeka kwa kuwa idadi ya watumiaji wa simu za mkononi imefikia milioni 40 kutoka milioni 27.62 mwaka 2012.
Hivyo takwimu hizi ni fursa kwa mamalishe kutumia mitandao kuuza chakula popote wapendapo, wafanyabiashara wa bidhaa ndogondogo kutafuta wateja, wauzaji wa magari, wamiliki wa shule za binafsi na wengine wengi wana fursa ya kunufaika na mitandao.
Kikubwa ambacho unapaswa kufanya ni kueleza tu kupitia mtandao unaotumia unafanya nini, upo wapi na unawezaje kufikisha huduma yako kwa anayeihitaji.
Naamini kama wajasiriamali wengi watatambua fursa hii wataweza kupunguza gharama za biashara zao kama kukodi ofisi kubwa na kulipa kodi kubwa. Tayari kuna baadhi ya wajasiriamali hasa vijana wa mijini wameanza kuchangamkia fursa hii ya mitandao ya kijamii licha ya kuitumia kutuma picha zao na kusaka kwa marafiki, pia wanatumia kurasa zao kutangaza biashara.
Lakini pia hata Serikali badala ya kuona tu mitandao ya kijamii ni adui hasa pale inapotumika kusambaza habari zisizo sahihi inapaswa kutambua ni chanzo mojawapo cha kukusanya kodi.
Kila mtu anatakiwa kutambua kuwa mitandao ya kijamii ni fursa nyingine ya kujikwamua na umaskini na kukuza uchumi licha ya kunufaika na habari lukuki. Hivyo, ni muhimu kutambua kuwa mitandano si tu sehemu ya kutumiana salamu, kujipiga picha na kubandika (selfie) na kutumiana majungu, bali ni sehemu ya kupambana na umaskini na kujiletea maendeleo.
Mussa Juma ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi mkoa Arusha.Mawasiliano - 0754296503.