Miundombinu ya umeme iboreshwe
Serikali ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuna upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wake wote, mijini na vijijini. Mwaka hadi mwaka, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imewekeza katika miradi mikubwa ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme, huku ikilenga kuimarisha uchumi wa viwanda na kuinua maisha ya wananchi. Moja ya mafanikio makubwa katika sekta hii ni kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere (Julius Nyerere Hydropower Project – JNHPP), ambao umefungua ukurasa mpya katika historia ya uzalishaji wa nishati ya umeme nchini.
Bwawa la Nyerere, linalojengwa katika Mto Rufiji, linazalisha megawati 2,115 za umeme, kiasi kikubwa kinachotarajiwa kuongeza zaidi ya mara mbili ya uwezo wa sasa wa kitaifa wa uzalishaji wa umeme. Kukamilika kwa mradi huu ni hatua kubwa katika kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa umeme kwa matumizi ya nyumbani, viwandani, katika taasisi na kwenye shughuli za kijamii kama shule, hospitali na vituo vya afya. Pia ni ishara ya kujitegemea kwa taifa katika sekta ya nishati, bila kutegemea umeme wa mafuta au nishati kutoka nje.
Pamoja na uzalishaji mkubwa wa umeme, serikali pia imejikita katika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme. Maboresho hayo yanahusisha ujenzi wa njia mpya za kusafirisha umeme wa msongo mkubwa (high voltage transmission lines), vituo vya kupoza umeme, na upanuzi wa gridi ya taifa ili kuunganisha maeneo mengi zaidi hususan ya vijijini. Kupitia mpango wa REA (Rural Energy Agency), maelfu ya vijiji tayari yameunganishwa na umeme, na juhudi zinaendelea kufikisha huduma hiyo kwa vijiji vilivyobaki.
Lengo la juhudi hizi zote ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata umeme wa uhakika, usiokatika ovyo, na kwa gharama nafuu. Umeme wa uhakika unachochea maendeleo ya kiuchumi, huwezesha shughuli za uzalishaji viwandani, kilimo cha kisasa (kama vile umwagiliaji), biashara ndogondogo, pamoja na kuwa chanzo muhimu kwa elimu na afya.
Kwa muktadha huo, ni dhahiri kuwa huu ni wakati mwafaka kwa bei ya umeme kupungua. Kwanza, uzalishaji mkubwa unaotokana na Bwawa la Nyerere utapunguza gharama za kutegemea umeme wa mafuta ambao ni ghali. Pili, kuunganishwa kwa maeneo mengi zaidi kwenye gridi ya taifa kunamaanisha kuwa mzigo wa gharama ya uzalishaji unasambazwa kwa watumiaji wengi, hivyo kupunguza kiwango cha tozo kwa kila mtumiaji mmoja.
Kupungua kwa bei ya umeme kutakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi, hasa wa kipato cha chini, na pia ni motisha kwa wawekezaji wa viwanda, hasa katika maeneo ya pembezoni. Ni matarajio ya wengi kuwa serikali itatumia fursa ya uwekezaji mkubwa uliokwisha kufanyika, pamoja na ongezeko la uzalishaji wa nishati, kupunguza gharama ya umeme kwa wananchi wake.
Upatikanaji wa umeme wa uhakika kupitia kukamilika kwa Bwawa la Nyerere, na kuwapo vituo vya Kinyerezi I na II pamoja na mikakati ya kuongeza Kituo cha Kinyerezi III ni hatua thabiti ya kuelekea Tanzania ya viwanda. Hatua hii isiishie tu katika kuzalisha na kusambaza umeme, bali iende sambamba na sera za kupunguza bei ili kuleta manufaa ya kweli kwa wananchi. Huu ni wakati sahihi kwa serikali kuchukua hatua hiyo muhimu kwa ajili ya maendeleo endelevu.