Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mume si fedha, elimu, wala madaraka yake

Hivi karibuni kumezuka matapeli hata wadhalilishaji, tena wengine wasomi, wajiitao wataalamu wa ndoa na saikolojia ya mwanamke wanaipotosha jamii hata kuiibia kwa kisingizio cha kutoa ushauri juu ya ndoa.

Watu hawa, kwa kujua na kudandia mfumo dume, wawe wanaume hata wanawake, waganganjaa, waganga wa kienyeji, na viongozi wengi wa dini wa kujipachika wamejigeuza wataalamu wa saikolojia ya ndoa na wanawake. Wanatoa ushauri ambao hauingii akilini, vinginevyo mwenye kuuchukua na kuuamini ima awe ni mjinga hata mpumbavu wa kutupwa, kuzidiwa, kutapatapa au kukata tamaa.

 Hivi karibuni tulitumiwa clip ya mshauri anayetambulishwa kama daktari wa saikolojia. Jamaa huyu anaongea bila aibu tena kwa mjumlisho na kujiamini.

Anadai eti wanawake ni kama watoto au ni watoto kwenye masuala ya kutafuta fedha. Anadai kuwa kila mwanamke anaamini kuwa kila mwanamume ni gwiji wa kusaka pesa. Hivyo, wanaume wasilalamike wanapokuwa hawana fedha. Je, hii ni kweli? Sisi kama wanandoa ambao tumedumu kwenye ndoa kwa miaka 27 tumestushwa na ushauri huu wa ajabu na hovyo. Kwa kutumia ujuzi na uzoefu wetu, tumeona hii ni kashfa, matusi, ujinga, udhalilishaji wa kijinsia, kuganga njaa na shaka juu ya taaluma na ushauri vya wahusika.

Kwanza, haiwezekani wanawake wote, kama binadamu yeyote, wakawa na tabia sawa katika jambo moja, yaani uwezo wa mwanamume kutafuta fedha. Hata wanyama hawana tabia moja inayofanana kwa wote kwenye jambo moja. Hata mbuzi hawafanani kitabia. Mmoja anaweza kupenda kushambulia mashamba na kula mazao.

Mwingine anaweza asipende kushambulia mashamba kwa vile alishaumizwa alipofanya hivyo nakadhalika.

Kimsingi, uwezo wa mtu wa kutafuta au kutotafuta fedha unategemea mambo mengi, kama vile mipango, motisha, uzoefu, malengo, makuzi, ndoto, aina ya jamii anamotoka, muda, mazingira, aina ya shughuli anayofanya kumuingizia fedha nakadhalika Pili, ni imani potofu kufikiri kuwa kila mwanamke, ima ni tegemezi au anaolewa kufuata fedha na si kutekeleza malengo na mipango yake kama binadamu.

Hivyo, licha ya kuwa udhalilishaji na uongo, ni ujinga na upofu kudhani kila mwanamke anaingia kwenye ndoa kutafuta au kufuata fedha. Ingekuwa hivyo, wanaume maskini wasingeoa. Haimaanishi kuwa hakuna watafuta fedha katika ndoa, hasa wanaosukumwa ama na tamaa binafsi au baadhi ya mila za kinyonyaji kama vile kutaka mume awe buzi la kumtunza mhusika na watu wake. Hii siyo kwa wote.

Tatu, ni imani potofu na kutowajua wanawake kama binadamu wa kawaida wenye uwezo sawa na wanaume kudhani kuwa ni tegemezi kwa wanaume, hivyo, wanafikiri kuwa kila mwanamume ni mashine ya kutapika fedha kama ATM ambayo haiishiwi fedha.

Nne, kuna wanawake matajiri ama wa kutafuta au kurithi wanaojua kuitafuta, kuitunza na kuitumia kuliko wanaume ambavyo pia wapo wanaume wa namna hii. Unapodai eti wanawake wote wanaamini wanaume ni ATMs, unajikumbusha kuwa wapo matajiri, wasomi, wenye madaraka tena makubwa kuliko waume zao? Hawa nao si wanawake?

Tano, ni wanaume wangapi waliooa wanawake matajiri? Je, hili nalo watalisemeaje hawa wataalamu wetu wenye kutia shaka? Huwezi kuhubiri maji ukanywa mvinyo. Kwa ufupi, katika ndoa, mume au mke si elimu, fedha au madaraka, bali ni mume au mke basi. Mengine, ni makandokando tu.

Pamoja na utaalamu, usomi na mengine kama hayo, wengi tunashauri kutokana na maisha yetu yaliyojengwa katika misingi fulani. Hivyo, usishangae mshauri unayemuamini au kumtegemea sana, akashauri kitu kisichokuingia akilini.

Hivyo, tunasema asemacho kinaweza kuakisi maisha yake binafsi ambayo pia yanaweza kuhitaji ushauri, japo yeye ni mshauri.

Binadamu hawezi kukimbia maisha na tabia zake. Kinyonga hata abadili rangi zake vipi, bado ni kinyonga. Kama umesomea ushauri na maisha yako hayafanani na unachoshauri au unashauri utopolo, jua kuna tatizo. Faida za kitu chochote lazima zianze nawe.