Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwaka 2025 uwe wa kulisuka upya Jeshi la Polisi

Leo tunaanza safari ya siku 365 za mwaka 2025, natamani tujiwekee malengo kama taifa kuwa uwe mwaka wa kulisuka upya jeshi letu la polisi kuanzia utendaji, weledi na maslahi ili kulirudisha kuwa jeshi linaloaminiwa na raia.

Tunatamani kuona ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka mifumo ya Tehama kusomana kati ya kituo kimoja hadi kingine na kutoka kituo kimoja hadi taasisi nyingine za Haki Jinai kama Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Tukirejea hotuba yake aliyoitoa Januari 31, 2023 jijini Dodoma, alitaka mifumo isomane kwamba mtu akikamatwa na Jeshi la Polisi kisha akatoa maelezo yake kwa hiari, basi DPP naye ayaone maelezo hayo moja kwa moja ofisini kwake.

Lakini natamani katika kusomana huko kwa mifumo, Jeshi la Polisi liwe na mfumo unaowezesha jalada la shauri (RB) linapofunguliwa kituo A jijini Dar es Salaam, basi taarifa hiyo iweze kuonwa na Polisi walioko kituo B Songea.

Hii itasaidia kuondoa sintofahamu pale mshukiwa wa uhalifu anapokamatwa na Polisi na ndugu wanatafuta kituo kimoja baada ya kingine bila mafanikio, kwani watakapofika kituoni, polisi anagusa tu kompyuta inamwambia yuko kituo C.

Ukweli una sifa moja kuu kwamba hata ukiuchukia au kuukataa, haugeuki kuwa uongo na siku zote ukweli huwa mchungu na unauma, kwa miongo kadhaa jeshi letu limeyumba na kutoka katika misingi ya kulinda raia na mali zao.

Msema kweli ni mpenzi wa Mungu, huko nyuma polisi wetu wakitokea wameua mtu au watu, kulikuwa na justification (uhalali) kuwa walikuwa ni wahalifu kweli na umma unakiri hivyo na wananchi walikuwa wanalipongeza.

Lakini tunamaliza 2024, nchi ikiwa imevimba, kwani wapo Watanzania wenzetu hadi leo hatujui wako wapi na kama wako hai ama la.

Tatizo limekuwa kubwa zaidi Serikali ilipoanza kutumia vikosi kazi, hasa kuanzia utawala wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, na hapo ndipo imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi ilipoanza kuporoka kwa kasi ya ajabu.

Baadhi ya vikosi kazi ambavyo vinajumuisha vyombo vya dola kutoka taasisi nyingine, vinakuwa havina mpango kazi, malengo wala uongozi wa ni taasisi gani ni lead agency (kiongozi) katika operesheni wanazoenda kufanya.

Kuna wakati havijui wala kuheshimu mamlaka (jurisdiction) kwamba mtu anakamatwa eneo A ambalo kuna kituo cha Polisi jirani kinachojulikana kama X, lakini hapelekwi katika kituo hicho na anaenda kufichwa kusikojulikana.

Ukamataji wao hauzingatii Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) RE 2022, na badala yake wanakuwa hawana sare, hawajitambulishi na ukamataji wao hautofautiani na ule unaofanywa na magenge ya kihalifu yanayoteka watu.

Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais 2023 ilibaini uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka ya kukamata na hii inawawia vigumu wananchi kutambua taasisi iliyomkamata ndugu yao na mahali alipohifadhiwa ili wampe msaada.

Pia, ilibaini uwepo wa vyombo vingi vya ukamataji na vyenye mahabusu, ulitafsiriwa na jamii kuwa ni sababu mojawapo ya watu waliokamatwa kupotea wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola na hadi leo hawajulikani walipo.

Leo hii kwa namna taharuki ilivyo kwa wananchi kwa kushindwa kutofautisha ukamataji halali wa polisi na utekaji raia, iko siku na siombei hili litokee, polisi wetu wema kabisa wanaweza kuumizwa hata kuuawa na raia.

Ukisoma ripoti ya Tume hiyo, nayo ilibaini ukweli kuwa taswira ya Jeshi la Polisi nchini kwa wananchi sio nzuri kutokana na vitendo vinavyochafua taswira ya jeshi hilo, ikiwamo ukiukwaji wa haki za binadamu, hususan utesaji washukiwa.

Tume ilipendekeza Jeshi la Polisi lifanyiwe maboresho makubwa kwa kuliunda na kulisuka upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo na libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra ili iwe ni taasisi ya kutoa huduma na si mabavu.

Sasa mwaka 2025 tukubaliane kama taifa kuwa tulirudishe jeshi letu kwenye mstari, watu wakamatwe kwa mujibu wa sheria, wawekwe mahabusu kwa mujibu wa sheria na kwa makosa madogo, mshukiwa aitwe kwa wito wa polisi.

Kama nilivyotangulia kusema taswira njema ya jeshi letu imechafuka na ukiacha matumizi ya nguvu na ya vikosi kazi, lakini Polisi kutumika kisiasa nako kunalichafua jeshi letu hadi wadau wanalifananisha na CCM B au refa mchezaji.

Kwa hiyo mwaka 2025 tulifanyie mapinduzi ya kiutendaji kuanzia weledi, ujuzi, makazi bora na vitendea kazi na tuliondoe katika kikokotoo cha mafao.

Mjema ni mtaalamu mshauri (media consultant) wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).