NIKWAMBIE MAMA: Ukicheka na nyani watakuachia mabua

Kwanza nikupe hongera kwa kujitoa kimasomaso kutupigania Watanzania kama kuku anavyofanya kwa vifaranga wake. Unanikumbusha kuku tuliyekuwa naye wakati nasoma shule ya msingi.

Alitaga mayai kumi na mawili na akayatotoa yote, tukawa na familia bora ya kuku wenye afya kumi na wanne. Siri ya mama ilikuwa ni kuruka na kunguru hewani pale kunguru alipomnyakua kifaranga wake.

Nisiwe mnafiki, ni lazima upewe maua yako kungali mapema kwani kazi inaonekana. Ingawaje sitasema yote hapa, lakini majambo ambayo watoto wa mjini wanasema “umeua”, ni pamoja na kurudisha msisimko kwenye kilimo na michezo.

Mambo haya mawili yanasifiwa duniani kwa kuingiza pato kubwa kwenye mataifa mbalimbali. Tena hapa kwetu kilimo tulikichukulia kuwa uti wa mgongo wa uhai wa Taifa.

Lakini pamoja na heshima yake, kilimo kilitupwa mkono. Katika wakati huu wa teknolojia, wakulima walichukuliwa kuwa ni waliopitwa na wakati na wasio na elimu ya kisasa. Lakini jitihada zako za kukirudishia hadhi yake zinaonyesha mafanikio.

Nikitaja kwa uchache; uhamasishaji mkubwa umefanyika katika Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika, uzinduzi wa mashamba makubwa ya pamoja kule Dodoma, ufunguzi wa maonyesho ya kilimo kule Qatar na kadhalika.

Kitendo cha kukabidhi hundi ya Sh200 milioni kwa vijana wanaofanya kazi za kilimo kumetupa hamasa kubwa. Umeondoa ile dhana ya kilimo kupitwa na wakati, kwani ulikabidhi vifaa vya kisasa kama “ndege nyuki” (drones) maalumu kwa ajili ya kilimo kwa vijana wetu.

Licha ya kuwa na uhakika wa kupata chakula cha kututosha na cha biashara, lakini pia tutaboresha mazingira yetu kwa ukijani na kupunguza tishio la mabadiliko ya hali ya nchi linaloutikisa ulimwengu kwa sasa.

Lakini kama kawaida, kwenye msafara wa mamba, kenge hawakosekani. Wazee wa “cha juu” hawakosi kutia mikono kwenye suala hilo, hasa baada ya kugundua kwamba vijana wanapata fursa ya kujiendeleza bila kupitia kwao.

Hawa ni watu wa “ganji-kuona”, kwenye kila wanachokiona hata kama hakiwahusu ni lazima wagawiwe. Kwa kuwa inaeleweka kuwa wataalamu ni watu wa lazima kwenye matumizi ya zana za kisasa, basi matapeli hao watajikita hapo.

Mpango wao katika suala hili hautatofautiana na uharibifu unaofanywa kwenye michezo. Tumeshuhudia miaka nenda rudi tukiyumba kimataifa. Inaeleweka kwamba unapotaka kupambana na adui inakupasa ujue mbinu zake kwanza.

Huwezi kuingia kwenye mapambano na bingwa wa kutupa magruneti ukiwa unatumia mishale. Sio siri kwamba kwenye viwanja vya michezo, watu wanaojua siri za mabingwa ni makocha.

Iwe mpira, ndondi au riadha, kocha atajifunza kwa bidii mbinu za mabingwa ili akazitoboe kwa adui zao atakaoingia nao mkataba. Sisi tunapoenda kupambana kimataifa, tunakubaliana kwa kauli moja kumlipa kocha huyo kwa lengo la kupanda kimataifa.

Tukifika huko tutalitangaza Taifa letu ili kuvuta wawekezaji na watalii, na hata kuuza bidhaa zetu na kuleta tija kwa Taifa letu.

Kwa bahati mbaya wazee wale wa “cha juu” wanainusa hiyo fursa na kuingia kwenye mzunguko. Watafungua kurasa za mitandao kukariri gharama za makocha walio bora. Lakini kwa kuwa wahuni wametapakaa duniani kote, wazee wetu kwa kutumia kodi za wananchi watakwea mapipa.

Lakini wakifika huko wataingia kwa matapeli wenzao; yaani kama vile umemtuma mtu mjini akakununulie suti mpya ya harusi, yeye akaenda kuvunjiwa bei mtumbani.

Wataongozwa na madalali wa huko na kupelekea kupata mtaalamu feki. Hata kule wapo wa kuungaunga ambao hawasiti kusaini hundi ya sifuri saba na kupokea nusu yake.

Wakimleta hapa wataanza kuughani wasifu wake uliotukuka, lakini Watanzania watakapolalamikia kazi mbovu ya mtaalamu huyo, ndipo nao watakapokuja juu na kumtimua. Hapa ni lazima utajiuliza kocha wa kimataifa mwenye mkataba anafukuzwaje kama panya na akakubali.

Sijui ilikuwa ni manogesho ya baraza la kahawa au vipi, lakini siku moja nilitokwa na machozi baada ya shabiki mmoja kutoa simulizi ya bondia aliyefungiwa baada ya kupata ushindi. Alisema bondia huyo alipewa pambano la nje ya nchi. Kumbe makubaliano yake na wakubwa zake yalikuwa akapigwe huko ili wakubwa hao wapate kisingizio cha kwenda kutafuta kocha ughaibuni.

Siku moja kabla ya safari, bondia alimweleza mkewe kwamba asishtuke atakapoona mumewe anachapika huko ugenini kwa sababu ni mipango tu.

Mke alikuja juu na kutangaza talaka iwapo matokeo yatakuwa hayo, hali iliyomuwia vigumu sana bondia wetu, kwani aliweka nadhiri ya kuwa tayari kufa kwa ajili ya kipenzi chake hiki.

Hivyo alipopanda ulingoni akashinda kwenye raundi za mapema. Fikiria mwenyewe hasira za mabosi waliokwisha kufunga mabegi ya safari.

Matapeli wa aina hii wasionekane kabisa kwenye sekta adhimu ya kilimo. Nakumbuka kauli yako Mama uliposema ni aibu kwa Afrika kulia njaa. Tunayo ardhi ya kumwaga tena yenye rutuba, mbegu bora za asili, rasilimali watu ya kutosha, na hata majira tuliyoumbiwa na Mwenyezi Mungu ni rafiki kwa mazao. Ukitaka kuvuna unayoyapanda, wafukuzie mbali sana hawa wezi. Wahenga walisema ukicheka na nyani utaambulia mabua.