Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Piga mswaki, piga deki, piga amani

Muktasari:

Na tunapiga walio mbele yetu tu. Iwapo wengine wanachafua amani kwa ufisadi wao, haituhusu. Iwapo wanatoa kila kitu benki yetu ya bongo, kwa amani na utulivu, sisi hatuna shida, shida ni nyinyi mnaojileta katika anga zetu. Kwa njia hii, ni nyinyi tu mnaovunja amani.

Mimi sipendi barua ya vitisho, hata kidogo. Na sipendi zaidi iwapo mtishaji hana hata uthubutu wa kutaja yeye ni nani. Ndiyo maana nilikasirika kupata barua jana. Sijui ilitoka kwa nani, lakini bila shaka mtaweza kuhisi.

We Makengeza,

Ushukuru kwamba wewe hukuwapo juzi kupokea mgawo wako wa mkong’oto. Kazi yako kutusema tu pamoja na mabwana zetu bila kujua kwamba aliyeshika nchi ameshika kila kitu. Kwa hiyo njoo tu, sisi ni wakarimu sana wa mikong’oto na yako imewekwa kwenye friji kwa siku ambayo utaonekana.

Maana najua unataka kuandika upumbavu wako kama kawaida. Eti tumewapiga wenzako ovyo. Badala ya kutulaumu sisi, walaumu na wao kwa kujileta mbele yetu tukiwa tumejiandaa. Nakwambia katika hali ile baada ya kujiandaa ipasavyo, tunaweza kupiga hata mama zetu au wadogo zetu, maana mikono inawasha hadi lazima tupige, kisha mnaleta vichwa vyenu mbele yenu. Hapo naweza kukubaliana na hawa mabwana zako kwamba ni lazima kubadilisha watu maana sisi tumelelewa kukong’ota, tumezoea kukong’ota na raha yetu ni katika kukong’ota hasa nyinyi mnaosumbua mabwana zetu. Hatutabadilika ng’o. Tena ng’o ya kong’ota.

Hebu jiulize juu ya maneno mawili ya Kiswahili.

Kwanza ‘jeshi’. Sisi ni jeshi, siyo huduma kama katika nchi zingine na wakati kaka zetu wanatumia kila aina ya silaha na nguvu kupambana na maadui wa nje, sisi kazi yetu ni kutumia kila aina ya silaha na nguvu kupambana na maadui wa ndani. Maadui wa ndani ni yeyote anayethubutu kuwa na wazo tofauti au kuonyesha hisia tofauti, hasa hadharani. Jeshi ni jeshi, unasikia rafiki. Kwa hiyo adui wangu ukitaka watu wa kubembeleza hamia kwingine. Na tunapiga walio mbele yetu tu. Iwapo wengine wanachafua amani kwa ufisadi wao, haituhusu. Iwapo wanatoa kila kitu benki yetu ya bongo, kwa amani na utulivu, sisi hatuna shida, shida ni nyinyi mnaojileta katika anga zetu. Kwa njia hii, ni nyinyi tu mnaovunja amani. Waache wao wanaoiba na kunyang’anya amani za watu kwa kuwahukumu maisha duni. Ili mradi wanaharibu kwa amani, viherehere vyote vya nini?

Pia, naona huelewi neno ‘piga’. Sera yetu ni ‘Piga Kwanza’ kwa sababu ‘piga’ ni msingi wa maendeleo. Asubuhi unafanya nini? Unapiga mswaki ili meno yasafishwe. Bila kupiga, meno yanabaki machafu na utaharibu maisha ya watu wengi kwa harufu unayotoa. Haya na ili nyumba iwe safi unapiga deki. Deki haisafishwi, inapigwa unasikia. Vinginevyo uchafu unang’ang’ania palepale.

Umenipata hapa adui wangu? Na ukitaka mawasiliano unafanya nini? Unapiga simu. Ndiyo. Bila kupiga, huwezi kutuma unatuma ujumbe unaoutaka. Na sisi tunatuma ujumbe kwa njia hiyo hiyo. Tena, upande wa kazi ni zaidi. Mfanyakazi bora anaitwa mchapakazi. Hafanyi kazi, hata hapigi kazi, anachapa kazi. Na bila kuchapa maendeleo yatapatikana wapi?

Ndiyo maana ukitaka nchi yenye amani, inabidi upige amani pia. Ndiyo au hata uchape amani. Amani haibembelezwi, haipatikani kwa pipi na ahadi tamu tamu. Lazima upige ndiyo amani ipatikane.

Kwa hiyo wewe njoo tukupige na wewe. Nadhani kwa njia hiyo tutanyoosha makengeza yako moja kwa moja. Wewe pigania haki au amani, sisi tunapiga.

Adui wako daima.

Duh, wakati nashika barua hii, akaja mwishiwa mwenzangu. Nilicheka, maana alikuwa amevaa kofia ya chuma.

‘We mwenzangu, tangu lini ununue bodaboda?’

‘Bodaboda ya nini mwishiwa mwenzangu? Hii ni kinga ya mikong’oto.’

Wacha tucheke kisha nilimwonyesha barua niliyoandikiwa. Baada ya kuisoma akaamka na kutaka kutoka.

‘Unaenda wapi rafiki yangu? Mbona mwoga hivyo?’

‘Uoga wa nini? Kwanza nikuachie kofia hii ya chuma, maana naona unahitaji zaidi yangu, kisha naenda kununua kofia nyingine.’

‘Wacha Bwana. Hebu tulia.’

Basi tukaamua kwenda kutafuta supu. Njiani alisema.

‘Lakini mwishiwa mwenzangu uliona mambo ya Wascottish?’

‘Niliona.’

‘Uliona kampeni zao zilivyokuwa kali?’

‘Kabisa, lakini sikuona mtu yeyote akivaa kofia ya chuma.’

‘Sawasawa. Hawakuwa na haja nazo. Raha sana kuweza kuongea kwa uhuru na kupigania kwa amani unachotaka bila kupigwa, wala amani kuchapwa.’

‘Na watu walitoa maneno mengi ya kuudhi, lakini wapi. Mwishoni viongozi pande zote mbili wanapeana heshima na polisi walilinda amani, badala ya kupiga amani.’

‘Nadhani shida ya hapa ni woga. Wanaogopa kuzidiwa hoja.’

‘Basi waende kutafuta hoja zaidi. Nakumbuka baada ya baba wa taifa kustaafu, wenzake wengine walimchukia sana na kumwita hata dikteta wakati silaha pekee aliyokuwa nayo ulikuwa ni mdomo tu, kauli. Lakini kwa kuwa aliwashinda watu sana kwa hoja, ilibidi watafute kumfitini wakati wao walikuwa na majeshi ya kila aina na vyombo vyote vya ukandamizaji. Nadhani walitamani kumpiga na yeye, lakini walishindwa. Fimbo yake ilitosha kama kofia ya chuma.

‘Sasa linalonishangaza mimi ni kwamba huko kwa Wascottish, ingawa wengi walitaka kujitenga, zaidi ya milioni, bado walipewa uhuru na walewale waliokuwa wanataka wasijitenge. Na mijadala ilikuwa wazi.’

‘Lakini ngoja nikupe siri rafiki yangu. Kuwaachia huru namna hii ilikuwa njia bora ya kuhakikisha kwamba hawatajitenga. Ukitaka watu waondoke, walazimishe kubaki. Uking’ang’ania kwa nguvu zote na kuziba midomo ya watu, wanazidi kuimarika katika kutaka kujitenga. Lakini iwapo yanajengeka mazingira ya kuheshimu mawazo yao hata kama unaona ni hatari, unaweza kudhibiti mihemko ya kutaka kujitenga. Ukiwaheshimu, hata kwa maneno na wao watakuheshimu pia. Ndiyo maana, ingawa hata mimi upande mwingine nimeshangaa kuona kwamba walitaka kubaki humu ndani, ilikuwa wazi kwamba walifanya uchambuzi na kupima kati ya mema na mabaya na kuona wabaki.’

‘Lakini nadhani pia, hata kama walishindwa, kwa kuwa walionyesha msimamo thabiti, watabadilisha hali ya Uingereza kwa ujumla moja kwa moja. Angalia watu walivyojitokeza kupiga kura. Kwenye uchaguzi hawajitokezi hivyo kwa sababu hata huko wamechoka tabaka la wanasiasa. Wamechoka ufisadi na unafiki wao. Wameshajua kwamba tabaka la wanasiasa ni sawa na tabaka la wanyonyaji wakubwa wanaofyonza jasho lao hadi damu yao.’

‘Mmmh! Mbona mkali mwenzangu.’

‘Ndiyo ukweli wenyewe. Na Wascottish wameonyesha kwamba watu wanaamka kila mahali duniani, kama walivyoamka Tunisia, Misri na sehemu nyingine. Ukuta uliowekwa na tabaka la wanasiasa kuficha ulaji wao unazidi kubomoka hivyo wasipojirekebisha mfumo mzima unaweza kubomoka na wao watakanyagwa kama mchwa waliokula nyumba. Na wanaoishi kwa kukong’ota wataishia kukong’otwa na wao.’

‘Ni kweli. Sasa kwa nini wenzetu hapa hawaoni hivi.’

‘Wanachoona ni chakula chao tu. Na pia hatujawaonyesha vizuri.’

‘Lakini tukitaka kuwaonyesha, wanapiga amani.’

‘Amani hauwezi kujengwa hivyo. Na hata sisi lazima tujue jinsi ya kupigania amani ya kweli dhidi ya wapiga amani kwa mbinu zenye akili zaidi, siyo kujipeleka hivihivi kwenye mdomo wa mamba.’

Wakati ule tulikuwa tumefikia kwenye supu kwa hiyo na sisi tuliamua kupiga mabakuli mawili.