Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia anaongozwa na falsafa gani katika uongozi wake?-4

Watumishi walio karibu na Rais SSH bila shaka wanafahamu zaidi juhudi zake za kuleta maridhiano katika sekta mbalimbali kuliko watu wa kawaida. Watu wa kawaida tunaona juu juu tu kama baba na mama wakianza kugombana hadharani bibi anawaambia “nendeni mkaongee ndani mie namalizia hadithi ya jana na wajukuu wangu!” Mathalani chukua sekta muhimu kama Jeshi la Ulinzi ambalo halikuwa na Amiri Jeshi mwanamke, kufumba na kufumbua kaingia SSH! Tukajiuliza je watakubali na kumtii?

Jeshi la Ulinzi popote duniani ni mhimili mkubwa wa amani kwa Taifa. Jeshi letu limetekeleza dhamana iliyonayo kwa taifa kwa utii uliotukuka. Licha ya kupata mafunzo kutoka nchi mbalimbali lakini limeweka uzalendo kwanza kwani, wanaelewa kuwa wao ni jamii moja. Pia wametumikia katika nchi jirani kila walipohitajika. Wanajitoa muhanga kwenda kulinda au kupigana kwa kufahamu kuwa kama nyumba ya jirani yako hana amani wewe pia hutalala.

 Kwa hiyo Jeshi letu lina heshima kubwa nyumbani na ugenini na mara moja likatambua Urais ni taasisi, yeyote atakae kalia kiti hicho watamtii. Kukubaliwa na Jeshi yalikuwa maridhiano muhimu hivyo tukashusha pumzi zetu na kupata amani na sababu ya kuvumiliana.

Jina likabaki Amiri, magwanda na buti yaleyale bali kofia ikabidi iwe juu ya hijab kulinda staha na utashi wa imani yake. Ikabaki suala la walinzi je watabaki kuwa wanaume au wapo walinzi wa kike wenye sifa za kumlinda Rais? Jibu likawa rahisi wapo, cha msingi watapewe mafunzo ya ziada kwani wanaweza. Tukamkumbuka marehemu Qaddafi yeye alikuwa na walinzi wanawake waliohitimu.

Kuvumiliana ni zoezi nyeti sana kwani machoni unaweza danganyika mko pamoja, lenu moja, mgange yajayo, lakini yaliyo moyoni mwa mtu ni siri kubwa! Pamoja na upungufu huo mkisharidhiana ni lazima kuwe na vigezo vya wazi kuwa mko tayari kuvumiliana maneno matupu hayakidhi nia.

Tuchukulie mfano mdogo ambao haukuanza leo. Jiulize kwa nini sifa nzuri zote apewe kiongozi/ mwanzilishi hata kama sie alietekeleza ndoto? Wanawake tunatabia fulani ambayo ni matokeo ya mfumo kandamizi. Unakuwa na wazo zuri la namna ya kutatua tatizo ndani ya ukoo. Lakini unaogopa kulitoa kwa kuwa litadharauliwa na watoa maamuzi ambao ni wanaume. Kwa hiyo unalisuka vizuri kwa mumeo mpaka analielewa kisha unamwambia akaliwakilishe yeye, unampaka mafuta kuwa yeye ni muongeaje mzuri.

Jamaa anakwenda kwenye kikao akijiamini kabisa na kuwakilisha kwa shagwe zote na kusahau kwamba lilkuwa wazo la mkewe. Mkewe ye anafurahi wazo limepita na mumewe kapata sifa zote. Ndio maana wakasema nyuma ya mafanikio ya mwanamume ni mwanamke na nyuma ya mafanikio ya mwanamke ni yeye mwenyewe japo sio wakati wote.

Katika jamii pana tumeshuhudia nchi zilizotawaliwa na wakoloni zikipambana bila kubaguana kila mmoja akitumia mbinu zake almuradi analengwa adui mmoja. Mfano mzuri ni Afrika ya Kusini na kabla yake Zimbabwe; kuna walio ingia mstuni na wengine walikwenda kusoma; kuna waliokimbia mateso nchini kwao na kujiunga na jeshi la msituni au kuongeza nguvu za kupinga ukoloni mkongwe.

Baada ya kupata Uhuru, chama ambacho kilishinda uchaguzi ndio kikawa Chama Tawala na wengine wapinzani. Hapa Afrika mfumo huo umekuwa chanzo cha kubaguana na migogoro isiyoisha.

Ni kama tumelazimishwa demokrasia ya vyama vingi ambayo tuliikubali kwa maridhiano na kuvumiliana lakini katika utekelezaji iliziba milango ya baadhi ya watendaji na viongozi wazuri.

Nchi inakuwa na vyama vya siasa 20 vyenye mitazamo mbalimbali kwenye nchi moja. Raia wanajibagua kwa itikadi wasizozielewa na sie wanawake sasa hivi hata hatueleweki, kila chama cha siasa kina wanawake wake ukichanganya na dini, makabila, asasi za hiyari ni mseto usio wa kawaida.

Ukichanganya na mitandao ya jamii na radio/luninga zilivyo sheheni je tunajenga maridhiano na kuvumiliana au tunajitayarisha kujibomoa? Je wote hawa wanaongozwa na itikadi ipi ya jamii?

Hata ndani ya Serikali kuna watendaji na viongozi wazuri katika ngazi mbalimbali lakini, wanajihisi kama wanacheza ngoma gizani nani anawaona? Nchi inaonekana haina wataalam au viongozi wenye uwezo kwa sababu ya mfumo, upendeleo au kujipendekeza.

 Enzi za mfumo wa zamani wa Serikali ulikuwa unapandishwa cheo kwa kukaa miaka fulani. Mfumo huu ulikuwa unakatisha tamaa kwa wenye juhudi na maarifa. Matokeo yake ufanisi kazini ulishuka. Haistahili kubweteka kusubiri upendeleo! Kila mtu afanye kazi kwa bidii ujuzi na maarifa. Ni wakati wakujenga upya namna gani wafanyakazi watapimwa na kupongezwa. Inaelekea mfumo wa mishahara haukidhi mahitaji ya wafanyakazi wala kiinua mgongo!

 Itaendelea kesho