Rais Samia anaongozwa na falasafa gani katika uongozi wake?-2

Tukio la Rais kufariki akiwa madarakani halikuwa ni geni kwa Watanzania kwani Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume aliuawa akiwa kazini. Tumeshuhudua kiongozi wa Taifa akifariki katikati ya utumishi wake kabla hajakamilisha ndoto zake. Laiti angemaliza muhula wa pili angetueleza kwa nini alifanya alivyofanya na kukiri pale alipokosea, lakini hakujaliwa kauli ya mwisho. Ikabidi kuulizana Katiba inasemaje, ilikuwa kindumbwendubwe chalia kwa wanasheria, wanasiasa na wazee wa hekima.

Uamuzi ukatolewa kwamba Katiba iheshimiwe na hivyo basi, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, atawazwe kuwa Rais kuondoa ombwe. Hilo nalo likawa gumzo la mji; mwanamke, Mzanzibari, Muislamu! Japo Samia alikuwa amezoea mikikimikiki ya kufanya kazi na Magufuli, na akatekeleza Ilani ya Chama chake 2015-2025, bado kulikuwa na hofu atavaaje viatu vya Magufuli! Wanawake na wapenda maendeleo walifurahia uteuzi wake japo sio wote.

Samia ni Rais mwanamke wa kwanza, Amiri Jeshi na Mwenyekiti wa Chama Tawala wa kwanza mwanamke Tanzania. Bila kutarajia akatwishwa dhamana iliyobeba Watanzania zaidi ya milioni 60. Je ataendesha nchi kwa falsafa na mikakati ipi!

Wakati wa kuapishwa SSH aliweka msimamo ambao ulisaidia kufungua fikra-mgando za wake kwa waume. “Huyu aliyesimama hapa katika umbo la KIKE ni RAIS. Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania! Kazi Iendelee!” Akaua ndege wanne kwa jiwe moja; Urais ni taasisi haubagui jinsi, tusibaguane kidini katika kusalimiana, udumu muungano na kazi iendelee.

Masuala haya yalihitaji maridhiano ya kifikra haraka, kwa hakika aliweza kukonga nyoyo za wengi. Kwa kujua au kutokujua alikuwa anatekeleza falsafa yake ya MARIDHIANO. Ukizingatia alikuwa Makamu wa Rais wa Magufuli ambaye ni mwanamume, alijua wengi watamwangalia kwa jicho tofauti. Je ataweza kufuata nyayo za Magufuli?

Ni dhahiri kwamba maridhiano peke yake hayatoshi. Wakati tunaanza mapinduzi ya uchumi kuna wanajamii waliopata maumivu, kuna sekta zilizofaidika kwa hiyo ni uvumilivu gani unahitajika? Ni mambo gani hayavumiliki ndani ya jamii? Je, wahenga walitumia mbinu gani kujenga ustahimilivu katika kaya na jamii kwa jumla? Tunajenga vipi ustahimilivu na watu wa nje? Je, diplomasia ya uchumi tunaijenga vipi ili iwe na maslahi kwetu?

Ili kupata uvumilivu lazima kuwe na mazungumzo na kusameheana. Ndipo vyombo vya habari vikawa huru, vyama vya siasa vikaanza kuongea, mijadala ya mikataba ikawapa wengi imani na kupoza munkari. Lakini maridhiano na uvumilivu peke yake havitoshi bila mageuzi.

Katika hotuba yake kwa taifa kupitia wanawake, Rais Samia alitumia sitiari kuelezea kwamba binadamu wote tuna nguvu sawa mithili ya pande mbili za sarafu moja. Alifafanua kuwa Mwenyezi Mungu katupa nguvu tofauti na zote ni nzito. Mwanamke ana uwezo wa kufanya uamuzi mgumu kama kutunga mimba na kulea, ana kipaji cha ushawishi kwa kutumia ulimi, ana subira na uvumilivu. Lakini kwa uvumilivu wake mwanamke anaangaliwa kama kiumbe dhaifu. Mwanamume anabeba mizigo, anajenga miundombinu, anafanya uamuzi mgumu kama kupigana vita.

Katika muktadha wa sitiari ya SSH, 2015 tulihitaji aina ya uongozi wa JPM ambao uliendana na hulka za wanaume; JPM hakutumia ulimi alitumia vitendo. Baba alitutandika viboko lakini akatuachia jengo, Mama analipa jengo uhai na joto la upendo.

Kumrithi aliyekutangulia sio rahisi, lakini kwa kutumia nguvu alizopewa mwanamke tunaona namna SSH anavyoongoza nchi. Kafunga mkaja ana demka kivyake hana papara! Si kazi rahisi kwa nchi yetu kubadilika haraka!

Kujenga upya ni mchakato, ni hatua ndefu; ni mapinduzi ya fikra na itikadi za jamii. Tumerithi mifumo kandamizi ya ukoloni iliyoathiri vibaya mila na desturi zetu kwa karne nyingi. Wakati umefika sasa tupate maridhiano ndani ya jamii. Wimbo wa taifa “Wake kwa Waume na Watoto hizi ni ngao zetu” na nembo ya Taifa iliyoshikwa na mwanamke na mwanamume inatukumbusha haki na usawa.

Wahenga wetu walikuwa na hekima, ujuzi, elimu na stadi za maisha ambazo ziliongoza jamii kila rika. Maendeleo ya Taifa lolote hayapimwi na vitu au nguvu za kijeshi. Taifa linapimwa kwa kuangalia hali ya wanawake, watoto na wazee, je, wana amani na furaha, wana afya, wanapendwa na wana maadili! Haya ni mapinduzi ya fikra ya kujitambua, kujiamini na kujithamini kama taifa yasiyo hitaji vita!

Je kuna uhusiano gani kati ya Serikali inavyoendesha nchi, Bunge linavyotunga sheria, na mahakama yanavyoendesha kesi na sisi wananchi ambao tuna imani zetu za kidini, za kimila zilizo dumu karne nyingi na vijana wa kisasa waso kwao! Je, falsafa ya SSH yenye mtangamano itaendelea kujenga fikra upya vipi ili tuendelee kuridhiana, ustahimiliana kuleta mageuzi chanya kama taifa?

Itaendelea kesho