Rais Samia anaongozwa na falsafa gani katika uongozi wake?-1

Samia Suluhu Hassan wakati akila kiapo cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Machi 19, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huongozwa na falsafa ambayo itamsaidia katika kukabiliana na changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi. Inambidi awe na hisia ya kujua mahitaji, matakwa na matarajio ya jamii. Je atakuwa mkombozi, msaliti au dalali madarakani?

Tanzania iliongozwa na marais watano katika mazingira tofauti. Awamu ya kwanza ni zao la harakati za kudai uhuru. Lengo kuu ilikuwa ukombozi dhidi ya uonevu wa kijamii, unyonywaji wa kiuchumi na kudharauliwa kisiasa. Tulikusudia kujenga nchi itakayozingatia ujamaa na kujitegemea. Tulikubali uchumi ujikite kwenye rasilimali zetu zaidi, kuliko pesa za kukopa au misaada. Msingi wa maendeleo ulikuwa ni ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora! Ubepari ni Unyama, Ujamaa ni Utu!

Miaka 10 ya kwanza ilionesha mafanikio ya maendeleo hata Waingereza walikubali. Lakini wakati tunaendelea kujipanga Idd Amin alituvamia tukaingia vitani. Japo tulishinda vita lakini luba walishaingia kwenye bwawa letu na kuanza kuharibu mifumo ya maisha yetu. Kelele za kutaka tuache kuwa maskini jeuri zilisababisha Mwalimu Nyerere ang’atuke kupisha matakwa ya wengi ya kurekebisha sera zetu za uchumi na kuachana na ushamba wa ujamaa na kujitegemea! Tukaingia katika Awamu ya Pili kwa mseleleko.

Tukajiunga katika ulimwengu wa utandawazi kwa matarajio kwamba na sisi tutakuwa sehemu muhimu ya maamuzi duniani na tutastawi kama wengine. Tulikubali kufungua milango ya soko huria, serikali ililazimika kuachia shughuli ya uchumi kwa wafanyibiashara za bidhaa na huduma. Awamu ya pili ikapewa jina la RUKSA! Kweli ikawa sandakarawe amina, mwenye kupata na apate, mwenye kukosa akose.

Mzee Mwinyi aliuona mtanziko akatoa tahadhari, “Ukifungua dirisha hewa itaingia, inzi na mbu nao wataingia. Kama utakula basi usikwangue mpaka ukoko!” Lakini tulikwisha kubali masharti ya wanaotawala Kijiji-Dunia. Tukafurahia vya nje bei poa, kafa Ulaya zimejaa na sabuni za kunukia tele tukasema kwaheri dawa ya mswaki ya majivu na mawese ya Kigoma!

Kwetu kukaanza kutetereka, wakulima na wazalishaji wengi waliumia. Bidhaa za ndani zikawa ghali kwa kukosa ruzuku na viwanda vilivyobinafsishwa vikakosa malighafi. Wafanyakazi wakapunguzwa kila mahali pamoja na serikalini.

Ikabidi awamu ya tatu idhibiti ruksa. Kukawa na mikataba, kanuni, taratibu, uwajibikaji, nidhamu na ufanisi serikalini. Juhudi za kupunguza ukali wa maisha zilikinzana na serikali kulipa madeni ya nje na ufisadi wa soko holela. Pamoja na kupata mamilionea wachache lakini ufukara nao ukaongezeka, jibu likawa mtaji wa masikini ni nguvu zako mwenyewe! Ndiyo yale ya RTD na ubepari, “kila mtu atakula kwa urefu wa kucha zake na ukali wa meno yake”!

Wakati tunalia ukata akaingia muungwana tunda la chama tawala; yeye hakuchelewa akatangaza Ari Mpya! Nguvu Mpya! Kasi Mpya! Matarajio ya kuondoa hali ngumu kwa kasi mpya yalikuwa makubwa. Wabongo hatukuelewa kuwa siyo rahisi kuvunja mikataba na wawekezaji ukisha vikwa nira. Mbinu za kasi za kidiplopmasia zilituvusha. Unaweza ukalinganisha na chenga kali za Pele, au ngumi za Mohamed Ali au labda kutembea angani kama Michael Jordan! Cha msingi nchi yetu ilikuwa imetulia.

Tukashutushwa na ngurumo la bulldozer usiku wa manane HAPA KAZI TU! Ndivyo tulivyoanza awamu ya tano, yaani hata tongotongo hazijatoka machoni ilibidi tugangamale! Tulishuhudia upepo wa kisulisuli dhidi ya ufisadi serikalini, baadhi ya wafanyibiashara walipigwa mwereka wakustukiza wa Bruce Lee! Wadau wa maendeleo wakafurahia kijino upande nao wakaimba Hapa Kazi Tu. Hatujakaa vizuri mikataba migumu nayo ikapigwa daflao, hapa palikuwa pazito! Ilipoingia UVIKO 19 na vipimo vya mbuzi, mapapai kugundulika wana Uviko ikazua tafrani ulimwenguni!

Watanzania tukaendelea na nyungu zetu na kazi huku awamu ya tano ikipepea na kuhamisha makao makuu kwenda Dodoma, miundombinu ya kila aina ikawepo na flyovers! Mageuzi kwenye huduma za afya na elimu hayakuachwa ili tuwe na nguvu kazi bora wakati tunaingia kwenye uchumi wa kati wenye sayansi na teknolojia. Kuhusu Katiba mpya kwanza kazi, maneno na mikutano badaaye. JPM hakujaliwa kumaliza muhula wa pili; Muumba wake alimchukua mapema. Samia Suluhu Hassan akashika hatamu; Je anaongozwa na falsafa gani?

Ni wachache wanajua falsafa zinazo mwongoza SSH. Nilisikia kwa mara ya kwanza wakati Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, alipowasilisha mada kwenye sherehe ya kuadhimisha miaka 36 ya TAMWA.

 Alituambia Rais Samia anaongozwa na mambo manne ambayo yanakamilisha falsafa yake katika kuongoza nchi; Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya. Nilijiuliza kwa nini maridhiano kwenye nchi tulivu kama Tanzania, ustahimilivu wa nini, ni mageuzi gani anayoyadhamiria na mambo gani ya kujenga upya? Ilibidi nifanye tathmini ya uongozi wa Rais Samia baada ya kuwarithi watangulizi wake watano wote wakiwa ni wanaume.

...Itaendelea kesho