Samia asimulia safari ya maisha yake kutoka ukarani hadi urais

Samia Suluhu Hassan wakati akila kiapo cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Machi 19, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Rais Samia amegusia ndoto yake kutaka kuwa mhudumu wa ndege, kufanya kazi ya ukarani  hadi kuja kuwa mkuu wa nchi.

Dar es Salaam. Machi 8, 2024, Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL),  iliendesha kongamano la nne la Jukwaa la The Citizen Rising Women na mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

 Kongamano hilo  lililofanyikia ukumbi wa The Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam, lilihudhuriwa na wageni mbalimbali akiwamo Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle.

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia alifanya mahojiano maalumu na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu aliyemuuliza mkuu huyo wa nchi wa kwanza mwanamke maswali mbalimbali kuhusu maisha yake na uongozi.

Katika mahojiano hayo, Rais Samia amegusia ndoto yake kutaka kuwa mhudumu wa ndege, kufanya kazi ya ukarani  hadi kuja kuwa mkuu wa nchi.

 Ni mahojiano yaliyochukua dakika 36 ambayo kuna nyakati yaliwafanya washiriki wa kongamano hilo kushangilia alipokuwa akijibu na kutoa ufafanuzi wa maswali hayo. Huu ni mtiririko wa mahojiano hayo.


Machumu: Miaka mitatu sasa baada ya kutoa tamko lako kuhusu kuwa aliyesimama hapa ni Rais mwenye maumbile ya kike. Nini kilikuwa ndani ya moyo na akili yako?

Rais Samia: Wakati natoa lile tamko nilikuwa nimekumbuka mambo ya kutiana moyo kwenye mazingira yetu ya maisha. Unajua mwanamume kama anafanya jambo na anaelekea kushindwa akienda kwa wenzie wanamwambia mlume jikaze nenda,  kwa hiyo na mimi siku ile nikasema hapa mlume ni kujikaza.

Nilisema bila kuwa na uhakika nakwenda kufanya nini lakini nilisema ngoja nisimame niwahakikishie Watanzania kwamba aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nilisema vile nikijua changamoto na wasiwasi uliopo mioyoni mwa watu kwamba ni mara ya kwanza kwa nchi  kupatwa na hali ile (msiba wa Rais akiwa madarakani) hivyo wengi walikuwa na hofu, halafu pia anayeingia angekuwa jibaba lenye misuli angalau roho zingetulia lakini anaingia mwanamke na vishungi vyake, anasema kwa wepesi zaidi, anatazama kama hataki.

Kwa hiyo nadhani wasiwasi ulikuwa mkubwa kwa watu nikaona ngoja niwatoe kwenye hofu, ile ilikuwa changamoto yangu ya kwanza nchi ina msiba ni lazima ivuke salama na aliyesimama ni lazima aoneshe nchi inaweza kuvuka. Kwa hiyo ule ulikuwa mtihani wangu wa kwanza.


Machumu: Ni nini hasa kilikusukuma kuhisi  watu walihitaji msimamo fulani?

Rais Samia: Yale maneno yaliwafanya watu waamini kwamba tumepata mtu ambaye kweli atasimama na kuivusha nchi. Kilichonisukuma kusema vile ni kwa sababu   tayari kulikuwa na minong’ono ataweza kweli huyu hebu angalieni, kweli inawezekana, mwanamke kweli, lakini nikawaambia aliyesimama hapa ni Rais lakini mwenye maumbile ya kike.

Urais hauna jinsi, ndiyo maana nikasema aliyesimama hapa ni Rais lakini maumbile yake ni ya kike. Urais hauna jinsi,  Rais ni Rais, mamlaka ni mamlaka.


Machumu: Umetugusia kidogo kuhusu kuwepo minong’ono

Rais Samia: Unajua hofu isingeacha kuwepo, kwa sababu tukio la kupoteza Rais akiwa madarakani halijawahi kutokea lakini pili mwanamke ndiye anaingia sasa kuchukua nafasi hiyo.

Pengine angekuwa mwanamke dume labda kidogo watu wangepata imani, lakini nimekuwa mwanamke kwa maana ya mwanamke kwa hiyo kidogo hii iliwapa watu hofu bila kujua kwamba akili haichagui kama ipo kwenye kichwa cha kiume au cha kike,  inategemea namna unavyoitumia.


Machumu: Wakati unakua ulitamani kuwa nani?

Rais Samia: Enzi zetu wakati upo shule ya msingi wala huwazi utakuwa nani, lakini nilipokuwa sekondari nilikuwa naona shirika la ndege la DRC na lilikuwa linafanya vizuri ndani ya Afrika.

Nilivyokuwa nawaona wale wahudumu wa ndege wanavyovaa nikawa navutiwa nikajikuta natamani kuwa kama wale. Hata hivyo, baba yangu alikuwa mwalimu na alitamani mtoto wake mmoja arithi kazi yake, akanipangia mimi.Nilipomaliza kidato cha nne nilienda hadi chuo cha ualimu lakini usiku wa siku hiyo niliyoripoti nikatoroka na kurejea nyumbani.


Machumu: Changamoto zipi ulikutana nazo utotoni na ulifanya nini kukabiliana nazo?

Rais Samia: Nikiwa shule ya msingi baba yangu alikuwa mwalimu, ikitokea kuna kosa la utovu wa nidhamu limefanyika darasani alikuwa akiniadhibu mimi ili kuwa mfano kwa wengine hilo siwezi kulisahau.

Nakumbuka pia nilipokwenda kuripoti Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM) Mzumbe Morogoro, kwanza ilikuwa safari yangu ya kwanza peke yangu halafu ilikuwa mara ya kwanza kwangu kusafiri nje ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Siku yangu ya kwanza chuoni pale IDM Mzumbe ilikuwa ngumu, niliangalia mazingira nikajikuta nalia, niliwaza likitokea tatizo nitatokaje kule. Matroni akaniuliza unalia nini, sikumwambia alinifariji hadi nikazoea mazingira, nakumbuka siku yangu ya kwanza chuoni nililia kama mtoto anayeenda kuanza darasa la kwanza.


Machumu: Kilio hiki kilikujenga vipi kupambana kufikia hapo?

Rais Samia: Kimenifanya nikue na nijue kwamba nilipofika ndiyo nimefika, naweza kupambana na nisimame mwenyewe na nilifanya kazi hiyo.


Machumu: Ni yapi yalikuwa mapito yako kutoka kwenye ukarani hadi urais.

Rais Samia: Ajira yangu ya kwanza nilikuwa karani wa kawaida, lakini jinsi nilivyokuwa nikifanya kazi nilikuwa najiona pale si mahali kwangu. Nikiwa pale nilikuwa natumika kukusanya data za watu wanaofanya masomo na walizokuwa wakizitumia kupata PhD zao.

Nikaona kumbe hata mimi naweza. Nikapata moyo wa kwenda mafunzo ya juu ili niweze kuondoka pale. Mwaka 1988 nikaajiriwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nikafanya kazi kwa miaka tisa.

Nilipata uzoefu mkubwa na mwelekeo mpya wa kazi ulionifanya nisifikirie tena kufanya kazi serikalini. Mkataba wangu ulipoisha nikaenda kufanya kazi kwenye asasi zisizo za kiserikali ndipo nilipapata muda wa kutosha kufanya kazi na wananchi.

Nilikuwa napenda kufuatilia vikao vya baraza la wawakilishi, nikaona yale yanayozungumzwa mule si yanayowagusa wananchi, nikahamasika kutamani kwenda huko ili nikawazungumzie wananchi.

LIVE: Rais Samia akishiriki kampeni ya ‘The Citizen Rising Woman’

Naweza kusema kilichonivuta kuingia kwenye siasa ni kuwasema wananchi, nikauliza taratibu nikaambiwa na watu wakaniitikia nikapata nafasi ya uwakilishi wa wanawake ndani ya baraza.

Hata hivyo, wiki mbili baada ya kuapishwa kama mjumbe, Rais akatengeneza Serikali yake nikajikuta nimekuwa waziri tena nikiwa mwanamke peke yangu kwenye baraza.

Nilipoenda jimboni ndiyo nilijua siasa ni nini, kule ndiko walinipevusha haya yanayosemwa sasa hivi, kwa mimi ni pwani, ninakotoka kule ndiyo bandarini.

Jimbo lile halikuwahi kuombwa na mwanamke mimi ndiye nilikuwa wa kwanza, wakati huo nimetoka kwenye mashirika ya kimataifa, haya mambo mnayoniona nayo sasa hivi ya vishungi na mitandio hayakuwepo, kama mtandio upo basi upo begani.

Haikuwa rahisi kwa mwanamke kukubalika kwenye jamii ile, nilisoma hali ilivyo nikakaa na wanawake nikawaelimisha kwa kuwaambia yote mnayoyasikia yanasema kuhusu mimi sio yangu peke yangu ni yenu pia, kwa hiyo msiponiunga mkono ina maana mnayakubali.

Nilizunguka jimbo lote na nikafanikiwa kuungwa mkono na wanawake nikachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo. Niliteuliwa kuwa Waziri katika ofisi ya Makamu wa Rais, nilikaa miaka mitano, sikuwahi kubadilishwa kwenye wizara.

Wakati napewa Unaibu Spika wa Bunge la Katiba, nilikuwa sijui hata Bunge linaendeshwaje. Lile Bunge likanipika. Nilivyoteuliwa kuwa mgombea mwenza haikunitisha kwa sababu nilijua kuna mtu juu yangu, lakini nilipokabidhiwa nchi niseme ukweli pale kijoto kilinipata.


Machumu: Nini ushauri wako kwa wanasiasa wengine wanawake kwenda majimboni?

Rais Samia: Wanawake wanapokwenda majimboni wanapaswa kujua lengo lao, mbali na lengo ni lazima uwe na mbinu ya kuingia na kuweza kuvuka vizuri.

Wote tunafahamu kwamba hamasa kwenye vyama vya siasa ipo kwa wanawake, kwa hiyo mbinu ya kwanza ni kwenda kukaa chini na wanawake huko majimboni. Na wanapokwenda wajue kuna maneno mengi, kinachotakiwa ni kuwaelimisha wanawake kwamba haya yanayosemwa si yangu bali ni yetu sote.

Pia, uwaeleweshe lengo lako sio tu kwamba unataka kuwa mbunge lazima useme ni kwa ajili gani na kitu gani utafanya. Ukielewana vizuri na wanawake walio chini watajitoa na kukunga mkono, wanaume wakiona wanawake wamesimama kwa nguvu moja na wenyewe watakuunga mkono.

Rais Samia Suluhu Hassan (kushoto) alipofanya mahojiano ya ana kwa ana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu (kulia) jana Ijumaa Machi 8, 2024 katika jukwaa la The Citizen Rising Woman lililoandaliwa na MCL.


Machumu: Uliwahi kufikiria kuwa ungekuwa kwenye nafasi  ya makamu wa Rais hadi urais?

Rais Samia: Ndoto yangu ilikuwa kwenye ubunge au baraza la wawakilishi, hata nilipotangazwa uwaziri nilishangaa, sikuwahi kuwa na ndoto ya kuwa makamo wa Rais wala Rais. Niliingia kwa makusudi nikawe mbunge nikasemee watu, mengine yaliyotokea yalitokea labda kwa sababu ilionekana naweza.


Machumu: Joto lilikuwaje ulipopokea kijiti cha urais?

Rais Samia: Joto nililopata ni kwamba naenda kuwa mkuu wa nchi na amiri jeshi mkuu, hiyo ni kazi pevu. Na kama mnavyojua wakati ule marehemu Rais wetu (John Magufuli) anaondoka tulikuwa tumeanza miradi mikubwa.

Kichwa kilinizunguka nitafanya vipi, nitapata wapi fedha ya kufanya yote haya. Niliwaza pia mapokezi yangu kama Rais wa kwanza mwanamke, nifanye nini ili wakubali kwamba unaweza, kwa kweli ilikuwa inaumiza kichwa.

Wakati naingia pia dunia ilikuwa kwenye janga la Uviko, uchumi unashuka, miradi inakutazama ilikuwa tanuru la moto,  lakini nikasema kama nilishika kitabu ninachokiamini na kuapa kuilinda nchi hii basi nikasema Mungu atanionesha njia.

Pia, nilitumia ujuzi na uzoefu niliokuwa nao,  kwa kifupi nilitumia mbinu za medani. Namshukuru Mungu nimeweza.


Machumu: Kuna wakati ulipowaapisha mawaziri,  ulisema wewe ni mama wakikuzingua mtazinguana, vipi wanakuzingua?

Rais Samia: Mimi ni mama, kwa bahati nzuri wengi niliowateua mimi ni mama kwao, wengi nina uwezo wa kuwazaa, na ndiyo maana nikapata uthubutu wa kuwaambia ukinizingua tutazinguana.

Nadhani huwa wanamsikia Zuhura (Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu) kila anayenizingua anafanya yake usiku usiku wakiamka wale walionizingua wanajikuta hawapo, waliobaki tunakwenda vizuri.


Machumu: Nini hasa yalikuwa maono yako kwenye falsafa ya 4R?

Rais Samia: Falsafa ya 4R ilikuja kwa sababu wakati ule naingia madarakani, jambo moja kubwa nililiambiwa ‘mama unganisha Taifa.

Sasa ile sentensi ikanipa mawazo, nikawa najiuliza kwa nini watu wanasema mama unganisha Taifa, kuna nini na wapi Taifa limegawanyika.

Kwa hiyo nikafanya kazi ya kusoma ile hali ilivyo na nikasema sasa nadhani tunahitaji kukaa na kuja na falsafa tunayoweza kuitumia kuliunganisha Taifa na tukaenda mbele.

Nikaanza mazungumzo na  vyama vya siasa, kutengeneza kamati mbalimbali kuangalia hali ilivyo ndani ya nchi na vipi inaweza kurekebishwa. Kwenye suala zima la ustahimilivu kama tumekosana basi tustahamiliane, tuvumiliane turudi tuzungumze tusonge mbele na tukisonga mbele tufanye mabadiliko katika yale tuliyokubaliana.

Nashukuru Watanzania ile falsafa ya 4R imepokewa, vyama vya siasa vimepokea, tunazungumza, tumekubaliana kuna ambayo hatukukubaliana tunavumiliana kama tunavyoona watu wanaandamana.

Kama wanataka maandamano fanyeni, naviambia vyombo vya ulinzi na usalama walindeni wasindikizeni mpaka wanapofika waacheni waseme wanayosema wakimaliza hakikisheni wanatawanyika vizuri hakuna kugombana wala kufinyana.

Katika masuala ya kitaifa,   vyama vya siasa, wadau wa maendeleo,  tumekuwa tukikutana na kujadiliana.

Kushirikisha  wengi kumenisaidia katika kufanya maamuzi kama kiongozi wa nchi.

Siyo kwamba nisingeweza kujifungia peke yangu na kuamua ningeweza tu na nina mamlaka hayo,  lakini kama ninavyosema kila siku hakuna mwenye warrant ya kuongoza nchi. Hii  nchi ni yetu sote,  ukishirikisha wengine unakwenda vizuri. Nimechagua njia ya kushirikishana na ndiyo maana mambo yanakwenda.


Machumu: Tutarajie nini katika kipindi kilichobaki kuelekea kwenye uchaguzi mkuu?

Rais Samia: Wanawake wajitokeze kwa wingi kwenye chaguzi, kuanzia Serikali za mitaa twende tukapambane huko. Tafiti zinaonesha taasisi ambazo kwenye uongozi kuna wanawake wengi mafanikio yanakuwa makubwa.

Endapo kwenye ngazi za vijiji, mitaa kutakuwa na wanawake wengi watakuwa na fursa ya kushughulikia changamoto zinazohusu jamii yao. Tunapokwenda kwenye uchaguzi mkuu na kule tunahitaji wengi zaidi. Ningependa wanawake wawe wengi kwenye baraza, lakini wawe wale wenye uwezo.

Sio tu kujazana kwa sababu tunataka 50 kwa 50 lazima iwe ni kwa wale wenye uwezo. Tuendelee kuweka utulivu na amani kuelekea chaguzi hizi.


Samia ni nani?

Samia alizaliwa Januari 27, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar. Ameolewa na Hafidh Ameir na wamejaaliwa watoto wanne, watatu wa kiume na mmoja wa kike.

Alipata elimu ya msingi katika shule mbalimbali, zikiwamo Shule ya Msingi Chwaka iliyoko Unguja kuanzia 1966 hadi 1968, Shule ya Msingi Ziwani mwaka 1970 na Shule ya Msingi Mahonda mwaka 1972.

Baada ya hapo, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Ng’ambo kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza hadi cha tatu na Shule ya Sekondari Lumumba kwa ajili ya kidato cha nne kati ya mwaka 1973 hadi 1976.

Mwaka 1983, alipata astashahada katika mafunzo ya takwimu kutoka Chuo cha Uchumi Zanzibar. Baada ya kufanya kazi kwa kipindi kifupi kwenye Wizara ya Mipango na Maendeleo, mwaka 1983 hadi 1986, alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM) kwa ajili ya masomo ya juu katika utawala wa umma.

Pia, alipata mafunzo mbalimbali katika  Chuo cha Utawala wa Umma Lahore, Pakistan 1987, Taasisi ya Eastern and Southern African Management Institute (ESAMI) 1991 na Taasisi ya Uongozi ya Hyderabad India 1998 kwa ajili ya astashahada ya utawala.

Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester kilichopo Uingereza kwa ajili ya masomo ya juu ya uchumi.

Vilevile, alipata shahada ya uzamili ya maendeleo ya jamii kupitia programu ya pamoja kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire, Marekani.

Mbali na nafasi za urais na makamu wa Rais, nyadhifa nyingine alizoshika ndani ya Serikali ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano 2010/2015; Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar 2005/2010 na Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake, na Watoto, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2000/2005.

Mwaka 2014, alihudumu Makamu Mwenyekiti wa Bunge lililojadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuandaa rasimu ya Katiba mpya ya Tanzania.

Mwaka 1987 hadi 1988, alikuwa ofisa mipango rasilimali watu na mwaka 1977 hadi 1983, alifanya kazi ya ukarani masijala.

Mwaka 2016,  Samia aliteuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon, kuwa mjumbe wa jopo la Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, akiwakilisha kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kati ya mwaka 2016 na 2017.

Katika kipindi cha ujumbe wake, aliwasilisha mambo 27 kwenye jopo hilo, ambayo Serikali ya Tanzania ilibainisha kama hatua za kimkakati, kwa ajili ya kuweka mfumo endelevu wa kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.