Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali Mbeya ijiandae kwa kulaumiwa, kupongezwa miradi hii Mbeya

Wakati Serikali mkoani Mbeya ikijivunia baadhi ya miradi ya kimkakati hususani upande wa miundombinu ya elimu, kwa sasa wananchi wanasubiri kwa hamu kuona utekelezaji wa miradi miwili mikubwa.

Miradi hiyo ni barabara ya njia nne yenye urefu wa kilomita 29 kutoka Nsalaga hadi Ifisi, ambayo hadi kukamilika kwake itagharimu Sh138.7 bilioni ambayo kwa kiasi kikubwa itaondoa changamoto ya msongamano magari jijini Mbeya.

Mbali na msongamano, itapunguza pia ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikiripotiwa, huku wananchi wakiona suluhisho lake ni kumaliza ujenzi wa barabara hizo za kimkakati.

Mbeya imekuwa ikiandamwa sana na ajali za mara kwa mara ambapo matarajio ya wananchi wengi ni kuona kukamilika kwa barabara hizo, kunaweza kuwa suluhisho la ajali.

Tumeshuhudia mipango na utekelezaji wa miradi upande wa elimu na afya kwa ujenzi wa madarasa na vituo vya afya, zahanati na hospitali, hivyo kwa sasa matamanio yetu ni kuona mradi huo wa barabara sambamba na ule wa maji kutoka Mto Kiwira.

Kwa sasa kilio zaidi kwa wananchi ni huduma ya maji, ambapo wakazi wa jijini Mbeya wanasubiri kwa hamu, mradi wa maji ili kuwaondolea adha.

Mradi huo ambao ambao unatarajia kukamilika mwaka huu, wananchi wanaona utekelezaji wake kama unasuasua kutokana na hatua iliyofikia ya asilimia 40, ukilinganisha muda uliobaki kukamilika.

Hadi kukamilika kwa mradi huo mkubwa na wa kimkakati, utagharimu Sh 119 bilioni huku ukihudumia wananchi zaidi ya milioni moja na kuzalisha lita 117 kwa siku na kumaliza kero ya maji jijini hapo.

Turudi kwenye mradi wa barabara. Kwa sasa mradi huo ulipaswa kuwa umekamilika kufikia Machi 31 kwa mujibu wa mkataba, lakini umesogezwa mbele hadi kabla ya uchaguzi mkuu, Oktoba 25 mwaka huu.

Kinachoendelea bado wananchi hawajaridhishwa na utekelezaji wake kwakuwa hatua ilipofikia haiendani na uhalisia wa mkataba huo, licha ya changamoto nyingi zinazotajwa kukwamisha kukamilika kwake kwa wakati.

Awali ilielezwa tatizo kubwa kuwa lilikuwa fedha, ambapo ilifikia hatua mkandarasi anayejenga kusimama kwa muda kwa madai ya kukosa fedha.

Hata hivyo, Serikali ilipambana na kulipa kiasi cha zaidi ya Sh 90 bilioni na kumfanya mkarandarasi kurejea kazini, ambapo kwa sasa anapaswa kukabidhi mradi huo kabla ya muda aliopewa.

Kwa upande wa mradi wa maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira, unasubiriwa zaidi na wananchi kutokana na kero ya uhaba wa maji iliyopo katika maeneo mengi jijini humo.

Iwapo miradi hiyo miwili itakamilika kwa wakati kulingana na mikataba, huenda wananchi wakaongeza imani kubwa kwa Serikali katika kuwafikishia huduma muhimu kama ilivyo kwenye sekta nyingine.

Pia wakati Serikali ikitimiza ahadi hizo, iangalie uwezekano katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 kuongeza kiwango kwa ajili ya barabara za pembeni ambazo ni changamoto kubwa kwa wananchi.

Kwa sasa maeneo mengi ya Jiji la Mbeya barabara zake za mitaani si nzuri na pale mvua inaponyesha husababisha karaha kwa watumiaji, hivyo wakati ikipambana na barabara ya njia nne isisahau za pembeni.

Pia maeneo mengine ya barabara kuu zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) nazo zinahitaji kuboreshwa kutokana na kuchimbika sana na kusababisha kero kwa watumiaji wa njia hizo.

Badhi ya maeneo ni barabara kuu Tanzam, inayotoka Uyole kuelekea mjini ambapo baadhi ya sehemu zimekwanguliwa na kuwa mashimo, hivyo kuwapa wakati mgumu madereva wa vyombo vya moto.

Lakini pia itazame uwezekano wa kuboresha vyanzo vingine vya maji kusaidia upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi, ambapo baadhi ya maeneo wanahangaika kupata maji.

Kama haitoshi, yapo maeneo mengine maji ni ya mgawo, hutoka nyakati za usiku hali inayowapa changamoto wananchi kuamka usiku wa manane kukinga maji na kusababisha migogoro kwenye familia.

Iwapo miradi hiyo itakwama, inaweza kuchukuliwa katika hali ya kisiasa kwamba huenda Serikali iliwahadaha wananchi wake na kuwapa nguvu wapinzani kuona namna ambavyo wameshindwa kuwahudumia wananchi.

Hili itakuwa changamoto kwa Serikali kuhakikisha inatimiza ahadi hiyo kwa wananchi wake na kuwapiga bao wapinzani ambao wanasubiri kwa namna fulani kuitumia kwenye kampeni kama sehemu ya mkwamo wa CCM.