Simba SC wasiidharau Kaizer Chiefs

Simba SC wasiidharau Kaizer Chiefs

Muktasari:

  • Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya mabingwa Afrika, Simba wamepangwa kukutana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ambayo mechi zake za mwanzo zitachezwa wiki mbili zijazo.

Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya mabingwa Afrika, Simba wamepangwa kukutana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ambayo mechi zake za mwanzo zitachezwa wiki mbili zijazo.

Droo na upangaji wa ratiba ya hatua hiyo ambayo itahusisha timu nane zilizoshika nafasi mbili za juu kwenye makundi manne ya mashindano hayo, ilifanyika juzi Ijumaa huko Cairo Misri yaliko makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Mbali ya Simba kupangwa dhidi ya Kaizer Chiefs, mechi nyingine katika hatua hiyo zitakuwa ni baina ya Al Ahly dhidi ya Mamelodi Sundowns, Wydad Casablanca dhidi ya MC Alger huku Esperance ikipangwa kuumana na CR Belouizdad.

Timu itakayopata matokeo mazuri katika mechi mbili baina ya Simba na Kaizer Chiefs itakwaana na mshindi wa mechi baina ya Wydad Casablanca na MC Alger kwenye hatua ya nusu fainali wakati atakayepita baina ya Mamelodi na Al Ahly ataumana na kinara wa mechi kati ya CR Belouizdad na Esperance.

Kumekuwa na matumaini makubwa kwa mashabiki na wadau wa mpira wa miguu nchini, kwamba Simba itafanya vizuri dhidi ya Kaizer Chiefs kutokana na kiwango bora ambacho imekuwa ikikionyesha katika mashindano hayo msimu huu kuanzia katika hatua za awali hadi zile za makundi.

Kitendo cha kuongoza kundi lake ikiwa imepata ushindi dhidi ya timu bora, ngumu na zenye uzoefu wa mashindano kama AS Vita na Al Ahly kimeleta imani kwamba safari hii Simba inaweza kufika mbali tofauti na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma pindi ilipkuwa ikishiriki mashindano hayo.

Lakini si tu kuongoza kundi, bali pia Simba imeonyesha kiwango bora cha kitimu na cha mchezaji mmojammoja na ndio maana haijawa jambo la kushangaza kuona ikiwa miongoni mwa timu vinara katika kufumania nyavu ikiwa imepachika jumla ya mabao tisa huku pia ikiwa ikishika nafasi ya pili kwa timu ambazo zimeruhusu idadi ndogo ya mabao katika hatua ya makundi baada ya nyavu zake kutikiswa mara mbili tu

Ukiweka kando takwimu hizo, Simba pia inajivunia rekodi yake nzuri dhidi ya timu kutoka nchi zinazounda Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika pindi inapokutana katika mashindano ya Afrika.

Simba wamekutana na klabu kutoka COSAFA mara 50 ambapo katika hizo, imeibuka na ushindi mara 26, ikitoka sare mara 11 na imepoteza idadi ya michezo 13.

Katika awamu 26 tofauti za mtoano ambazo imekutana na klabu za Kusini mwa Afrika, Simba imevuka mara 19 na mara saba (7) ilijikuta ikitupwa nje.

Hata hivyo pamoja na Simba kupewa nafasi kubwa kuitoa Kaizer Chiefs, haipaswi kubweteka na kujiamini kupita kiasi hadi kupelekea wajione kama wameshatinga hatua ya nusu fainali.

Wanapaswa kujiandaa vilivyo kimbinu na kiufundi kwa kufanyia kazi udhaifu walioonyesha katika hatua ya makundi lakini pia kufanya tathmini ya kina juu ya ubora na udhaifu wa wapinzani wao na kisha kutafuta mpango bora wa kuhakikisha haiwapi mwanya Kaizer Chiefs kuwaadhibu.

Simba ni lazima ijue kwamba mafanikio iliyoyapata yanaweza kuisababishia matatizo yenyewe kwani bila shaka yamezishtua timu na kila moja lazima ijiandae kikamilifu pindi inapopangwa kukabiliana nayo.

Pamoja na yote, Kaizer Chiefs ina kundi kubwa la wachezaji wenyewe uwezo binafsi, walio na uzoefu wa kucheza mechi za hatua kubwa na muhimu kama hii, hivyo bila shaka itawategemea kama silaha muhimu pindi itakapokabiliana na Simba.

Wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa bila shaka wanayo kumbukumbu ya jinsi walivyotolewa na timu dhaifu ya UD Songo ya Msumbiji katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/2019 kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya bao 1-1 hapa Tanzania huku wakiwa wametoka sare tasa kule Msumbiji.

Ilionekana na wengi kwamba Simba ilikuwa na nafasi kubwa ya kuwatoa Songo baada ya msimu mmoja nyuma kuonyesha kiwango bora na kutinga robo fainali lakini safari yao ikaishia kwa raundi ya awali.

Bila shaka Simba hawako tayari kuona hilo lilitokea tena na wanajiandaa kikamilifu ili waweze kuikabili Kaizer Chiefs wakiwa wamekamilika kiufundi, mbinu na kiakili.