Taasisi zinazosemekana kuwasaidia wastaafu lakini wastaafu wako pale pale!
Iwapo taasisi na vikundi kadha wa kadha vinavyoanzishwa kwa kile kisemekanacho kuwa ni kwa ajili ya kumsaidia mstaafu awaze kukabiliana na hali ngumu ya maisha anayokabiliana nayo, zingekuwa zinafanya kazi kweli, wastaafu wangekuwa sasa wanapokea pensheni ya shilingi milioni moja kwa mwezi..
Mstaafu wetu anaomba tena kurudia hapo ili kuweka msisitizo. Inawezekana kumlipa mstaafu aliyelijenga Taifa hili Pensheni ya shilingi milioni moja kwa mwezi. Inawezekana. Ni utashi tu.
Kama tunaweza kuwalipa wabunge karibu 400 shilingi milioni 16 kila mwezi kila mmoja, kwa miaka mitano tu, basi tunaweza pia tukamlipa mstaafu aliyelijenga na kulifikisha Taifa hapa pa watu kulipana shilingi milioni 16 kwa mwezi! rudia tena, ni utashi tu.
Vingi ya vikundi, taasisi na NGO’s hizi hushamiri zaidi kuanzisha hasa wakati linapokuwepo suala la kuwastaafisha waajiriwa, hasa wale wa ngazi za chini za ajira, ambao haileweki siku zote kwa nini mafao yao hucheleweshwa na kuzungushwa zungushwa.
Mstaafu wetu hajawahi kusikia wala kuona vikundi, NGO’s na taasisi hizi zikianzishwa fasta ili kumsaidia waziri, katibu mkuu ama mkurugenzi wa shirika la umma ambaye ni muajiriwa wa wananchi anapostaafu. kucheleweshewa pensheni yao kiasi cha vikundi hivi kuazishwa na kuwepo! Huwa ni kwa ajili ya wastaafu walalahoi.
Kamwe huwezi kuwaona 'waajiriwa' wa aina hii, ambao Katiba yetu hufikia kuwafanya waajiri wetu wakati wao ndio wanaopaswa kuwa waajiriwa wetu, wakipanda na kushuka ngazi kwenye ofisi za vibubu vyetu wakifukuzia mafao, never! Ndio, kamwe kwao hakuna kuhakikiwa.
Tuna miaka karibuni 30 sasa taasisi na vikundi hivi vilivyopo kwa madai ya kumpigania mstaafu vipo lakini wastaafu wetu wa Taifa wa kima cha chini bado wanaendelea kupokea pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi, elfu hamsini iliyoongezwa Januari hii, ili kuboresha maisha yao.
Tuache utani wa Kinondoni na maisha ya wastaafu jamani!
Inasikitisha Sana kwamba baada ya miaka 30 ya uwepo wake, bado mstaafu wetu anategemewa 'aboreshe' maisha yake kwa shilingi laki moja kwa mwezi, ukiacha hio elfu hamsini iliyoongezwa kwa bashasha kuanzia Januari mwaka huu na kumfanya mstaafu apokee shilingi laki moja na elfu hamsini, kwa mwezi ! Na hizi taasisi, NGO’s na vikundi
vilivyoanzishwa ili kumsaidia mstaafu vipo!
Mstaafu wetu anajua kuwa nyingi ya taasisi na NGO’s hizi zina magari na ofisi zenye samani za bei mbaya zinazolipiwa na wafadhili.
Mstaafu anaiomba hapa aviweke kando vile vikundi ambavyo huibuka zaidi wakati mstaafu akisaka mafao yake na ofisi zake mara nyingi ni 'mobile' yaani ziko kwenye briefcase!
Sana sana ni kumsaidia mstaafu kuyapata haraka....Kwa malipo maalumu na ada ya kila mwezi, wakati pensheni ya laki moja na elfu hamsini ya 'kuboresha' maisha ya wastaafu' yako duni pale pale!
Haya, pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi, matibabu ya bure kwa wazee wa kuanzia miaka 60 imeishia kuwa maneno ya kanga' kutaka vibubu vya wastaafu vianzishe benki ndogo ya kuwapa mikopo midogo yenye riba na tozo nafuu maana hela yao wanayo na wanaifanyia biashara, yote yameshindikana na imebaki hadithi tu.
Sasa taasisi, NGO’s na vikundi binafsi lipi lingine wanaloweza kufanya kumsaidia kweli mstaafu?