Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TAHARIRI: Suala la udanganyifu wa nauli, TRC itumie teknolojia

Wiki iliyopita, umma wa Watanzania ulijulishwa kupitia taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa kumekuwepo na udanganyifu katika ulipaji wa nauli kwa safari za treni SGR ambayo imeanza karibuni.

Kuna msemo wa Kiswahili usemao, "usipoziba ufa, utajenga ukuta," ukimaanisha kuwa jambo lisipodhibitiwa mapema linaweza kugharimu pakubwa zaidi, hivyo hili la SGR ni lazima lidhibitiwe mapema kwa kutumia teknolojia ya kidijitali.

Ni lazima Shirika la Reli Tanzania (TRC) likubali kuwa dunia inahama kutoka matumizi ya analojia kwenda dijitali, ikihusisha matumizi ya programu za kielektroniki katika ukataji tiketi na kudhibiti udanganyifu.

Takukuru katika taarifa yake ilieleza kuwa uchunguzi wake umethibitisha kuwepo baadhi ya abiria wanaotoka Dar es Salaam na kulipa nauli ya vituo vya njiani, huendelea na safari hadi vituo vya mbali bila kulipa nauli inayostahili.

Taasisi hiyo ilitaja vituo vilivyokithiri kwa abiria kupitiliza vituo walivyolipia kuwa ni Pugu, Soga, Ruvu na Ngerengere. Walisema kama vitendo hivyo vitaachwa viendelee, TRC itashindwa kujiendesha hapo baadaye.

Siku moja baada ya Takukuru kufichua udanganyifu huo, TRC ilijibu kwa taarifa kuwa tayari imewakamata watu wanaohujumu usafiri wa SGR kwa kutolipa nauli sahihi, na pia imewakamata wale wanaokatisha tiketi na kuzilangua.

TRC, kupitia Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Jamila Mbarouk, ilieleza kuwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara. Tofauti na awali ambapo abiria walikuwa hawakaguliwi tena wakishapanda treni.

Mbali na ukaguzi huo ndani ya treni, shirika hilo limesema sasa litakuwa likikagua tiketi wakati wa kupanda na kushuka, na mashine zao zina uwezo wa kuwabaini abiria waliofanya udanganyifu kwa kupiga kelele.

Tunaipongeza TRC kwa kuchukua hatua hizi kwa haraka, lakini tunaona bado wana uwezo wa kuja na teknolojia rafiki ambayo haitaleta usumbufu kwa abiria na kufanya usafiri huo wa SGR kuwa kero kwa baadhi yao.

Tunasema hivyo kwa sababu, endapo hakutakuwepo na mfumo bora wa kidijitali katika kuingia na kushuka ndani ya treni, na badala yake kutumia watu kukagua abiria wanaposhuka au kupanda, tuna wasiwasi kuwa tutashuhudia foleni vituo vya SGR.

Tunaamini kuna mifumo na programu za kisasa za kompyuta kwa ajili ya ukataji tiketi wa kidijitali, kama zile zilizotumika katika Kombe la Dunia, ambazo zilihakikisha walioingia ndani ya uwanja ni wale tu waliokata tiketi.

TRC inapaswa kwenda kujifunza kutoka mataifa mengine namna wanavyoendesha treni zake za kisasa na wanavyotumia mifumo kudhibiti udanganyifu. Kama Takukuru walivyosema, "usipoziba ufa, utalazimika kujenga ukuta."

Ni lazima TRC iende na kasi ya teknolojia ya kidijitali, ikiwezekana msafiri awe na kadi maalumu ya kuchanja anapoingia mlangoni na anapotoka, ili kupunguza hitaji la wahudumu kukagua tiketi kwa macho.

Mhudumu wa SGR awe anasimama tu katika mlango wa kuingia kwenye treni kuhakikisha kila abiria anayeingia amechanja kadi yake, na wakati wa kushuka pia kuwe na wahudumu kuhakikisha kila anayeshuka amechanja kadi.

Tunaamini hii itapunguza kwa kiasi kikubwa TRC kutumia rasilimali na nguvu kazi kubwa katika kukagua tiketi ndani ya treni au wakati wa kuingia, na hivyo kuepusha foleni, adha, na usumbufu kwa abiria. Dijitali ndio mkombozi wa sasa.