Tamu, chungu za mtoto kulelewa na mzazi mmoja

“Binafsi nimelelewa na mzazi mmoja ambaye ni mama, sijawahi pata hata mapenzi ya baba.”

Ni kauli ya John Haule, mkazi wa Kinondoni Jijini Dar es Salaam, ambaye nilizungumza naye wiki iliyopita kuhusiana na athari au faida ya mtoto kulelewa na mzazi mmoja.

Haule anasema malezi ya mzazi mmoja yana changamoto nyingi. “Nasema hivi kwa sababu nilikuwa namshuhudia mama yangu alivyokuwa anapata tabu ya kututimizia mahitaji yetu. Kwa kweli ilikuwa ngumu sana hata nashindwa kuelezea, mama yetu alipata shida sana,” alimalizia hivyo.

Kauli ya Haule ilinifaya niwaze zaidi, nikajisemea moyoni kuwa huenda mzazi huyo alikuwa akikumbwa na huzuni ambayo ilikuwa akiwaathiri watoto wake kisaikolojia.

Tukumbuke kuwa mara nyingi watoto huwa na tabia ya kufanya na kutii wanachokiona kutoka kwa wazazi au mzazi wake, hivyo, tabia ya mzazi wake huyo inaweza ikamdhuru.

Hapa namaanisha kuwa malezi ambayo mzazi mmoja ndiye mwenye kubeba majukumu ya kumlea na kumkuza mtoto au watoto na mzazi huyu anakuwa ndiye mtoa huduma kwa kiasi kikubwa na mara nyingi anakuwa haishi na mzazi mwenzake kwa sababu tofauti, huleta madhara makubwa kwa watoto.

Takwimu za sasa ulimwenguni zinaonesha ongezeko kubwa la watoto wanaolelewa na kukuzwa na mzazi mmoja, inaongezeka kila kukicha.

Na malezi haya yanaonekana kuwa utamaduni wa kawaida sana hivi sasa kwa jamii nyingi duniani.

Hivyo, kwa jicho lingine, inaweza kuonekana ni sawa, lakini wataalamu wa malezi na makuzi ya mtoto wanatuambia kuwa ina madhara makubwa na matokeo makubwa katika jamii ya kesho.

Unaweza kukuta mmoja wa wanandoa akajikuta anawalea na kuwakuza watoto peke yake bila sababu ya msingi, licha ya kuwa mzazi mwenzake yupo.

Ingawa wapo wale ambao hujikuta wakizidiwa na majukumu na mmoja akawa anaishi mbali na familia yake kwa muda mrefu na kurejea mara mojamoja kuungana nao.

Hapo ndipo mzazi mmoja hujikuta analazimika kufanya majukumu yote ya baba na mama kwa mtoto au watoto kwa kipindi kirefu cha kutokuwepo kwa mzazi mwingine.

Wako wazazi wengi wa aina hii wanaojitahidi kwa kila hali kujaribu kuchukuliana na kuyaweza majukumu ya kikazi na kifamilia.

Kwa upande mmoja mzazi huyu anayemlea mtoto au watoto peke yake anabanwa na majukumu ya kazini ambayo ndiyo yanampa mkate wake na watoto na kwa upande mwingine, majukumu ya kifamilia yanamsubiri na wakati huo hana msaada katika hayo yote.

Kuwa mzazi mmoja inasumbua sana nyakati nyingine na wakati huo huo hujui namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo unaotokana na hali hiyo.

Ndiyo maana Haule pale juu amesema alikuwa akimuonea huruma mama yake na hawezi kuelezea zaidi, kwa sababu anajaribu kuvaa viatu vya mama yake.

Hivyo ni wazi kuwa athari hizi haziishii kwa mzazi tu, bali pia zinakwenda hadi kwa watoto. Hakuna mtoto anayetamani kukuzwa au kulelewa na mzazi mmoja, ni mazingira tu yanayolazimisha hali hiyo.

Kwa kiasi kikubwa uelewa wa hali hizi na yale yatokanayo na hali hii, inaweza kuwasaidia wale ambao wanaweza kujikuta wanaingia katika malezi ya mzazi mmoja au hata wale ambao tayari wako katika maisha ya namna hii.

Baadhi ya mambo ya kujifunza katika hili ni kwamba, licha malezi ya mzazi mmoja wakati mwingine haiepukiki, lakini bado yapo mazingira ambayo wengine wanaamua kuwalea peke yao kwa makusudi mazima, yaani mtu anadhamiria licha ya kufahamu kuwa kuna changamoto lukuki, anaamua kuwa hivyo. Ila ukifuata misingi ya malezi bora, haipaswi kuwa hivyo.

Yapo mambo mazuri pia ambayo mtu anaweza kujifunza kutokana na kuwa mlezi pekee.

Mara nyingine mzazi anayelea na kukuza mtoto au watoto peke yake anaweza kuzigundua jitihada zake na uwezo alionao ambao asingeweza kuufahamu kama wangekuwa wazazi wawili.

Wengi wamejikuta wanao uwezo wa kujituma zaidi na kufanya zaidi pasipo kuwa tegemezi, tofauti na wanapokuwa na mzazi mwingine. Wengine wamejifunza kuwa furaha ya kweli haitokani na mtu mwingine, bali inachochewa na mtu mwenyewe kutokea ndani yake yeye mwenyewe.

Nafahamu ukweli kwamba kulea mtoto au watoto peke yako sio kazi rahisi, lakini pia upo ukweli kwamba ziko baadhi ya faida kama utakubaliana na changamoto hizi na kuchukuliana nazo kwa mtazamo chanya.

Lakini zipo changamoto nyingi sana zinazowakabili walea peke na mojawapo kubwa inayowakabili wazazi wengi ni jitihada za kuhakikisha wanajikimu maisha yao na ya watoto wao ya kila siku kifedha.

Mara nyingi wazazi wa aina hii wanalazimika kuishi kwa kutegemea chanzo kimoja cha mapato, tofauti na familia nyingine ambazo wazazi wote wawili wanafanya kazi na wanaingiza kipato.

Kama inatokea wazazi hawa wanatengana, basi mzazi anayebaki na watoto analazimika kuhakikisha anayashuhulikia masuala yanayohusu watoto na mahusiano yao na mzazi wao anayeondoka, hapa kunakuwa na mambo kama kuhakikisha kuna mpango wa watoto au mtoto kumtembelea mzazi mwingine, analala au kushinda naye mara ngapi, fedha na huduma za mtoto zinakuwaje na zinafika vipi kwa mzazi mwenye mtoto au watoto.

Mambo haya yote sio madogo, yana changamoto zake na msongo mkubwa wa mawazo.

Binafsi huwa nasema wana heri wale wanaoweza kusuluhisha tofauti zao bila misuguano mikubwa, maana hii inafanya hali kuwa ya amani na maelewano sio tu kwa wazazi, bali na kwa watoto pia.

Pamoja na hayo yote, changamoto hizi zinaweza pia kuwapa fursa za kujifunza na kuendelea vema.