Tunawaongozaje watoto kuchagua tahasusi kidato cha tano?

Baada ya shamra shamra za kufaulu mitihani ya kidato cha nne mwaka jana, wiki mbili hizi mwezi huu kila mzazi alikuwa anahaha kutafuta namna ya kuhakikisha kijana wake anapata fursa ya kuendelea na ngazi inayofuata ya masomo.
Katika mfumo wa elimu nchini Tanzania, hatua ya kuchagua tahasusi kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne ni muhimu sana. Serikali hutoa siku 21 kwa wanafunzi kubadili tahasusi zao na baada ya muda huo huwa hakuna nafasi nyingine.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Charles Msonde, aliwahi kunukuliwa akisema dirisha la mabadiliko lingeanza Aprili 6, 2023.
Hii inaonyesha umuhimu wa mwongozo na ushauri wa kina kwa wanafunzi wakati wa kuchagua tahasusi zao.
Wanafunzi wanahitaji kuelewa uwezo wao, vipaji, na matamanio yao kabla ya kufanya uamuzi wa tahasusi.
Dk John Dewey anasema, "Elimu inapaswa kuwa mchakato wa kuwapa wanafunzi zana za kufikiri na kuchagua."
Kwa waliofaulu kwenda vyuo vya ufundi huenda a hawana bugudha zihusuzo uchaguzi wa tahasusi kwani uchaguzi wa fani huwa unaeleweka na mwanafunzi hujua kwa vitendo kozi gani anapaswa aisomee.
Hali ni tofauti kwa vijana wa kidato cha tano, ambao hukumbwa na tatizo la uchaguzi wa masomo ya kwenda nayo hadi chuo kikuu.
Nasema ni changamoto kwa kuwa wanafunzi wengi waliofaulu kidato cha nne na kujikuta kila tahasusi imekubal, mara zote hukumbwa na mkanganyiko wa kuchagua ni masomo gani yawapeleke mbele, huku mihemko ya kuigana katika makundi rika ikishika kasi baina yao.
Kwa baadhi ya familia ambazo wazazi hawakubahatika kwenda shule, wanafunzi hujikuta katika wakati mgumu na kupata mkanganyiko.
Ikumbukwe kuwa misingi ya elimu imebadilika tofauti na zamani, kwani miaka ya 1990 ilikuwa ni vigumu kwa mwanafunzi aliyefeli hisabati kuparamia masomo ya sayansi.
Hivi sasa si ajabu kukuta mwanafunzi mwenye F ama daraja D katika hisabati anapata mwanya wa kusomea kemia, biolojia na jiografia (CBG) na wengi hufaulu vizuri kidato cha sita, huku misingi ya hisabati ikizidi kuwekwa kando.
Mwanafunzi anaporuhusiwa kubadili tahasusi akiwa shuleni tayari inahitaji nguvu ya ziada, kwani walio wengi huingia mtego kwa kujitosa kwenye masomo ambayo hawana uwezo wa kuyamudu siku za usoni.
Baadhi ya shule za binafsi walimu huwapigia simu wazazi na kushauriana na mtoto ni tahasusi ipi anapaswa kuisomea na mzazi hutakiwa kuandika barua ya kukiri kushiriki katika maamuzi aliyofanya kijana huyo. Mbinu hii ni nzuri kwani huondoa mkanganyiko na lawama baina ya walimu na wazazi wa wanafunzi.
Katika nchi zilizoendelea kama Finland, mifumo ya elimu inatilia mkazo ushauri na mwongozo kwa wanafunzi tangu wakiwa wadogo.
Finland ina walimu maalum wa mwongozo ambao hufanya kazi bega kwa bega na wanafunzi kuwasaidia kuelewa uwezo na vipaji vyao.
Wazazi na walezi wana nafasi kubwa katika kusaidia watoto wao kuchagua tahasusi zinazofaa.
Wazazi wanapaswa kushirikiana na walimu na washauri wa elimu ili kuhakikisha watoto wao wanachagua tahasusi zinazowafaa.
Katika mfumo wa elimu wa Uingereza, wazazi wanashirikishwa kikamilifu katika mchakato wa kuchagua masomo na shule za watoto wao.
Wanahudhuria mikutano ya ushauri na walimu na kupata taarifa kamili kuhusu maendeleo na vipaji vya watoto wao.
Profesa Linda Darling-Hammond, mtaalamu wa elimu nchini Marekani, anasisitiza umuhimu wa walimu kuwa na ujuzi na uelewa wa kutosha ili kuwaongoza wanafunzi.
"Walimu wanapaswa kuwa na uwezo wa kutambua vipaji vya wanafunzi na kuwasaidia kuvikuza," anasema.
Zaidi ya wazazi na walimu, ni muhimu kuwashirikisha wataalamu wa nje kama wanasaikolojia wa elimu na wataalamu wa ajira.
Hawa wataalamu wanaweza kutoa mwongozo wa kitaalamu kuhusu soko la ajira na mahitaji yake, hivyo kuwasaidia wanafunzi kufanya uamuzi bora zaidi kuhusu tahasusi zao.
Nchini Marekani, wanafunzi wanapata fursa ya kushauriana na wataalamu wa ajira na kuhudhuria warsha za mwongozo wa kitaaluma.
Ifahamike kuwa mchakato wa kuchagua tahasusi ni zaidi ya kuchagua masomo; ni kuchagua mustakabali wa mtoto. Ni muhimu kuhakikisha wanafunzi wanapewa mwongozo na ushauri wa kutosha ili kufanya maamuzi sahihi.
Katika nchi zilizoendelea, watoto wanapewa fursa ya kukuza vipaji vyao tangu wakiwa wadogo. Mifumo ya elimu kama ile ya Singapore, imeweka mkazo katika kutoa elimu inayolenga kumsaidia mwanafunzi kutambua na kukuza vipaji vyake.
Mwongozo na ushauri kwa wanafunzi ni muhimu sana kwa sababu inawasaidia kufanya maamuzi sahihi na kufikia ndoto zao.
Wazazi, walimu, na wataalamu wa elimu wanapaswa kushirikiana ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mwongozo wa kutosha.
Kama alivyosema Dk Msonde, "Wanafunzi ambao hawatapata muda wa kufanya marekebisho, taarifa zitakazotumika ni zile walizojaza wakiwa shuleni." Hii inaonyesha kuwa ushauri wa mapema ni muhimu ili kuepuka makosa ya baadaye.
Hivyo, mchakato wa kuchagua tahasusi ni muhimu sana kwa wanafunzi na unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wanafunzi, wazazi, walimu, na wataalamu wa elimu. Kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mwongozo wa kutosha, tunaweza kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi na kufikia ndoto zao.
Mfumo wa elimu unapaswa kuwa jumuishi na kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wote ili waweze kufikia malengo yao na kuwa na mustakabali mzuri.