Mchengerwa: Tumejipanga utekelezaji wa tahasusi mpya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa akizungumza katika ofisi za Mwananchi Communications Ltd leo Machi 21, 2023

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema Watanzania hawapaswi kuwa na hofu juu ya utekelezaji wake, kwani maandalizi  yamekwishafanyika na walimu 11,000 wapya wataajiriwa.

Dar es Salaam. Wakati wadau wa elimu wakihoji utayari wa Serikali kuwahudumia wanafunzi watakaochagua tahasusi 65, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema wamejipanga kibajeti, walimu na miundombinu.

Amesema Watanzania hawapaswi kuwa na hofu juu ya utekelezaji wake, kwani maandalizi  yamekwishafanyika na walimu 11,000 wapya wataajiriwa.

Ametoa maelezo hayo siku moja  tangu alipotangaza tahasusi mpya 49 za masomo mbalimbali. Awali kulikuwa na tahasusi 16.

Tahasusi hizo zimetengwa kwenye makundi saba na zitaanza kutumika Julai mwaka huu. Makundi hayo ni sayansi ya jamii, lugha, masomo ya biashara, tahasusi za sayansi, michezo, sanaa na elimu ya dini.

Juzi, Mchengerwa ametaja sababu ya kuanzishwa kwa tahasusi hizo, kuwa ni utekelezaji wa mabadiliko ya sera ya elimu ya mafunzo ya mwaka 2024 toleo la 2023 na mitalaa ya elimu ya kidato cha tano.

Mara baada ya kuzitangaza tahasusi hizo, kuliibuka mijadala mbalimbali kutoka kwa wadau. Wapo waliopongeza wakisema zinafungua fursa kwa wanafunzi kuwa na mawanda ya kuchagua tahahasusi na wengine wakihoji utayari wa Serikali.


Maandalizi utekelezaji

Katikati ya hoja hizo za wadau, Waziri Mchengerwa akizungumza na Mwananchi Digital kwenye mahojiano maalumu leo Machi 21 2024, amesema Watanzania hawapaswi kuwa na hofu juu ya utekelezaji wa tahasusi hizo, akisema: “...katika hili, Serikali imejipanga vizuri na wala haijakurupuka.”

Waziri Mchengerwa aliyetembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini, Dar es Salaam, ameongeza:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa akizungumza na  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu (aliyevaa miwani) na Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi  Communications Ltd ,Victor Mushi baada ya mazungumzo  alipotembelea ofisi za MCL Tabata Relini jijini Dar es Salaam leo Machi 21, 2024.

“Sisi Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu tumeshajipanga vizuri kuhakikisha tunao watalaamu wa kutosha kuhakikisha tunatibu tatizo hilo.’’

Miongoni mwa mikakati aliyotaja ni kuajiri walimu 11,000 ifikapo Aprili mwaka huu watakaokwenda kupunguza upungufu wa walimu.

Mchengerwa: Tumejipanga utekelezaji wa tahasusi mpya

“Mheshimiwa Rais ameshatoa vibali vya ajira takribani walimu 11,000 tunaokwenda kuajiri kuanzia mwezi unaokuja, watakaokwenda ‘kufiti’ kwenye maeneo ambayo kuna uhaba wa walimu katika baadhi ya tahasusi nilizozungumza hapo awali,” amesema.

Kuhusu bajeti, waziri huyo amesema Serikali tayari imejipanga na imefanya mazungumzo na Benki ya Dunia (WB) walioahidi kusaidia.

“Sasa huwezi kusaidiwa kama hujaonesha eneo unalotaka kusaidiwa na katika hili, kama mnavyojua tumeanzisha madarasa mtandao,”amesema.

Waziri Mchengerwa ametaja matumizi ya teknolojia ya digitali katika kufundisha ili kukabiliana na upungufu wa walimu,  akisema mwalimu mmoja anaweza kufundisha nchi nzima ikiwa tutakuwa tumefunga madarasa mtandao.

“Mwalimu mmoja anaweza kufundisha shule zaidi ya 100, 200 au hata 500. Eneo hili tumeshaweka mikakati kwa kuwataka wakurugenzi wa halmashauri katika maeneo yao kuweka katika bajeti.

“Moja ya mikakati ni kuhakikisha kunakuwa na vifaa vya kidigitali katika shule zetu na tumekubaliana kila halmashauri ihakikishe inakuwa na shule moja kwa kuanzia, ambapo mwalimu mmoja anaweza kukaa pale Kibaha (Mkoa wa Pwani) au akakaa Dodoma shule zote nchi nzima akazifundisha,” amesema.

Amesema tayari majaribio yamefanyika na yamekwenda vizuri na kupitia njia hiyo hata wanafunzi wa maeneo mbalimbali wanaokuwa wameunganishwa kwenye mfumo wanaonana.

Alitaja pia mpango wa elimu kwa njia ya mafunzo (internship program) utakaowezesha wanafunzi kupata ujuzi na uzoefu.

“Kwa hiyo wanafunzi wanaomaliza masomo yao katika vyuo mbalimbali, stashahada na astashahada maana yake anakwenda kuanza ajira ya Serikali kutakuwa na mafunzo ya vitendo, kwa hiyo kutakuwa na mamilioni ya walimu,” amesema.


Ajibu mjadala tahasusi za dini

Kuhusu tahasusi za dini ambazo baadhi ya wadau wamekuwa wakihoji kuanzishwa kwake kunaweza kuwa na lengo la kuingilia dini za watu, waziri huyo alisema si kweli na zimeanzishwa baada ya kupata maoni yao.

“Mwanafunzi anapotoka hapo sio tu anakwenda kuwa padri, elimu ya upadri bado utahitaji kwenda kuipata katika maeneo yaliyoandaliwa. Huko ni kuwatengeneza Watanzania katika maeneo waliyosomea na huko ni kuwajenga katika uadilifu.

Kwa hiyo ninachoweza kusema, hizi tahasusi zimetokana na maono ya Watanzania wenyewe walioshirikishwa na sisi kama Serikali tumejipanga kusimamia utekelezaji wake,” amesema Waziri Mchengerwa.

Amesema kuanzishwa kwa tahasusi hizo ni fursa kwa wanafunzi kuwa na mawanda mapana ya kuchagua tahasusi wazipendazo, kwani kuna tahasusi za michezo, sanaa na hii itawafanya wachague wakipendacho.


Mitazamo ya wadau

Wakizungumza leo na Mwananchi Digital baadhi ya wadau wa elimu wakiwamo viongozi wa dini wamehoji uharaka wa Serikali katika kuongeza tahasusi na kwamba wazazi hawakushirikishwa.

Wamesema kabla ya kutangazwa kwa tahasusi hizo, wanafunzi na wazazi wangepewa elimu, kwani upo uwezekano wa mwanafunzi kusoma tahasusi zilizoletwa sasa akakosa pa kuelekea baada ya kuhitimu.

Mwandishi wa vitabu, Richard Mabala amesema mabadiliko makubwa yanayofanyika kwa kiasi hicho yanaibua maswali ni namna gani maandalizi yamefanyika.

“Naona mwitikio wa wananchi umekuwa hasi, wapo wachache waliopongeza sasa kwangu naona maandalizi hayajafanyika vya kutosha na kwenye maandalizi hayo walimu wapo, vitabu vipo?”

“Taasisi ya Elimu Tanzania tayari ina kazi kubwa ya kuandika vitabu vya sekondari na shule ya msingi kulingana na mitalaa mipya sasa wataweza kuandika vitabu vyote, sasa ni kwa nini hatujachukua muda kufanya maandalizi tuna uharaka gani?” amehoji.

Amesema maandalizi yaliyopaswa kufanyika ni kuwashirikisha walimu, wanafunzi na wazazi juu ya tahasusi hizo na baadaye kutoka kuiambia jamii juu ya mabadiliko yaliyofanyika.

Hata hivyo, gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk Aneth Komba kujua maandalizi vitabu ambapo alijibu kwa ujumbe mfupi wa maandishi akisema: “Ndio tunakamilisha.”

Mdau mwingine, Alistidia Kamugisha alisema maboresho hayo yanaakisi kiu ya mabadiliko waliyokuwa nayo Watanzania wengi.

Amesema mabadiliko yaliyofanyika eneo la sanaa lengo ni kuwezesha wasomi waliopo nchi wawe na uwezo wa kutoka nje ya nchi na kuwasiliana kwa ufasaha.

“Mtu anapojifunza lugha mbalimbali anapokuwa nje ya nchi anaweza kuwasiliana na kuwa na ujasiri, unyong’onyevu unatokana na mtu kushindwa kuwasiliana hasa anapohudhuria mikutano ya kimataifa hivyo kwa upande wa kumuuza mhitimu wa Tanzania ni jambo zuri,’’ amesema.


Walichokisema viongozi wa dini

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Alhaj Nuhu Mruma amesema kupewa uzito masomo ya dini kwenye sekta elimu yalikuwa malengo yao ya muda mrefu.

“Tulitaka muda mrefu masomo ya dini yawe miongoni mwa masomo yanayotahiniwa na kutunukiwa katika mitihani ya mwisho, sasa wameipa uzito kilio chetu somo la dini linatusaidia kutengeneza maadili ndio maana tuliomba liwe somo la lazima kwa wanafunzi wa sekondari na msingi,” amesema.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima amesema:

“Ninachoona katika hizi tahahusi,  kunapaswa kuangaliwa pia tunacholenga kama nchi katika kujenga umahiri wa wanafunzi kwenye uelewa wa kisayansi waweze kuchangamana na mazingira ya nchi na dunia lakini atakwenda kusoma nini baada ya hapo.”

Miongoni mwa tahasusi za kidini ambazo wanafunzi wataweza kusoma kutokana na machaguo yao ni Islamic, Historia Jiogorafia (IHG), Somo la Dini la Wakristo, Historia na Jiogorafia (DHG).