TUONGEE KIUME: Hizi M tano kila mwanamume anazihitaji

Mtu mmoja aliniambia, kila mwanamume anahitaji 'M' tano katika maisha ili atoshe kuitwa mwanamume. Nilipomuuliza ni zipi hizo, akaniambia:

Kwanza, anahitaji Mind (akili) iliyotulia, inayofanya kazi sawasawa, atakayoitumia kufanya uamuzi.

Utake usitake, asilimia 70 ya maisha yako kama mwanamume yanatawaliwa na kufanya uamuzi muhimu kuanzia madogo mpaka makubwa, kwa hiyo kama kichwa chako hakifanyi kazi vizuri uanaume utakushinda tu.

Utatakiwa kuamua kuanzia mtoto anakwenda kusoma shule gani mpaka jinsi unavyoweza kujigawa kwa ajili ya ofisi na familia.

Na uzito ni kwamba uamuzi wote unaofanywa na mwanamume haumgusi yeye pekee, bali watu wote walio nyuma yake, wategemezi wake.

Pili, mwanamume anahitaji Money (pesa), kwenye hili hakuna hata haja ya kuongea sana, kama wewe ni mwanamume na siku moja ilitokea ukakosa fedha ya kutosha kumudu maisha yako ya kawaida bila shaka una uzoefu wa nini kilitokea mbeleni.

Na tunaposema fedha hatumaanishi wote tuwe nazo kama za Bakhresa, hapana na haiwezekani, tunamaanisha ya kumudu maisha yako ya kawaida ya kila siku na uwezo wa kuhudumia familia kwa kiwango chako. Na ukiona somo la umuhimu wa mwanamume kuwa na fedha hulielewi, waulize wanaume wenzio yaliyowakuta baada ya kukosa za kuhudumia familia zao.

M ya tatu ni Material (vitu), unatakiwa uwe na ardhi, uwe na nyumba, uwe na mali zitakazowasaidia wategemezi wako siku ukiwa mbali na dunia.

M ya nne ni Men (wanaume), ukiwa mwanamume asilimia 70 ya watu unaochangamana nao ni wanaume.

Baa tunakunywa na wanaume, maofisini kwetu kuna idadi kubwa zaidi ya wanaume, kwa hiyo ni wazi kwamba mwanamume unahitaji mtandao wa wanaume wenzio ambao kwa pamoja mnajengana, mnakuzana na kushikana mikono.

Kama somo hili ni gumu kuelewa, fuatilia ujue mitandao ya wanaume wengi waliofanikiwa ikoje.

M ya mwisho ni Muscles (misuli), kwa maana ya kwamba kuwa na afya njema. Kwa dunia tunayoishi sasa, unene kupitia kiasi ni dalili ya kutokuwa na afya njema, haya ni maneno ya madaktari, sio mimi, labda kama tuamue kuwa wabishi tu.

Na kwa mantiki hiyo ili ufanye mambo yako vizuri, mwanamume unahitaji kuwa na afya njema.

Siyo uwe na misuli kama mlinzi wa ‘night club,’ hapana, bali kuwa na afya, kujilinda na magonjwa unayoweza kujilinda nayo na kadhalika.

Pointi hapa sio lazima uwe na vyote kwa wakati huu, hapana, bali unahitaji M ya kwanza ambayo ni Mind (akili). Ukiwa na akili inayofanya kazi utajijenga kupata yote mengine yanayohitajika.