Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tuwachague viongozi wenye uwezo, kwa maslahi ya Taifa

Wananchi wakiwa katika foleni ya kupiga kura. Picha na Maktaba

Mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025 hapa nchini umeanza, huku vyama vya siasa vikiendelea kutoa fomu kwa wanachama wao wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, zikiwemo ubunge na udiwani.

Ni katika kipindi hiki ambapo kila kada ya jamii, wafanyabiashara, wasanii, madereva, waimbaji, DJ, wanaharakati, na makada wa chama wanajitokeza kuwania nafasi hizi muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Hali hii ni kiashiria cha demokrasia inayochipuka ambapo kila Mtanzania ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa. Hata hivyo, uhuru huu unapaswa kuambatana na tafakari ya kina kuhusu aina ya viongozi tunaowachagua.

Tunapaswa kufahamu kuwa wajibu wa Mbunge na Diwani ni zaidi ya Umaarufu. Kazi kuu ya Bunge ni kutunga sheria, kuisimamia Serikali na kuwakilisha wananchi.

Hii ni kazi muhimu inayohitaji mtu mwenye uelewa, si tu wa sheria, bali pia wa masuala ya kiuchumi, kijamii na kimazingira yanayowakabili wapiga kura wake.

Viongozi wanaoingia katika vyombo hivi vya maamuzi wanapaswa kuwa na uwezo wa kusoma na kuchambua miswada, kushiriki mijadala ya kisera kwa hoja nzito, na kutoa maamuzi yanayozingatia maslahi mapana ya nchi.

Kwa msingi huu, ni muhimu sana kwa wananchi kuangalia sifa za kiongozi zaidi ya jina lake, umaarufu wake au ukaribu wake na chama.

Mbunge au Diwani anayechaguliwa si kwa sababu ya uwezo bali kwa sababu ya ukada au jina maarufu, anaweza kuishia kuwa bubu bungeni au kwenye baraza, akikubali kila kinachosemwa bila kuchangia kwa hoja.

Hii ni hatari kwa maendeleo ya taifa, kwani sheria na maamuzi yanayopitishwa yanaathiri maisha ya wananchi wote.

Ingawa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka mgombea wa ubunge awe na uwezo wa kusoma na kuandika tu, kwa hali ya sasa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia tunahitaji zaidi ya hapo.

Tunahitaji wabunge wenye uwezo wa kuelewa kwa undani tafsiri ya sheria, madhara ya maamuzi ya kisera, na jinsi ya kuibua hoja zenye mashiko.

Hili haimaanishi kuwa darasa la saba hawezi kuwa kiongozi bora, bali ni vema kuhakikisha kuwa wanaogombea nafasi hizi wanapewa angalau mafunzo mafupi ya sheria na majukumu yao kabla ya kupewa ridhaa ya wananchi.

Mafunzo haya yanaweza kusaidia kuwaandaa vyema kwa nafasi wanazozitaka. Wengine wamekuwa vinyonga wa kisiasa, wakichagua kupitisha kila jambo linalotolewa na chama hata kama linaumiza wananchi waliowachagua.

Wananchi wanapaswa kukumbuka kuwa kura yao ni silaha ya mabadiliko. Chagua mbunge au diwani ambaye ataweka mbele maslahi ya jamii kuliko ya chama chake au maslahi yake binafsi. Wananchi wanapaswa kuchagua mtu anayeweza kuuliza maswali magumu, kutoa hoja, na kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma.

Uchaguzi si harusi, ni mkataba wa miaka mitano kati ya mwananchi na kiongozi wake. Uamuzi wa kumpa mtu ambaye hana uwezo lakini anakupa tisheti, kitenge au pesa kidogo ni sawa na kuuza maisha yako ya baadaye kwa faida ya muda mfupi. Mfanyabiashara anaweza kuwa diwani au mbunge bora iwapo ataelewa majukumu yake na akawa na mtazamo wa kusaidia jamii.

Vivyo hivyo kwa msanii au dereva. Lakini pale kada hawa wanapochukulia nafasi hizi kama fursa za kujinufaisha badala ya kuhudumia wananchi, basi tunakuwa tumefeli kama taifa.

Hapa ndipo mafunzo ya kisheria na uongozi yanapopaswa kupewa kipaumbele kabla ya mtu kuingia katika siasa.

Wananchi wanapaswa kutambua kuwa uchaguzi si mashindano ya mavazi ya kijani, njano au nyekundu.

Si mashindano ya kelele kwenye kampeni. Uchaguzi ni mchakato wa kuchagua mtu anayekuja kusimamia maisha yao kwa miaka mitano.

Tuchague watu wenye dira, si maneno. Wenye mipango, si nderemo. Tuchague wawakilishi wetu kwa akili, si kwa mihemko ya kisiasa.

Katika mchakato huu wa uchaguzi mkuu, kila Mtanzania anapaswa kujitafakari. Je, kiongozi ninayemchagua ana uwezo wa kutunga sheria bora?

Anaweza kuibua hoja bungeni au kwenye baraza la madiwani? Ana ujasiri wa kuhoji matumizi ya bajeti na kushinikiza maendeleo ya jimbo au kata yake?

Kama jibu ni hapana, basi huyo si chaguo sahihi. Tujifunze kusema hapana kwa kiongozi asiyefaa, bila kujali chama chake au zawadi alizotupa.

Huu ni wakati wa kuamka na kulinda maslahi ya taifa letu, kwa kuchagua wabunge na madiwani wenye uwezo, maono na uzalendo. Taifa bora linajengwa na maamuzi bora ya wananchi.