Prime
Tuwahukumu wagombea kwa mema na mazuri na si kwa mabaya pekee
Uchaguzi ni wakati ambapo viongozi huletwa hukumuni mbele ya umma. Katika mchakato huu, kauli na mitazamo vina nafasi kubwa.
Moja ya changamoto kubwa nchini mwetu ni mitazamo tuliyojiwekea, hasa ule mtazamo hasi (negative attitude) unaotufanya tuone matatizo kuliko fursa. Mitazamo chanya (positive outlook) hujenga matumaini na mwelekeo wa maendeleo, ilhali mitazamo hasi huzuia ustawi wa taifa.
Tanzania ni nchi tajiri sana. Tuna rasilimali watu, ardhi yenye rutuba, siasa safi, na uongozi ulio na misingi ya kikatiba. Tuna madini ya aina mbalimbali, maliasili, vivutio vya utalii, vyanzo vya maji na gesi asilia.
Tuna pia chuma cha kutosha katika Liganga na Mchuchuma. Kwa utajiri huu, hakuna sababu ya kujiita maskini. Tatizo ni kwamba tunapojinenea umasikini, tunajenga hali hiyo kiakili na kiutendaji.
Ni lazima tubadili mitazamo yetu na kuanza kutumia kauli chanya ili kuunda jamii na taifa lenye mtazamo wa matumaini.
Tunapojiandaa kwa uchaguzi, tuwapime wagombea kwa kuangalia mema na mafanikio yao badala ya kusimama katika mabaya na mapungufu pekee.
Mfano rahisi ni glasi yenye maji nusu; mmoja ataona imejaa nusu (mtazamo chanya) na mwingine ataona imepungua nusu (mtazamo hasi). Wote wako sahihi, lakini tafsiri ya kwanza hujenga, ya pili hubomoa.
Mfano wa kuangalia mazuri tunaweza kuupata katika utendaji wa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita.
Serikali imeweka msingi wa mageuzi ya kisiasa na demokrasia kwa kuruhusu mikutano ya hadhara, kubadili sheria ya uchaguzi na kuanzisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania.
Ni kweli kwamba mabadiliko haya yamefanyika bila kwanza kufanya marekebisho ya Katiba mama ili kuitambua Tume Huru, jambo ambalo lingekuwa sahihi kisheria.
Hata hivyo, nia njema na dhamira ya Rais Samia ni wazi, na mafanikio ya kuanzisha INEC yanapaswa kuangaliwa kama hatua chanya.
Akilihutubia Bunge la 12 jijini Dodoma, Rais Samia alisema hatua hizi ni sehemu ya falsafa yake ya R4 inayotafasiri mageuzi, maridhiano, ustahimilivu na ujenzi mpya wa taifa.
Lengo ni kuondoa misuguano ya kisiasa ili taifa liungane katika ajenda ya maendeleo. Hatua ya kuondoa zuio la mikutano ya hadhara na kuboresha sheria muhimu kama Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Sheria ya Vyama vya Siasa, imetimiza kilio cha muda mrefu cha vyama vya siasa na asasi za kiraia kuhusu usawa wa kisiasa.
Ni kweli kwamba sheria hizi mpya zimejengwa juu ya misingi ya kikatiba iliyopo, ambayo wengine huona ina upungufu. Lakini kwa kuwa serikali imekuta mfumo huo ukitumika kwa muda mrefu, tusimlaumu Rais kwa urithi huo, bali tumpongeze kwa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya. Hii ni ahadi muhimu katika Ilani ya CCM kwa mwaka 2025–2030.
Rais pia ameeleza kwamba Tume ya Uchaguzi inapaswa kuwalazimisha wagombea na vyama kuwasilisha ilani za uchaguzi, lengo ni kwa wananchi waweze kuwapima kwa sera na mipango.
Kuhusu ruzuku, Serikali imetoa Sh87.8 bilioni hadi Juni 2025 kwa vyama vinavyostahili na Baraza la Vyama vya Siasa limefanya mikutano sita iliyozalisha mapendekezo yaliyofanyiwa kazi na serikali.
“Kila hatua tuliyochukua imekuwa ya mashauriano,” amesema Rais Samia, akisisitiza kwamba uchaguzi uendeshwe kwa uhuru, haki, amani na ushirikishwaji wa wadau wote. Dhamira ni kuhakikisha mageuzi haya yanakuwa ya kudumu, kulinda maridhiano ya kitaifa na kulinda demokrasia kwa vizazi vijavyo.
Pamoja na mafanikio haya, changamoto bado zipo, ikiwamo kuibuka tena kwa tatizo la “wasiojulikana.” Wapo wanaodhani hawa wanahusishwa na mamlaka fulani.
Ni jukumu la serikali, kupitia vyombo vya ulinzi na usalama, kuhakikisha vitendo hivi vinakomeshwa ili visiwe doa katika safari ya uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Kwa msingi huo, tunapaswa kuwahukumu wagombea na vyama kwa mema na mazuri waliyofanikisha, huku tukitafuta suluhu za changamoto zilizopo, badala ya kutumia upungufu wao kama kipimo pekee cha uamuzi. Uchaguzi si tu hukumu ya adhabu, bali pia ni nafasi ya kuthamini na kuendeleza mazuri yaliyopatikana.
Mungu ibariki Tanzania.