Ubabe unaoelezwa TRA ufanyiwe kazi

Muktasari:
Waziri Mpango alisema hayo wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau hao na Mawaziri wa Fedha na Mipango na Waziri wa Viwanda na Biashara, kwamba kukusanya kodi kusiwe kama vile watu wapo kwenye misitu ya Congo kwa kila siku iwe kazi ya kukimbizana.
Gazeti hili toleo la jana lilikuwa na habari iliyomnukuu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akimtaka Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutafuta njia rafiki za kukusanya kodi kutoka kwa wadau wa sekta binafsi.
Waziri Mpango alisema hayo wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau hao na Mawaziri wa Fedha na Mipango na Waziri wa Viwanda na Biashara, kwamba kukusanya kodi kusiwe kama vile watu wapo kwenye misitu ya Congo kwa kila siku iwe kazi ya kukimbizana.
Kauli ya Waziri Mpango ambaye kwa kipindi kifupi aliwahi kukaimu nafasi ya Kamishna Mkuu wa TRA, ilikuwa mwiba kwa mamlaka hiyo, lakini mwanga wenye matumaini kwa wafanyabiashara.
Tunaamini kauli yake kwamba anatambua sekta binafsi ni ‘injini’ ya uchumi, hivyo wizara yake haipo tayari kuona sekta hiyo inarudi nyuma, ataisimamia kwa dhati.
Waziri Mpango hayuko pekee katika kuinyooshea kidole TRA, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisikitishwa na kitendo kilichofanywa na wahusika wa mamlaka hiyo cha kuwanyang’anya basi wachezaji wa timu ya Serengeti Boys aliokuwa amewaalika nyumbani kwake kwa ajili ya chakula cha jioni.
Makamu wa Rais aliwataka TRA wasitumie mabavu wanapodai kodi, kwani kitendo hicho kinaichonganisha Serikali na wananchi wake.
Pia, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe naye hakuwa nyuma katika hilo, kwanza alihimiza umuhimu wa kulipa kodi, lakini aliwataka TRA kutumia busara katika ukusanyaji wa kodi.
Tunaheshimu kazi inayofanywa na TRA katika kukusanya kodi ya Serikali kwa mujibu wa sheria, na tunafahamu kwamba maendeleo ya nchi na wananchi wake hayawezi kuwapo kama watu hawalipi kodi.
Pia, tunatambua kazi ya kukusanya kodi si nyepesi, lakini TRA yenyewe imeweka utaratibu wa namna ya kushirikiana na wateja wake.
Utaratibu huo unawaelekeza watendaji wa mamlaka hiyo kushirikiana na walipakodi na wadau wake kwa misingi ya kujali heshima, utu na kuwa na mtazamo wa kumjali mteja.
Pia, wafanyakazi wa mamlaka hiyo wanaelekezwa na kanuni zao kuonyesha heshima wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Tunahoji iwapo TRA imebadili taratibu zake za kuonyesha ushirikiano na heshima kwa wateja wake na sasa imeamua kutumia mabavu na ubabe wakati wa kudai kodi.
Wengi wanajiuliza TRA iliyoanza kufanya kazi Julai Mosi, 1996 kipindi chote hicho haikuwahi kusikika kutekeleza majukumu yake kwa mabavu, iweje sasa itumike nguvu kubwa wakati walipa kodi ni watu wenye uelewa na sheria zipo.
Kauli zilizotolewa na Makamu wa Rais, Waziri wa Habari na Waziri wa Fedha, ni dalili kwamba utendaji wa sasa wa TRA haujengi taswira nzuri kati ya mamlaka hiyo na mlipakodi.
Tunaamini kama alivyosema Waziri Mpango kwamba sekta binafsi ni injini ya uchumi, hivyo Tanzania ya viwanda tunayoitaka itafikiwa tu iwapo yale yaliyobainishwa na baadhi ya viongozi wa Serikali kuhusu TRA kama yatafanyiwa kazi.
Ubabe huchangia kupenya mbinu chafu ambazo zitaifanya mamlaka hiyo iwe na kazi ya ziada katika kupambana nazo.
Ni vema wahusika ndani ya mamlaka hiyo wakayafanyia kazi yanayozungumzwa na viongozi kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.