Uhusiano wa India na Tanzania ni wa kipekee

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akilakiwa na Watanzania mara baada ya kuwasili New Delhi nchini India kwa ajili ya kuanza rasmi ziara ya Kitaifa tarehe 08 Oktoba, 2023.

UHUSIANO baina ya Tanzania na India ni wa kihistoria na umedumu kwa muda mrefu kwa sababu msingi wake ni ushirikiano wenye faida kwa pande zote.

Ziara ya kitaifa ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini India inayofanyika kati ya Oktoba 8 hadi 11 mwaka huu, itapeleka uhusiano huo katika viwango vya juu zaidi – ukisimikwa na historia yetu ya nyuma, ujirani wetu kijiografia na mwelekeo wa kimkakati wa sera zetu za mambo ya nje.

Maingiliano yetu na India yalianza karne kadhaa zilizopita pale biashara baina ya wakazi na Waswahili wa Pwani ya Tanzania (Tanganyika na Zanzibar) na wenzao waishio kandoni mwa kingo za Mto Mandovi huko Gujarat India ilipoanza kurekodiwa rasmi.

Nyakati hizo za awali zilishuhudia kuwasili kwa wafanyabiashara kutoka India – hasa pwani ya Gujarat, kwenye pwani ya Zanzibar kwanza na baadaye Tanganyika. Wakisafiri kwa kutumia pepo za Monsoon, wafanyabiashara wa Asia na Ulaya waliotumia njia ya bahari walitumia upepo huo na mitumbwi kusafiri kufanya biashara kila mwaka.

Utambuzi wa pepo za Monsoon ulichochea sana biashara kupitia baharini. Ndiyo uliosababisha wafanyabiashara kutoka Afrika (ikiwemo Tanzania ya leo), Uajemi, India na Kusini Mashariki mwa Asia kuchangamana kibiashara.

Kwa nchi hizi mbili, mtandao wa biashara ulipoanza kukua, maingiliano hayo baina ya watu wa Pwani ya Tanzania na India yalizidi kuimarika. Matokeo yake yalikuwa kuimarika kwanza kwa uhusiano baina ya watu wenyewe na baadaye ikawa rahisi kwa serikali zetu kushirikiana.

Baada ya kufunguliwa rasmi kwa balozi katika nchi hizi mbili nchini Tanganyika na India kwenye miaka ya 1961 na 1962 mtawalia, uhusiano wote ukawa imara zaidi. Leo hii, Tanzania na India zinafurahia uhusiano mzuri kwa sababu ya hamu yetu ya kutaka kuwa bora zaidi kiuchumi, kisiasa, kitamaduni na kijamii. Huu ni uhusiano wa kidugu.

Mahusiano baina ya nchi hizi mbili yamejengwa kwenye msingi wa kuwa mtaaifa haya mawili yana maono yanayoshabihiana kwenye kuleta maendeleo kwa watu wetu, kupambana na changamoto za kila siku za kwenye kukuza uchumi na kubainisha njia za kibunifu zenye kusaidia nchi zetu kunawiri.

Katika muktadha huo, ni muhimu nikampongeza Rais Samia Suluhu Hassan, Mwanadiplomasia wetu namba moja, kwa uongozi wake uliosababisha marekebisho katika sera zetu za uwekezaji, kuimarika kwa mazingira wezeshi kibiashara, ukuzaji wa demokrasia na utawala bora na kujikita kwenye diplomasia ya uchumi.

Ziara hii ya Rais Samia nchini India itaupeleka uhusiano huu katika zama mpya ambapo serikali yake na ya mwenzake, Rais Droupadi Murmu na Waziri Mkuu, Narendra Modi, zitaingia kwenye zama za uhusiano unaojikita kwenye biashara na ukuaji wa uchumi wa nchi zetu.

Leo, India ni nchi ya nne kwa kufanya biashara kwa wingi na Tanzania. Biashara baina yetu inakadiriwa kuwa na thamani ya dola za Kimarekani bilioni 6.5 mwaka 2022/23 (kwa mujibu wa takwimu za India), na dola bilioni 3.1 kwa mwaka 2021/2022 (kwa mujibu wa takwimu za Tanzania) – kutoka dola bilioni 2.6. kwa mwaka 2017/2018.


Vile vile India ni kati ya vyanzo vitano vikubwa vya mitaji ya uwekezaji inayoingia Tanzania. Mwaka 2021/2022, jumla ya miradi ya uwekezaji 630 yenye thamani ya dola bilioni 3.7 ilisajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Zaidi ya ari hii ya kutaka kurejesha uhusiano baina yetu na India, sisi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, tumeshuhudia namna Rais Samia anavyopandisha hadhi ya taifa na utekelezwaji wa sera yetu ya mambo ya nje.

Tangu aingie madarakani, amebeba kwa dhati suala la kuifungua nchi yetu kwa ajili ya biashara na uhusiano wetu na nchi moja moja na jamii ya kimataifa kwa ujumla. Bila ya kutoka katika misingi ya Sera ya Mambo ya Nje, ameweka msukumo mpya katika maeneo mapya ya ushirikiano kwa kuitumia vema misingi ya mahusiano iliyojengwa tayari – na marafiki kama India wakiwa mstari wa mbele.

Tanzania na India sasa zinashirikiana katika maeneo ya kimkakati kama vile maji, afya, elimu, kilimo, tehama, uchumi wa buluu, uwekezaji na ukuzaji wa biashara baina yetu. Lengo letu ni kuvutia mitaji zaidi kutoka India kwa ajili ya kukuza uchumi wetu.

Tangu katika enzi za awali za biashara kupitia pepo za Monsoon, ambazo kwa hakika ni daraja lililo baharini, Tanzania na India zina uhusiano imara wa kiuchumi katika maeneo ya biashara na uwekezaji.

Kama waziri ninayehusika na mambo ya nje, najisikia fahari kuzungumzia kudumu kwa uhusiano wa kibiashara baina ya India na Tanzania. Uhusiano huu ni wa kipekee na ni matarajio yetu kuwa safari hii nzuri itaendelea.

Ni matumaini yangu makubwa kwamba safari hii itachagiza ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuona vikwazo vyote vinavyoizuia Tanzania isipae kiuchumi vinaondoka.

Mwandishi wa makala haya ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.