Unampa simu yako mpenzi wako? Shauri yako..

...Chukua simu yangu uangalie kanitumia sms kibao.

...Tangu mwaka jana nilipokuambia ananitumia ujumbe wa kunitaka hajaacha...si unaona hizi sms kabla hata sijajifungua Junior.

Hii ni tabia ya wanawake wenye kiherehere ambacho baadaye huja kuwatokea puani.

Hudhani wakiwaonyesha wenza wao ujumbe wanaotumiwa kwenye simu hasa unaohusu wakware wanaowataka ndiyo kujenga uaminifu.

Mapenzi au mahusiano yakiwa moto moto siku za mwanzoni hujifanya wao ni wasafi na wanataka kutumia simu pamoja na wenza wao kwa kuiacha bila nywila (password) na kuwalazimisha waangalie angalie vitu vyao wanavyotumiwa, ukiwamo ujumbe mfupi wanaotumiwa na wanaume wanaowatongoza.

Kinachotokea au wanachokitengeneza ni hamu ya mwanaume kutaka kusoma ujumbe wa namna hiyo unaotumwa katika simu, kila mara ili kujua nani kamtongoza mkewe au mpenzi wake na amejibiwa nini?

Binadamu siku zote hajakamilika, ni mtu wa makosa, wakati mwenza wako unamjengea kiu hiyo kuwa akirudi lazima aangalie nani amekupigia, umempigia, umetumiwa ujumbe gani, unahusu nini na nani, jiandae siku ukijikanyaga tu imekula kwako.

 Miongoni mwa wanaokutongoza yupo utakayeamua uwe naye au umchune hivyo hutamuonyesha mwenza wako na wala hutomzuia huyo mtu kuwasiliana na wewe, hapo ndiyo utakapojutia kiranga cha kutaka kutumia simu moja watu wawili.

Pia kuna watu tunawasiliana nao na kuzoeana nao, wahusika wanachukulia mazoea yao ya kawaida, lakini mtu mwingine hususani mwenza akiona mawasiliano yenu itakuchukua mwaka mzima kumueleza kuwa huyo mtu si mwanamume wako.

Kuna marafiki vichaa pia anaweza kuamka asubuhi akaanza kukuhadithia mikasa yake inayohusu mahusiano yake haramu unayoyajua kupitia simu.

Hapo akiziona mwenza wako jasho litakutoka kutoa maelezo hadi akuelewe.

Ndiyo utakumbuka kumpa simu yako ulikuwa unajipalia makaa mwenyewe, maana kila kinachotumwa itabidi uwe unakitolea maelezo.

Maana ukikutana naye jambo la kwanza ni kuomba simu, halafu salamu inafuatia, kwa taarifa yako ukikaa wiki moja hujampa sms ya mtu anayekutongoza, lazima akasirike atajua kuna kitu unamficha.

Hata kama umsafi kiasi gani, kuna namna nyingi za kuonyesha uaminifu badala ya kuwa mchonganishi.

Naam! Huu ni uchonganishi maana hujui mwenza wako ana uwezo kiasi gani wa kuzuia hasira zake, anaweza kumfuata aliyekutongoza na kugombana au hata kuuana kabisa.

Tabia hii naiita kiranga kwa sababu itafikia mahali utaona kero tena hutaki akague simu yako mara kwa mara, pengine siyo kwa mabaya, labda hutaki ajue kama una kikoba, wazazi wako wanakuomba fedha, migogoro ya familia yako mnayojadili katika makundi yenu.

Lakini utakuwa umeshachelewa, yaani huna haja ya kumueleza mumeo kitu maana anavijua vyote kupitia simu yako ambayo ameshazoea kuikagua atakavyo.

Katika mahusiano kuna vitu ambavyo ukiviacha hukosi ladha ya mapenzi na ukivifanya yapo palepale, hivi unapaswa kuvipunguza. Mwanamke kuwa na kiherehere kisichokuwa na macho wala miguu haipendezi sana.

Kuna mambo mengi ukifanya yatakuweka pazuri na mwenza wako, nakuambia ukimpikia vizuri, ukajituma faragha wala hatakumbuka kama huwa unachati na kutongozwa. Sasa ya nini kujipa jaka moyo.

Kila siku narudia mambo mengi katika mahusiano tunafanya kujichosha, la msingi ni moja, kumpa burudani ya uhakika katika sita kwa sita, anaweza kukufumania na akakusamehe.

Simu ni bomu, kila mmoja akae na lake ili likimlipukia lisiwe na madhara makubwa.


 Nikimpa vizuri analia, nikimnyima analia namuacha

Anti naona nibaki peke yangu mpaka nitakapopata mwenza mwingine, huyu niliyenaye nahisi ana matatizo ya akili lakini hataki kukubali.

Nipo naye huu mwezi wa tisa, ila naona ipo siku litakuja kuwa tatizo kubwa, kwani kila unachomfanya analia, ukichelewa kurudi, ukimpa vizuri, ukimtania pia anaweza kuamua kulia.

Kwa kawaida ni nadra sana kumuona mwanamume analialia ovyo, ila huyu wangu hapana, nahisi kuna shida kichwani mwake, analia mara nyingi kuliko anavyonipa raha.

Nikimuudhi analia, akiudhi analia. Ilimradi siku zote tupo msibani. Ninajua unaposoma unapata picha ya mtu wa hovyo labda asiyejua anafanya nini, basi kwa kazi anayofanya pengine amewahi kukuhudumia na kukuponya, maana ni mtaalamu kwenye fani yake, tena mbobezi, nadhifu, mrefu ana rangi ya huzurungi, akivaa anapendeza, shida yake vilio.

Nimejaribu kuwashirikisha rafiki zake aliosoma nao chuo na kukaa nao hosteli kwa zaidi ya miaka minne, wananishangaa wanasema hakuwa na tabia hiyo.

Nimemueleza labda kuna kitu kinamuanza kichwani twende hospitali, hapo napo ninaweza kuanzisha kesi mpya itakayozaa kilio. Sasa nashindwa nifanye nini, ninawaza hadi nimepungua mwili, ninampenda nahisi pia ananipenda kwa sababu ana huruma na ananijali sana. Sijui nifanyeje labda unishauri, kuna wakati nahisi atakuja kuninyonga kilio kikimnogea.

……Dah! Nakosa hata cha kusema, mwanamume kulialia bila sababu za msingi siyo kawaida kama ulivyosema.

Bora angekuwa analia tu mnapokuwa faragha ningesema unampatia sana, lakini kila mara hii inatia mashaka.

Inawezekana anakupenda sana kiasi kwamba hajielewi akiwa na wewe anajiona ni mwenye bahati hadi anaishia kulia.

Ila ninaungana na wewe kuwa kuna shida mahali, hatuwezi kuwa na uhakika na hili hadi akapimwe, hivyo washirikishe ndugu zake anaowaheshimu lakini wenye nasaba unayoweza kuwaeleza mambo ya kwenye ndoa kama shangazi, bibi, dada mkubwa na shemeji ili mtafute suluhisho la pamoja, hii si akili ya kawaida, pengine ana kitu kinamsumbua.