Uteuzi huu Udart, Dart ulete manufaa

Miongoni mwa uteuzi alioufanya Rais Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa wiki, ni wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), Waziri Kindamba.

Kindamba ameteuliwa kushika nafasi hiyo akitoka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, na kabla ya hapo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, nafasi aliyoishika akitokea kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Kindamba ameteuliwa ikiwa imepita miezi miwili tangu Rais Samia kumteua Athuman Kihamia kuwa Mtendaji Mkuu mpya wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART). Teuzi hizi zimekuja wakati eneo hilo likigubikwa na changamoto nyingi. Awali ilitarajiwa kuwa usafiri wa mabasi hayo ungeleta ahueni kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini matarajio hayo yameyeyuka na umekuwa na changamoto nyingi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni ubovu wa mabasi, upotevu wa mapato kutokana na mifumo isiyo ya tija ya ukusanyaji wake. Changamoto ya ubovu wa mabasi si tu inapunguza idadi ya mabasi hayo, bali pia inaongeza ukubwa wa tatizo, kwani mabasi yaliyosalia hayatoshi na mengine mengi mabovu yanazidi kulundikana yakisubiri vipuri.

Hali hiyo imekuwa ikisababisha abiria waliokata tiketi kukaa vituoni kwa muda mrefu wakisubiri mabasi, hali inayopoteza maana ya ‘haraka’ katika mradi huo.

Matokeo yake watu wameamua kurejea kwenye mabasi ya daladala za kawaida, bajaji na wengine wakitumia pikipiki na magari ya kukodi kwa gharama kubwa ili kuwahi kwenye shughuli zao za kila siku.

Wakati hayo yakiendelea, Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka, na tayari Barabara ya Kilwa hadi Mbagala imeshakamilika, lakini haina mabasi ya kuingiza kwenye njia hiyo.

Kama changamoto ya upungufu wa mabasi itaendelea, maana yake hata huo ujenzi wa miundombinu ya usafiri huo utakuwa hauna maana yoyote.

Kwenye upotevu wa mapato, inaelezwa kuwa ni kutokana na kukatisha tiketi kwa mkono badala ya njia ya kielektroniki iliyotarajiwa.

Tunadhani, huu ni wakati wa watendaji walioteuliwa kuonyesha uwezo wao kwa kukabiliana na changamoto hizo ili kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwa mradi huo yanatimia.

Kwa mfano, katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa mabasi, UDART inapaswa kuhakikisha mabasi mabovu yanakarabatiwa yote kwa wakati na mengine mapya yananunuliwa kutosheleza mahitaji.

Inawezekana ukarabati huo ukagharimu fedha nyingi, na hapo ndipo linapokuja suala la udhibiti wa mapato, kwa kuhakikisha unapatikana mfumo wa kielektroniki utakaowezesha ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wa DART, viangaliwe vigezo vya kisheria, itafute washindani kutoka sekta binafsi ili waingize mabasi yao na mtaji katika miundombinu ambayo tayari ipo na inayoendelea kujengwa, ili kutoa huduma shindani na bora kwa wananchi.

Ni vizuri pia kujifunza kwa mataifa mengine yanayotekeleza miradi kama huu na kuangalia wapi walifanikiwa na walifanyaje kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.

Serikali pia iziwezeshe DART na UDART kisheria na kifedha kutekeleza majukumu yake, maana huwezi kuwahukumu bila kuangalia mambo yanayowakwaza.