Mambo matatu yamsubiri Kindamba Udart

Muktasari:

  •  Mkurugenzi mpya anatakiwa pia kuboresha huduma za usafiri wa mabasi na kukabiliana na changamoto za ukosefu wa fedha na usimamizi duni katika kampuni.

Dar es Salaam. Udhibiti wa mianya ya wizi wa makusanyo ya fedha na kutegua kitendawili cha mkwamo wa vipuri vya mabasi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  ni sehemu ya mzigo unaomkabili Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Waziri Kindamba.

 Mengine yanayosubiri utendaji wake ni kuboresha huduma za usafiri wa mabasi hayo, ambazo kwa sasa zimegubikwa na malalamiko kutoka kwa wananchi.

Waziri Kindamba anakabiliwa na majukumu hayo, baada ya juzi Rais Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa Mkurugenzi wa Udart, akichukua nafasi ya Gilliard Ngewe ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Kindamba anakuwa Mkurugenzi wa nne ndani ya Dart tangu ilipoanzishwa. Aliyeanza ni Charles Newe, alifuatiwa na John Nguya, kisha Ngewe na sasa ni Kindamba.

Hata hivyo, utendaji katika nafasi hiyo Udart,  unatajwa kukwamishwa na changamoto zilizopo, ikiwemo wizi uliokithiri wa makusanyo unaosababisha kukosekana fedha za kuboresha huduma kama ambavyo Mwananchi Digital limearifiwa.


Kulingana na chanzo cha taarifa hiyo, kikwazo kingine cha utendaji katika kampuni hiyo ni mkwamo wa mzigo wa vipuri vya mabasi hayo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Changamoto zilizopo

Chanzo  cha kuaminika ndani ya Udart, kinaeleza ubovu wa mabasi na kupotea kwa mapato kulikokithiri ndilo jinamizi linaloikabili kampuni hiyo.

Kulingana na chanzo hicho, katika kampuni hiyo yenye mabasi takriban 200, karibu nusu yake  hayatembei, yakiwa  yameegeshwa kwa sababu ya ubovu.

Hali hiyo, chanzo kinaeleza inasababisha kudorora kwa huduma, kwa kuwa idadi ya mabasi hailingani na mahitaji halisi, kikisisitiza: "...hapo ndipo malalamiko ya abiria yanapoanzia."


Mkwamo wa vipuri TRA

Lakini yote hayo, mzizi wake, chanzo kinasema ni kukwama kwa makontena ya vipuri vya mabasi hayo, jambo linalokwaza ufanyikaji wa matengenezo kwa yale yaliyoharibika.

"Unaangalia utapata wapi fedha ya kununua vipuri wakati vilivyopo vimezuiliwa na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania)," kinasema.

Chanzo hicho kinaweka wazi vipuri vilivyozuiwa TRA, ni vya mabasi 140 na kwamba iwapo vingeachiwa na kuanza kutumika, angalau mabasi 50 yangefanyiwa matengenezo.

Kilipoulizwa chanzo hicho kueleza sababu za mkwamo wa vipuri hivyo TRA, kilidokeza kwa ufupi kuwa, "ni misunderstanding (hali ya kutoelewana."

Hata hivyo, chanzo hicho hakijaweka wazi ni nani aliye katika hali ya kutoelewana na TRA kiasi cha kusababisha mkwamo wa vipuri hivyo.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi (TRA), Richard Kayombo hakupatikana mara kadhaa jana alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia sakata hilo. Simu ya Kamishna Mkuu TRA, Alphayo Kidata iliita bila kupokewa.


Kauli ya Tamisemi

Alipotafutwa kuzungumzia mkwamo wa vipuri hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amekiri uwepo wa jambo hilo.

Pamoja na kukiri, Mchengerwa amesema mazungumzo yanaendelea kati ya TRA na wizara hiyo kukwamua mkwamo huo.

"Tunaendelea na mazungumzo kuona namna ya kuliweka hilo vizuri," alijibu kwa ufupi akidokeza kuwa yupo  kikaoni.


Mapato kuvuja

Katika mazingira hayo, chanzo hicho kinabainisha bado kuna upotevu uliokithiri wa mapato, unaosababishwa na wizi katika mfumo wa ukusanyaji nauli.

"Mfumo wa ukusanyaji mapato ni manual (ni wa mikono) wale wahudumu wanaamua wanachokitaka, anaweza kumpa abiria tiketi ya mwanafunzi ya Sh200, ilhali ni mtu mzima aliyelipa Sh650, kwa hiyo iliyobaki mkusanyaji anaweka mfukoni," amesema.

Kutokana na mfumo uliopo, chanzo hicho kinaeleza ni vigumu kumkamata yeyote na haiwezekani kusimamia wasiibe.

Chanzo hicho kinaeleza suluhu pekee ya uvujaji unaoendelea ni kubadili mfumo kutoka wa sasa na kutumia kadi, ili kusiwe na utaratibu wa kupokea fedha mkononi.

Kinachoshangaza chanzo hicho, kimesema uamuzi wa kutumia mfumo huo umekuwa kizungumkuti.

Kinaweka wazi kuwa, kulikuwepo makubaliano kati ya Udart na Dart Desemba mwaka jana, juu ya utaratibu wa matumizi ya kadi uanze, lakini kilichofanyika ni kusaini mkataba na mkandarasi wa kuifanya kazi hiyo pekee.

"Desemba kilichofanyika ni Dart kusaini mkataba na mkandarasi wa mfumo huo na hadi sasa haujaanza," amesema.


Ilichokisema Dart kuhusu mfumo

Alipotafutwa kuzungumzia hatua za mabadiliko ya mfumo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka ( Dart), Athuman Kihamia,  amesema tayari kadi 200,000 zimeshanunuliwa tangu Februari mwaka huu, kwa ajili ya mfumo huo.

Sambamba na kadi hizo, Kihamia amesema kazi iliyobaki ni utengenezaji wa mageti janja, kazi ambayo inafanywa na mkandarasi kutoka Italia.

"Matarajio yetu ni mwezi huu Machi au mwanzoni mwa Aprili kazi hiyo itakamilika na mfumo wa kadi utaanza kutumika," amesema.


Kibarua mkurugenzi mpya Udart

Chanzo hicho kilipoulizwa kuhusu nini anapaswa kufanya Mkurugenzi mpya wa Udart, kimesema ni kuhakikisha anafanikisha kufufua mabasi mabovu yaingie barabarani kufanya kazi.

Lingine litakalorekodiwa kama mafanikio kwa mkurugenzi mpya, chanzo hicho kilieleza ni kuhakikisha abiria wanasafiri kama ilivyotarajiwa.

Jambo lingine, kimesema ni kudhibiti mfumo wa ukusanyaji mapato.


Malalamiko ya wananchi

Msingi wa malalamiko ya wananchi wengi, ni uchache wa mabasi hayo unaowasababishia kukaa muda mrefu vituoni bila kupata huduma.

Malalamiko mengine dhidi ya mradi huo, ni utaratibu wa baadhi ya mabasi kupitiliza vituoni bila kupakia, ilhali abiria wamesongamana.

Kutokana na hayo, wananchi wamedai ile tafsiri ya mabasi yaendayo haraka imepoteza uhalisia,  kwa kuwa wanatumia muda mwingi kupata huduma kwenda kazini na kurudi nyumbani.

Malalamiko hayo yaliwahi kufika hata kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na hivyo Aprili mwaka 2021 alifanya ziara ya kustukiza katika mradi huo.

Pamoja na mambo mengine, akiwa katika karakana ya mabasi hayo, Jangwani jijini Dar es Salaam, Majaliwa alieleza kukerwa na usimamizi mbovu wa mradi huo.

Alipofika katika karakana hiyo, Majaliwa alikuta mabasi 40 kati ya 140 yameharibika na hakukuwa na fedha ya kufanyia matengenezo.

"Ukosefu wa fedha ndani ya Udart umechangia kushindwa kununua baadhi ya vifaa vya kukarabati mabasi 40 yaliyoharibika sababu ni usimamizi mbaya," alisema.

Katika ziara yake hiyo, Majaliwa alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha na Maendeleo ya Biashara wa Udart, Suzana Chaula kwa kushindwa kusimamia vema makusanyo.

Tangu wakati huo, mradi wa mwendokasi umebaki kulalamikiwa na watumiaji, wengi wakisema hakuna mpangilio mzuri wa matumizi ya mabasi, kazi ambayo vyanzo vyetu vinasema ndicho kibarua cha bosi mpya Kindamba na pia kinaweza kuwa ndiyo kitanzi chake.