Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vipimo kwa mabondia viwe lazima nchini

Wiki iliyopita, gazeti hili lilichapisha ripoti maalum ya uchunguzi kuhusu vipimo vya afya kwa mabondia kabla na baada ya kupanda ulingoni.

Uchunguzi huo ulibaini kwamba idadi kubwa ya mabondia nchini wamekuwa hawafanyiwi vipimo muhimu kama MRI na CT Scan na hivyo kuwaweka hatarini katika kazi yao.

Vipimo hivyo viwili kwa mujibu wa madaktari havipaswi kuepukwa na mabondia kulingana na aina ya mchezo ambao wanashiriki.

Kupitia vipimo hivyo wanaweza kugundua majeraha ya ubongo, uvujaji damu, uvimbe au nyufa za fuvu ambazo haziwezi kuonekana kwa uchunguzi wa kawaida.

Bondia mwenye jeraha la zamani anaweza kuonekana mzima, lakini akipokea pigo jingine linaweza kuzidi na kusababisha ulemavu wa kudumu au kifo.

Ni kupitia vipimo daktari anaweza kuamua kama bondia yuko salama kupanda ulingoni ama anahitaji matibabu au mapumziko zaidi.

Pia badala ya kutibu dalili kwa dawa za maumivu pekee, vipimo vinaonyesha chanzo halisi cha tatizo ili matibabu yafanyike kwa usahihi.

Mchezo wa ngumi ni wa hatari na unahusisha mapigo yanayoelekezwa kichwani, sehemu ambayo ikipata majeraha au mtikisiko inaweza kugharimu maisha ya bondia au kumpatia ulemavu wa kudumu.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, kila mwaka wastani wa mabondia 13 hupoteza maisha kutokana na matatizo yatokanayo na vipigo.

Kuliwahi kutolewa ripoti kwamba kuanzia 1890 hadi 2011, idadi ya mabondia 1,604 walifariki kutokana na majeraha waliyopata ulingoni.

Hivyo vipimo hivyo vya CT Scan na MRI ni lazima vifanywe kwa mabondia ili kulinda uhai na usalama wa maisha yao.

Hoja kubwa ambayo inatolewa na mabondia na mapromota ni kwamba vipimo hivyo ni gharama kubwa ndio maana wahusika wanashindwa kuvifanya kabla au baada ya kupanda ulingoni kupigana.

Hata hivyo madhara ya kutofanya yanaweza kuwa makubwa zaidi ya hata hizo gharama ambazo mabondia na mapromota wanazikwepa kwa kisingizio kwamba ni kubwa.

Kutokana na hilo, ni vyema serikali kwa kushirikiana na Kamisheni ya kusimamia ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC) zikaongeza ukali katika suala la vipimo kwa mabondia na kuweka miongozo itakayolazimisha mtu asipande ulingoni bila kupira katika MRI na CT Scan.

Yapo mambo ambayo busara inaweza kutumika katika kuyashughulikia lakini sio kama hili ambalo linagusa moja kwa moja maisha na uhai wa watu.

Tunategemea kuona kanuni na miongozo ambayo itawalazimisha mabondia kupimwa na ambaye ataonekana hayuko tayari kufanya hivyo, basi azuiwe kupigana na vibali vyake vizuiwe.

Sehemu ya fedha ambazo bondia anapata, itumike katika kugharamia vipimo hivyo kwani vina faida kwa yeye mwenyewe.

Wakati hilo likifanyika, pia juhudi zifanyike ili kuwepo na unafuu wa gharama za vipimo hivyo.