Prime
Waraka wa Rostam Aziz kushamiri matukio ya utekaji, mauaji Tanzania
Katika siku za karibuni nchi yetu imeshuhudia kujirudia tena kwa matukio ya kikatili ambayo yamehusisha kuripotiwa kwa vitendo vya utekaji, utesaji na jana Jumapili Septemba 8, 2024 tukashuhudia tukio baya zaidi la mauaji ya kiongozi wa Chadema, Ali Mohamed Kibao.
Naungana na Watanzania wema wote kutoa mkono wa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na viongozi na wanachama wa Chadema kwa msiba huo wenye kuhuzunisha sana.
Nimetiwa moyo sana na taarifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambapo alieleza kusikitishwa kwake na mauaji hayo na kutoa pole kwa wafiwa na wakati huohuo kuagiza uchunguzi wa haraka wa tukio hilo na mengine kama hayo.
Rais Samia hakuishia hapo, bali alitoa ujumbe mzito kwa kusema kuwa: "Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii."
Namuunga mkono Rais wetu ambaye kwa nafasi yake ndiye Mfariji Mkuu wa Taifa (Comforter-in-Chief) kwa kujitokeza na kuwafariji wafiwa na Watanzania na kuwatangazia hatua za mara moja ambazo amezichukua, ili kukomesha ukatili huu.
Rais wetu siku zote ametuthibitishia kwa maneno na vitendo kuwa kamwe hakubaliani na matendo ya aina yoyote ya kuumizana ama kutotenda haki. Amejipambanua kuwa ni muumini thabiti wa haki kamili za kila binadamu.
Nikiwa raia wa Tanzania, ambaye nimeitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali za uongozi na ambaye nililelewa katika Taifa linalothamini tunu za utu na thamani ya ubinadamu wetu chini ya misingi ya uhuru na haki, nawaomba Watanzania wenzangu sote tuungane kukataa kurudishwa kwenye zama za giza ambapo utu na maisha ya mtu vilionekana havina thamani.
Naomba sote tuungane na Rais wetu kuhakikisha vitendo vya kishetani vya aina hii vinakomeshwa na havirejei tena katika nchi yetu. Sote tusimame pamoja kuona Taifa letu linarudi katika misingi yake ya utu, uhuru na haki iliyojengwa na waasisi wake.
Rostam Aziz ni mfanyabiashara ndani na nje ya Tanzania